ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 6, 2011

Igunga ni uwanja wa vita CCM, Chadema


Mweka Hazina CCM aeleza mikakati yao
  Kamati Kuu ya Chadema yakutana kuamua
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa
Harakati kubwa za kujipanga kwa ajili ya kuwania kiti cha ubunge cha Jimbo la Igunga kilichoachwa wazi na mbunge wake, Rostam Aziz, aliyejiuzulu mwezi uliopita, zinaelekea kuwa baina ya vyama viwili vya siasa ambavyo kwa sasa vimekwisha kutoa kauli zao kuliwania.
Ikiwa ni siku moja tu baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza kuwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo utafanyika Oktoba 2, mwaka huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ndivyo vimeonyesha dhahiri kukamia kiti hicho. Kaimu Mkurugenzi wa NEC, Dk. Sisti Cariah,
katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, alisema kuwa uteuzi wa wagombea utafanyika Septemba 6 na kampeni zitaanza Septemba 7 kisha uchaguzi kufanyika Oktoba 2, mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, uwekaji wa Daftari la Kudumu la wapiga Kura utafanyika kuanzia Septemba 22, mwaka huu katika vituo walivyojiandikisha wapiga kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 na zoezi hilo litafanyika kwa siku saba.

KAMATI KUU CHADEMA KUJADILI LEO
Katika kujiandaa na uchaguzi huo, Kamati Kuu ya Chadema, leo inakutana mjini Dodoma ambapo pamoja na mambo mengine, itajadili jinsi ya kulichukua Jimbo la Igunga.
Akizungumza na NIPASHE jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema kwamba uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Igunga ni moja ya ajenda zitakazopewa uzito katika kikao hicho kikuu cha chama hicho.
Dk. Slaa alisema ajenda ya kujipanga kwa ajili ya uchaguzi wa Igunga itajadiliwa na Kamati Kuu kwa kuwa tayari NEC imetangaza mchakato wa uchaguzi huo na kupanga ratiba. Alisema kuwa mbali na kikao hicho kujadili namna ya kulitwaa Jimbo la Igunga, pia watajadili hali ya kisiasa inavyoendelea nchini.
“Kwa chama makini kama kilivyo cha kwetu, kila inapokutana Kamati Kuu, huwa ni lazima ijadili ajenda ya kila siku kwenye vikao vyake ambayo ni hii ya kuangalia hali ya siasa inavyoendelea nchini na kisha kutoa msimamo wa chama kuhusiana na jambo hilo,” alisema.
Aidha, Dk. Slaa alithibitisha kuwa suala linalowahusu madiwani wa chama hicho walioandikiwa barua ya kuachia nafasi zao walizopewa ikiwemo ile ya Unaibu Meya katika Halmashauri ya Jiji la Arusha baada ya mwafaka walioufikia na madiwani wa CCM, litakuwa ni sehemu ya ajenda za kikao hicho.

CCM YATAMBA KUSHINDA
Wakati huo huo, CCM kimemkabidhi Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Uchumi na Fedha), Mwigulu Nchemba, kikosi cha kampeni kwa ajili ya uchaguzi huo. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Nchemba alisema ingawa kampeni hizo zitashughulikiwa na kamati za siasa za ngazi ya kata, wilaya na mkoa wa Tabora, lakini yeye ataongoza kikosi cha taifa katika kampeni hizo.
Nchemba alitamba kwamba, CCM haina kitu cha kuhofia katika uchaguzi mdogo wa Igunga unaotarajiwa kufanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa na Rostam, ambaye alijiuzulu wadhifa huo sambamba na ujumbe wa NEC ya CCM Julai 13, mwaka huu kwa madai ya kuchoshwa na siasa uchwara na za kuchimbana.
“Niwaambie hatuna hofu ya uchaguzi mdogo Igunga…kama kuna anayebisha kuwa CCM haitashinda, tuwekeane dau, lakini namhurumia kwa sababu nitamlia pesa yake. Tunakwenda kushinda,” alisema Nchemba.
Bila kufafanua zaidi, Nchemba alisema kuwa taarifa zaidi kuhusiana na kampeni za Igunga ikiwemo gharama zitakazotumiwa na chama hicho katika uchaguzi huu zitajulikana baadaye. Hata hivyo, Nchemba alisema kuwa gharama hizo hazitazidi Sh. milioni 600.
Huu ni uchaguzi mdogo wa pili kufanyika katika Jimbo la Igunga tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi. Wa kwanza ulifanyika mwaka 1994 ambao ulimwingiza madarakani Rostam mara baada ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi nchini mwaka 1992. Tangu wakati huo Rostam alikuwa mbunge wa jimbo hilo, mara nyingine akipita bila kupingwa. Kujiengua kwake kwenye nafasi hiyo kunaelezwa kuacha hali ya kisiasa inayotarajiwa kuleta ushindani mkubwa miongoni mwa vyama.
Katika hatua nyingine, Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi kwa tiketi ya chama hicho aliitaka jamii kutokubali kuburuzwa na vyama vingine vya siasa kwa maslahi ya watu wachache wenye mwelekeo wa kulazimisha kushika madaraka kwa nguvu.
Alidai lengo zaidi la maandamano yanayofanywa na Chadema, si kutoa taarifa wala kuikosoa serikali, bali yana lengo la kuvunja amani.
CHANZO: NIPASHE

No comments: