ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 25, 2011

Ikibidi, mpenzi wako asiiguse kabisa simu yako!-2



WIKI iliyopita mtakumbuka nilianza kuzungumzia mada iliyokuwa na kichwa cha habari hicho hapo juu. Ni mada iliyonifanya nipokee simu na meseji nyingi kutoka kwa wasomaji wangu, hicho ndicho nilichokuwa nakitaka.

Kikubwa tujadiliane halafu mwisho tupate ufumbuzi wa tatizo hili. Mimi nirudie tena kusema kwamba, ikibidi tusiziguse kabisa simu za wapenzi wetu.

Faida ya kufanya hivyo ni kubwa na ukitakata kuijua, zungumza na wale ambao wamekuwa na tabia ya kupekua simu za wapenzi wao kila mara, wengine inafika hatua wanajuta kwa nini wazilishika.

Simu ni kitu cha ajabu sana na ile habari ya kwamba wengi wameachana kwa sababu ya chombo hicho cha mawasiliano ingetosha kuwafanya wapenzi wanaopendana kwa dhati na kuaminiana kupeana uhuru wa simu zao.


Labda niseme tu kwamba, wanaopenda kushikashika simu za wapenzi wanaashiria mambo haya matano yafuatayo ambayo si mazuri:

Kwanza, wanaonesha hawawaamini kabisa wapenzi wao. Wanadhani wanaweza kusalitiwa kwa kutumia chombo hicho. Kama kweli unampenda jenga mazingira ya kumuamini.

Kitendo cha wewe kumfuatilia mpenzi wako kupitia simu yake ya mkononi kinaonesha huna imani naye, mazingira yanayoweza kupunguza mapenzi kati yenu kwa kiwango kikubwa.

Pili, inaelezwa wale wenye tabia ya kuzisogelea simu za wapenzi wao mara kwa mara ni kama kuna kitu wanakitafuta na wengine hufikia hatua ya kusema, kugusa simu ya mpenzi wako unatafuta sababu ya kumuacha.

 Utaishika simu yake, mara inaingia meseji isiyoeleweka kutoka kwa mwanaume, mara mwanaume mwingine anapiga simu na  kukuambia mpenzi wako ni demu wake, wewe unachunwa tu.

Yawezekana ni jitu tu limepata namba ya mpenzi wako na linataka kukuchezea, ikitokea hivyo mara mbili au tatu, unaweza kuchukua hatua za kumpiga chini ukijua anakusaliti.Nasema hivyo kwa kuwa, kuna ambao yameshawakuta.

Tatu, hutaki kumpa amani mpenzi wako akiwa na wewe. Jiangalie na utabaini kuwa, kama una tabia ya kuichunguza simu ya mpenzi wako, kila unapokutana naye anakosa amani. Je, unataka kumkosesha amani kwa makusudi mpenzi wako? Kama jibu ni hapana, mwache na simu yake, kama anakusaliti mbona utajua tu bila hata kuigusa simu yake?

Nne, unataka mpenzi wako awe ni mtu wa kujieleza kwako kila saa. Itaingia sms sasa hivi, utamuuliza huyo ni nani, atakujibu. Atapigiwa simu, utamuuliza, atakujibu lakini kuna siku utakutana na sms za mapenzi kwenye simu yake, napo atakupa maelezo.

Hivi ukiwa na mpenzi wako hamna mambo mengine ya kufanya mpaka muutumie muda wenu kuulizana nani kakutumia sms, nani kakupigia? Jamani, vitu vingine ni kupoteza muda bure, hata kama ni suala la wivu lakini hii ni ‘too much’.

Tano, una nia ya kumfanya mpenzi wako ajutie kuwa na simu.Ana haki ya kujuta. Hivi kama kweli anakupenda na kila siku mkakorofishana kwa sababu ya simu, huoni atakuwa amefanya uamuzi wa busara kutokuwa na simu ili mdumu?
Nasema hivyo kwa sababu wapo watu huko mtaani wanajuta kuwa na simu, sababu ni kwamba, kila wakati wanakorofishana na wapenzi wao.

Kimsingi simu ni tatizo lakini itategemea na mapenzi yenu yalivyo. Kama mnapendana kwa dhati na kila mmoja anamuamini mwenzake, tusichunguzane kiivyo mpaka kufikia hatua ya kukoseshana amani.

Kama mpenzi wako hajatulia, Mungu atakusaidia utambaini kwa njia nyingine lakini si kwa kila saa kuigusa simu yake ukidhani itakusaidia kumlinda.

Kwa leo niishie hapo ila kama una lolote unataka kushea na mimi, tuwasiliane kwa namba za simu hizo hapo chini.

www.globalpublishers.info

No comments: