ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 24, 2011

Ili awe bora, tafuta kuwa bora kwanza!

HELLO ladies and gents! Mpo poa? Karibuni kwenye uwanja wetu tujadiliane kuhusu mapenzi. Yes,  tunazungumza kuhusu mapenzi. Nawashukuru wote mnaowasiliana nami kwa njia mbalimbali na kunipongeza, wengine kuomba ushauri n.k. Ahsanteni wote kwa ujumla wenu.

Marafiki zangu, katika uhusiano umakini wa hali ya juu huhitajika ili uweze kuwa bora kila siku na kuufanya uhusiano wako kuwa wenye nguvu na usiotetereka! Katika hili hutegemea zaidi jinsi unavyoendesha uhusiano wako.


Ukitaka mpenzi wako akuchoke au umchoke, wewe ndiye mwamuzi, lakini pia ukitaka mpenzi asikuchoke au usimchoke wewe ndiye mwenye uamuzi kwa kuwa una uwezo wa kuyafanya yote hayo.

Wengi hawaelewi kuhusu hili, anaingia kwenye ndoa na mke wake au mumewe lakini baada ya muda anajikuta mapenzi yakipungua siku hadi siku mpaka anafikia hatua ya kuwa na mwanaume mwingine nje ya ndoa au kama ni mwanaume anaamua kuwa na nyumba ndogo! Hayo yote nayaita ni mambo ya kujitakia!

Inawezekana ukaendelea kuwa bora kwa mpenzi wako, inawezekana mpenzi wako akaendelea kuwa bora kwako ikiwa utahitaji kufanya hayo kwa dhati. Hakika kama ukitaka unaweza kuendelea kuwa wa kisasa katika uhusiano wako.

Yapo mambo ambayo ukiyafanya kwa ufanisi mkubwa, basi wewe utaendelea kuwa bora kwake naye atakuwa bora kwako. Hakuna kuchokana tena. Je, unajua njia hizo? Unajua kitu cha kufanya? Twende kwenye vipengele hapo chini...

MLIANZAJE?
Siku zote nimekuwa nikisisitiza kuwa, jinsi unavyoanza ndivyo utakavyomaliza! Waswahili hawakuishia hapo, wakaongeza kuwa: “Unavuna kile ulichopanda!” Naamini katika semi hizo kuna mambo umejifunza.

Kama ulianza vibaya uhusiano wako tegemea kumaliza vibaya, lakini kama ulianza vizuri basi tarajia maisha mazuri ya kimapenzi yasiyo na maumivu katika moyo wako.

Kama unatarajia kuingia katika uhusiano na mpenzi mpya hakikisha hujionyeshi tofauti na hali yako halisi ilivyo. Jifunze kujikubali, hata kama unafanya kazi ambayo unadhani ni hadhi ya chini, mbainishe mpenzi wako hali halisi ilivyo. Kama anakupenda, kazi yako haiwezi kupunguza mapenzi baina yenu.

Kudanganya ni utumwa, usikubali kuingia katika utumwa au kifungo cha aina hiyo. Rafiki yangu mmoja alimdanganya mpenzi wake anafanya kazi katika shirika fulani kama kiongozi mkubwa, jamaa hakuishia hapo, akadai mshahara wake ni mkubwa na mambo mengine mengi.

Mpenzi wake kwa kuwa alijua boyfriend wake ana kazi na mshahara mzuri, alikuwa akimsumbua mara kwa mara amfanyie shopping! Kilichotokea hapo ni kwamba jamaa alikuwa akimkwepa kila kukicha. Unajua kwanini? Hana pesa.

Kama asingeongopa usumbufu wote alioupata usingetokea. Marafiki zangu, jifunzeni kujikubali mlivyo, msitake kujionyesha kwa watu mpo katika hadhi fulani kumbe hali halisi haipo hivyo, huo ni ulimbukeni ambao unatakiwa kuushinda.

Kwani kama jamaa angekuwa mkweli kwa mwanamke wake, angesumbuliwa kiasi kile? Inawezekana yule mwanamke alikuwa na mapenzi ya kweli kwa jamaa, lakini kichwani alikuwa akijua kuwa mpenzi wake mambo safi....sasa alikuwa na kosa gani kutaka shoopping? Fikiria zaidi.

JITHAMINI/JIKUBALI
Itakuwa kichekesho kama utasema unampenda mpenzi wako wakati wewe hujipendi! Huwezi ukasema unamthamini mpenzi wako wakati thamani yako mwenyewe huitambui.
Naamini tunakwenda sawa, kama unashindwa hata kuoga na kubadilisha nguo safi nani atakayekupenda? Huwezi kuwa wa kisasa kama huzingatii usafi, jithamini.

Mwingine anaweza kukuta anajichukia bila mwenyewe kujua. Unaweza ukamkuta mtu anajitoa kasoro mwenyewe, mara mimi mweusi sana mara mimi mweupe sana, miguu yangu imekaa upande, kwa nini nisingezaliwa kama fulani na maneno mengine yanayofanana na hayo. Amini ulivyoubwa hakuna makosa yoyoto, jinsi ulivyo unapaswa kuwa kama ulivyo.

Acha kujitoa makosa. Jipe moyo, wewe ni mzuri kuliko mwingine. Kikubwa zaidi ni kwamba, wewe utakuwa mzuri zaidi kwa yule ambaye anakupenda tu; ndiyo maan unaweza kusikia watu wanawasema wenzao walio kwenye mapenzi yao: “Mh! Jamani. Yule demu kampendea nini yule mshikaji hana lolote, sura ngumu, bangi tupu, mtaa mzima unamjua...”

Pamoja na maneno hayo, utakuta mapenzi yao ni motomoto na kila mmoja anamjali mwenzake, huku waswahili wakibaki na maneno yao. Upo?
Kujikubali ni silaha kubwa sana katika kuupa nguvu uhusiano wako na si uhusiano pekee, bali hata maisha kwa ujumla. Asiyejiamini na kujikubali, hawezi hata kujieleza.

Siku nzima atapoteza muda kwenye kioo akijikagua, mwisho anaweza kujitoa makosa hata jina lake!
Jiamini rafiki yangu, jithamini utakuwa mpya zaidi na bora kwenye uhusiano wako na maisha kwa ujumla.

Umenipata eeeh!? Haya basi, nimefurahi kama ndivyo. Dawa bado inaendelea, nafasi ni ndogo, wiki ijayo tutaendelea. USIKOSE!
Ramadhan Kareem!

Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love. Kwa makala zaidi tembelea; www.globalpublisherstz.com

No comments: