ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 2, 2011

Hatma ya Moshi, Mwaikimba kwa Poulsen

kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen
Calvin Kiwia
SHIRIKISHO la soka Tanzania, TFF linasubiri taarifa kutoka kwa kocha mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen ili liweze kuwachukulia hatua za kinidhamu wachezaji Haruna Moshi (Simba) na Gaudence Mwaikimba (Moro Utd) kwa kukaidi wito wa kuichezea U-23.

Wachezaji hao wawili waliteuliwa na Poulsen kujiunga na kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana chini miaka 23 kwa ajili ya kutazama viwango vyao vya soka ili aweze  kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachoingia kambini kujiandaa na pambano lake dhidi ya Algeria katika kusaka tiketi ya kucheza fainali za mataifa ya Afrika mwakani huko Gabon na Ikweta ya Guinea.

Ofisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema jana kuwa wanasubiri taarifa kutoka kwa kocha Poulsen ili waweze kuwachukulia hatua za kinidhamu wachezaji hao na kuwa fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

"TFF tukiwa kama wenye dhamana ya kusimamia mpira Tanzania hatuwezi kulifumbia macho suala hili lazima hatua kali za kinidhamu zichukuliwe juu yao kwa kitendo hicho cha utovu wa nidhamu walichomwonyesha kocha," alisema Wambura.

Alisema TFF watakutana na kocha Poulsen pamoja na wachezaji hao kwa ajili ya kujadili suala hilo na endapo watakosa sababu zinazojitosheleza na kuonekana walikaidi wito huo, adhabu kali juu yao itatolewa.

Hata hivyo kocha wa Simba, Moses Basena alipopata taarifa hizo alisikitishwa na mchezaji wake Haruna Moshi kushindwa kuitikia wito huo na kusema hawezi kuelezea sababu hasa zilizomfanya kushindwa kujiunga na timu hiyo kutokana na kumpatia ruhusu ya kujiunga na timu hiyo.

"Kwa kweli sina sababu rasmi ambazo naweza kueleza zilizomfanya Boban kushindwa kujiunga na timu ya Vijana U-23 kwa sababu aliniomba ruhusu nami nikampatia ghafla akarejea na kusema hawezi kujiunga na timu hiyo," alisema Basena.

Naye kocha wa Moro Utd, Hassan Banyai alikiri kuwa mshambuliaji wake Gaudence Mwaikimba alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria.

"Gaudence alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa malaria hata mchezo wetu dhidi ya Azam FC hakuweza kucheza kutokana na kuwa mgonjwa," alisema Banyai.

Wachezaji ambao walioitikia wito wa Poulsen kujiunga na kikosi cha timu ya Taifa ya U-23 ni Salum Machaku (Simba) na Juma Seif 'Kijiko' (Yanga) ambaye anapewa nafasi kubwa ya kujumuishwa kwenye kikosi hicho kutokana na kuonyesha  kiwango cha hali ya juu kwenye mechi hizo mbili dhidi ya Shelisheli zilizofanyaika jijini Arusha.


Mwananchi

No comments: