ANGALIA LIVE NEWS
Monday, August 22, 2011
Katibu wa Mbunge Lema adakwa kwa ujambazi
KATIBU wa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Goobless Lema, anashikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi Arusha akituhumiwa kuhusika na matukio kadhaa ya ujambazi mkoani Arusha.
Katibu huyo, Gervas Mgonja, pia gari lake binafsi linahusishwa na kuhusika kubeba watuhumiwa wa ujambazi wanaoshikiliwa na Polisi na wako katika vituo mbalimbali vya polisi mkoani Arusha wakihojiwa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Thobias Andengenye alipoulizwa jana kuhusu suala hilo, alisema yuko safarini, lakini aulizwe Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa, Leonard Paul kwa maelezo zaidi.
“Niko safarini naelekea Dar es Salaam…hilo suala liko mikononi mwa RCO (Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa) hivyo ni vema ukawasiliana naye ili upate maelezo zaidi,” alisema Kamanda Andengenye.
Naye RCO Leonard Paul alipoulizwa kuhusu kukamatwa kwa Mgonja, alikiri na kueleza kuwa yuko chini ya ulinzi wa Polisi baada ya watuhumiwa wa ujambazi kutaja gari lake kutumika katika ujambazi.
“Ni kweli tunamshikilia kwani watuhumiwa wa ujambazi waliokamatwa wamemtaja kuwa aliwakodishia gari na limekwenda kufanya uhalifu,” alisema RCO Paul.
Alisema taarifa zaidi za tukio hilo zitatolewa leo baada ya upelelezi kukamilika kwani kwa sasa wanakamilisha baadhi ya maelezo kwa watuhumiwa wengine waliokamatwa.
Alisema Mgonja alikamatwa na Polisi wa Jiji la Arusha tangu Ijumaa na yuko chini ya ulinzi wa Polisi ili aeleze kwa kina kuhusika kwake baada ya kutajwa na wenzake.
Hata hivyo, habari zaidi zinadai kuwa Mgonja ndiye aliyekuwa akiendesha gari hilo na alikimbia baada ya kufanya uhalifu na kuwatosa watuhumiwa wengine na kutokomea kukimbia kukamatwa na polisi.
Vyanzo vya habari vilidai kuwa polisi waliwabana watuhumiwa wengine wa ujambazi ambao ni wakazi wa Sekei na kumtaja Katibu huyo wa Mbunge kuhusika kuwabeba na kushirikiana katika matukio hayo ya ujambazi, lakini alifanikiwa kukimbia.
Alipoulizwa jana kwa simu kuhusu kukamatwa kwa Katibu wake, Mbunge Lema alisema, “niko nyumbani Arusha, lakini sina taarifa…ngoja nimpigie (Katibu) nijue ukweli wa taarifa hizo.”
Wakati huo huo, Polisi mkoani Arusha imezima jaribio la uporaji wa fedha zilizokuwa zikipelekwa benki, na watu saba wanashikiliwa juu ya tukio hilo ikiwemo kukutwa na silaha aina ya SMG na bastola.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Thobias Andengenye aliwataja majambazi hao kuwa ni Yahaya Seleman maarufu kama Degeraa (39), mkazi wa Olmatejoo jijini Arusha; Philemon Inyasi maarufu Arsenal (44) mkazi Kiboroloni mkoani Kilimanjaro na Frank John (35) mkazi wa Kambi ya Fisi katika Manispaa ya Jiji la Arusha.
Wengine ni Frank Mollel maarufu kwa jina la Chalii (35) na Charles George maarufu Kibaka (40) wote wakazi wa Sanawari; Priva Aloyce (29) na Julius William (29), wote wakazi wa Tarakea Rombo.
Kamanda Andengenye alisema majambazi hao walikamatwa Agosti 17 na 18, mwaka huu, kwa nyakati tofauti, kwa ushirikiano wa polisi wa Arusha na wenzao wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Alisema majambazi hao walikuwa wamepanga njama za kupora fedha zilizokuwa zinatoka katika Kampuni ya Bulk kupelekwa benki.
Alisema walipatikana katika maeneo ya Olmatejoo na Sanawari ya Juu baada ya polisi kuwawekea mtego na kuwakuta na silaha aina ya SMG ikiwa na risasi 27 na bastola moja ikiwa na risasi nne.
Alisema watuhumiwa hao bado wanaendelea kuhojiwa na wanahusishwa pia na matukio ya mauaji na unyang’anyi wa kutumia silaha na watafikishwa mahakamani pindi upelelezi utakapokamilika.
Habari Leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
2 comments:
Mmh!!Katibu wa Mbunge Lema anaitwa GABRIEL MBUKI, labda kama huyu Mgonja ni wa zamani. Kweli siasa mchezo mchafu, amkeni watanzania.
Just for masahihisho, Gabriel naye alikuwa wa muda tu, katibu wake hasa anayefahamika ni Lucy Fransisco. Sasa mpaka mambo ya Libya yatokee then nafikiri Watanzania tutaheshimiana.
Post a Comment