Serikali imesema itaunda mamlaka itakayosimamia uendelezaji wa Mji Mpya wa Kigamboni katika mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Hayo yalisemwa jana bungeni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa, Anne Tibaijuka, wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio na matumizi ya kwa mwaka 2011/2012.
Alisema mamlaka hiyo itaandaa mipango ya kina ya ujenzi wa miundombinu, itafanya uthamini wa mali na kutayarisha maeneo mbadala na makazi kwa ajili ya wananchi watakaolazimika kuhama maeneo yao ya sasa na kwenda katika maeneo mapya, lakini ndani ya eneo hilo hilo la Kigamboni.
“Wizara kwa kushirikiana na na Wizara ya fedha itaendelea na juhudi za kutafuta fedha kwa ajili ya kulipa fidia stahiki kwa wananchi,” alisema na kuongeza mamlaka hiyo mpya itatumia mbinu za kisasa kupata fedha za kutosha za kulipa fidia.
Alitoa mfano wa njia hizo ni kutangaza municipal bond’ ili wananchi wenye uwezo wachangie gharama hizo kwa kujipatia hisa katika eneo hilo litakalokuwa la kisasa.
Aliwaomba wananchi hao kuendelea kuwa wavumilinu wakati jitihada zikiendelea kufanyika kukamilisha zoezi hilo la kwanza kipekee nchini .
“Napenda kuwakumbusha wananchi kuwa ni ukiukaji wa sheria ya MipangoMiji kujenga katika eneo la Mpango kabambe wa Mji Mpya wa Kigamboni bila kuwa na kibali halali cha ujenzi, kwani maendelezo yatakayofanyika kinyume na sheria hayatatambulika wala kutolewa fidia,” alisema.
Wakati huo huo, Profesa Tibaijuka alisema kuwa wamedhamiria kurejesha kada ya askari ardhi (Land Ranger) katika muundo wa halmashauri zote nchini.
Alisema katika mwaka wa fedha 2011/2012, wizara itashirikiana na halmashauri za manispaa zote za Jiji la Dar es Saalam na itaratibu kazi za askari ardhi wa muda ambao wameshaanza kazi jijini Dar es Saalam, ili kudhibiti ujenzi holela.
Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa askari hao ambao watawezesha wizara na halmashauri kudhibiti ujenzi holela na uvamizi wa maeneo ya umma.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment