Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) imesema inafanya uchunguzi kujua sababu zinazofanya baadhi ya vituo vya mafuta vya kampuni za Total Tanzania Limited na Oryx Oil Company Limited, kutouza bidhaa hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Haruna Masebu, alisema hayo jana baada ya kuelezwa na waandishi wa habari kwamba, kuna vituo vya kampuni hizo, ambavyo haviuzi mafuta.
Vituo hivyo vilivyoko maeneo mbalimbali nchini, takriban wiki sasa, vimekuwa vikishuhudiwa kutouza mafuta licha ya kampuni za mafuta kurejea kuuza bidhaa hiyo baada ya kusitisha mgomo.
Masebu alisema vipo baadhi ya vituo vya kampuni hizo vinavyouza mafuta na pia upakiaji wa mafuta kwenye matenka kutoka kwenye maghala kwa ajili ya kuingizwa sokoni, unaendelea kufanywa na kampuni hizo.
Hata hivyo, alisema wamejipa muda kuchunguza ili kujua sababu zinazofanya vituo, ambavyo haviuzi mafuta, kutofanya hivyo, badala ya kukimbilia kuviadhibu kwa vile adhabu yake ni kali.
Alisema hatua ya Ewura kutangaza marekebisho ya bei ya mafuta juzi, haina uhusiano wowote na mgogoro uliokuwapo kati ya mamlaka hiyo na wafanyabiashara ya mafuta, bali ilikuwa ni kuendeleza utaratibu wao wa muda mrefu.
Masebu alisema utaratibu huo umekuwa ukitekelezwa na Ewura kwa miaka mitatu mfululizo, kwa kutumia fomula mpya ya kukokotoa hesabu za vitu vyote vinavyohusiana na mafuta ili kupata bei elekezi/kikomo kwa kuzingatia thamani ya Shilingi ya Tanzania na bei ya bidhaa hiyo katika soko la dunia.
Kuhusu akiba ya mafuta, alisema mabadiliko ya bei kama ilivyo kwenye kodi, huanza kutumika wakati inatangazwa bila kujali akiba iliyopo.
“Kwa hiyo wafanyabiashara mara nyingine wanafaidika, na mara nyingine wanapata hasara,” alisema Masebu.
Alisema suala la mafuta yaliyomo kwenye maghala lina sura mbili; ya kwanza ikiwa ni bei mpya, ambayo inamrudishia mtaji aliyewekeza kwenye akiba alizonazo, na ya pili, ni bei, ambayo inatakiwa imuwezeshe kuwa na mtaji wa kutosha kuagiza shehena nyingine kwa bei itakayokuwapo kwenye soko wakati anaagiza.
Masebu alisema endapo bei haitatosha, mwekezaji huyo hataweza kuagiza upya na mzunguko wa biashara utakwama na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya mafuta kwenye soko la ndani.
Pia alisema endapo akiba zingekuwa ni kigezo cha ukokotoaji wa bei ya mafuta, ingebidi kila wakati kuhakiki kwenye maghala na vituo nchi nzima kabla ya kutangaza mabadiliko ya bei, zoezi ambalo alisema ni gumu na siyo utaratibu wa biashara ya mafuta duniani kote.
“Kimsingi hizo ndizo sababu zilizofanya kukubaliana kutoa bei mpya kila baada ya wiki mbili,” alisema Masebu.
“Kwa mfano, katika toleo la bei za mafuta zilizoanza kutumika Jumatano ya tarehe 8 Juni 2011, bei za mafuta zilishuka kwa asilimia 4.30 kwa petroli, asilimia 4.8 kwa dizeli na asilimia 5.71 kwa mafuta ya taa. Kushuka huko kwa bei za mafuta kulihusisha pia mafuta yaliyokuwa kwenye akiba,” aliongeza.
MAFUTA YA TAA,DIZELI ADIMU DAR
Katika hatua nyingine, licha ya Ewura kutangaza bei mpya ya mafuta, baadhi ya vituo vimeshuhudiwa vikiwa havina mafuta ya dizeli na taa.
Uchunguzi uliofanywa na NIPASHE umebaini vituo vingi vikiwa vinauza mafuta ya petroli pekee, huku vituo vya kampuni ya Total vikishuhudiwa vikiwa vimesitisha kutoa huduma hiyo kwa madai ya kuishiwa na bidhaa hiyo.
Baadhi ya vituo vya kampuni hiyo vilishuhudiwa jana vikiwa haviuzi mafuta, huku vikionekana vikiwa vimezungushiwa kamba na wafanyakazi wake wakiwa wameondoka eneo la kazi.
Mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha Total kilichopo eneo la karibu na Mlimani City, ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini, alisema wameishiwa na mafuta tangu juzi na kwamba, tayari magari yameenda kufuata katika ghala.
“Mafuta yametuishia tangu juzi. Ila huenda leo (jana) jioni tukaletewa kwani tumeambiwa magari yameenda kuchukua katika ghala la mafuta,” alisema.
Vituo, ambavyo vilikutwa vinatoa huduma ni vya kampuni za Engen, Oilcom na Gapco, TSN (Bamaga), Big Bon (Sinza), Camel Oil (Africa Sana), Oilcom (Sokota) na Lake Oil vilivyopo karibu na soko la Urafiki, maarufu kama “Big Brother”.
Vingine ni Mt Meru (Tabata), Oilcom (Tabata Relini), Oryx (Posta) na GBP (Kilwa Road-Temeke).
Baadhi ya vituo vilikuwa vinauza petroli pekee, huku wafanyakazi wake wakidai kuishiwa na dizeli mafuta ya taa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment