

Hatma yao ni Septemba
CC yaacha kazi kwa NECHatma ya wanachama wawili wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao wanatakiwa kupima wenyewe uzito wa tuhuma zinazowakabili na kisha kujiondoa kwenye nafasi za uongozi ndani ya chama, itajulikana mwezi ujao wakati Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itakapokutana kutoa maamuzi.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na kikao cha siku moja cha Kamati Kuu (CC) kilichofanyika juzi mjini hapa.
Alisema chama kinaendelea kusisitiza kuhusiana na maadili ya viongozi na wanachama wake na kwamba ni vita ya kudumu kuhakikisha CCM inaendelea kuwa chama chenye maadili.
“Kuendelea kuwataka wale wote wanaotakiwa kuwajibika kutumia muda huu kujipima na kuwajibika kwa maslahi mapana ya chama chetu. Aidha, Halmashauri Kuu ya CCM Taifa inatarajiwa kukutana wakati wowote mwezi Septemba ambapo pamoja na mambo mengine itatathmini utekelezaji wa maamuzi yake,” alisema na kuongeza:
“Mnajua uamuzi wa kujivua gamba na maamuzi mengine haya yalipitishwa na Halmashauri Kuu ya Taifa na kipindi cha upimaji wa utekelezaji kama tulivyosema ni kutoka kikao kimoja cha NEC kwenda kikao kingine. Kwa hiyo bado upo muda huo sasa kutoka NEC iliyopita kwenda NEC ijayo ambayo ni wakati wowote Septemba itakaa.”
Alisema kuwa wanaokabiliwa na tuhuma hasa ngazi ya Taifa bado wanao muda wa kutafakari na kuchukua hatua kabla ya Septemba.
Hadi sasa ni Rostam Aziz aliyetii maagizo ya NEC baada ya kutangaza kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Igunga sambamba na ujumbe wa NEC kupitia Mkoa wa Tabora. Rostam ambaye alikuwa akituhumiwa kuhusika na Kampuni ya Kagoda Agriculture Limited iliyokwapua Sh. bilioni 40 za Malipo ya Madeni ya Nje (EPA) katika benki Kuu ya Tanzania (BoT) na kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Limited, alijiuzulu Julai 13, mwaka huu.
Rostam pia alijiuzulu ubunge wa Igunga ambao ameushikilia tangu mwaka 1994 mfumo wa vyama vingi ulipoanza nchini. Rostam alishinda ubunge wa jimbo hilo baada ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wake na Waziri katika serikali ya awamu ya pili, Charles Kabeho.
Makada wawili, waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa ya Richmond, Edward Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge, ambaye naye alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Miundombinu (sasa Ujenzi) bado hawajajiuzulu nyadhifa zao za Wajumbe wa NEC au ubunge licha ya kikao cha NEC cha Aprili, mwaka huu kutaka wafanye hivyo.
Chenge ambaye ni Mbunge wa Bariadi Mashariki anakabiliwa na tuhuna za kashfa ya ununuzi wa rada ya kijeshi kutoka Uingereza mwaka 2002 kwa bei ya juu kuliko thamani halisi wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alipoulizwa kuwa CCM kuchelea kuchukua maamuzi dhidi ya wanaotakiwa kujivua gamba kunaweza kukasababisha kuondoka kwa wanachama wanaowaunga mkono watuhumiwa, Nnauye alisema: “Nasikitishwa na hali ya watu kuokota maneno barabarani, habari nilizozitoa ndizo habari za ndani ya kikao.
Taarifa ya chama ni ile iliyotokana na kikao kama kuna mtu ana wasiwasi na taarifa ile lazima iende ikabadilishwe na kikao si barabarani. “Ndio maana nikasema hubadilishi maamuzi ya Halmashauri Kuu kwa kucheza sarakasi barabarani, kuandamana na kuweka mabango haiwezi kubadilisha taarifa, ukaitisha mkutano ukatukana kuanzia asubuhi hadi jioni haibadilidishi maamuzi ya Halmashauri Kuu. Maamuzi ya Halmashauri Kuu yanabadilishwa kwenye kikao.”
HAKUNA MTU MASHUHURI KULIKO CCM
Alisema kama kuna mtu alikuwa na hofu, Kamati Kuu imekutana na wamesema kuwa sekretarieti imefanya vuzuri. “Mengine yote yanakufa natural death (kifo cha asili) hakuna mtu maarufu kuliko chama na chama hiki hakijaanza jana kuchukua hatua za namna hii, kama kuna watu wanadhani wao ni maarufu kuliko chama wajaribu tutawatimua na chama kitabaki pale pale, hatuogopi kwenda kwenye uchaguzi na ndio maana tunajipanga kwenda kwenye uchaguzi mdogo wa Igunga,” alisema Nnauye.
“Samaki ana nguvu ndani ya maji, lakini mtoe ndani ya maji uone. Wako watu leo hii wanadhani wana nguvu sana. Wakati mwingine watu wanakuwa wanakudanganya toka ndani ya chama uone wanakwambia tutakufa na wewe. Chama hakina wasiwasi,” alisema kisha akaongeza:
“Ni bora tukakapoteza jimbo, kata, sehemu ya utawala wetu, lakini tukasimama kwenye maadili yetu kwa sababu ndio msingi wa chama chetu, tukiyumba pale tunapoteza chama chote.”
“Sasa tung’ang’anie kidole kinachotukosesha? Bora tukikate kuliko tupoteze mwili mzima, sasa tukang’ang’anie kidole (kicheko) kwa sababu kinaufanya mkono uonekane mzuri ili kansa isambae mwili mzima… Watu wanaodhani kuwa tuna wasiwasi hayo ni ya kwao, tumesema kikao hadi kikao na tumeendelea kushikilia msimamo huo huo, leo ni siku ya ngapi na bado tunasimamia maamuzi yetu kama kuna mtu anadhani tunayumba hakuna kuyumba katika jambo hili,” alisisitiza.
CC YARIDHIA ROSTAM KUJIUZULU
Kuhusu kujiuzulu kwa Rostam Aziz, Nnauye alisema CC imejadili na kuridhia kujiuzulu kwake ujumbe wa NEC na imempongeza kwa uamuzi huo ambao ulizingatia maslahi mapana ya chama chake.
“Mtakumbuka ilikuwa ni wito wa chama chetu kwamba baadhi ya wanachama wetu wachukue hatua, yeye bahati nzuri amechukua hatua. CC imempongeza kwa uamuzi huo kwa kuwa umezingatia maslahi mapana ya chama chetu na imepokea na kuridhia,” alisema.
Alisema pia CC imepokea na kukubali taarifa ya kujiuzulu kwa Rostam katika nafasi ya ubunge wa Igunga na kwamba chama kinajipanga kutoa ratiba ya mchakato wa kumpata mgombea wa CCM Jimbo la Igunga. Alisema ratiba yao itazingatia ratiba itakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa sababu ndiyo yenye jukumu la kutangaza kuwa jimbo liko wazi na ratiba ya uchaguzi.
“Chama kitatengeneza ratiba ya mchakato wa ndani ya kumpata mgombea mbunge wa jimbo la Igunga na tutaitoa hivi karibuni,” alisema Nnauye na kufafanua kuwa CCM imeagiza kuwa shughuli zote za kampeni katika jimbo la Igunga zitasimamiwa na CCM Mkoa wa Tabora, Wilaya ya Igunga, kata zote, matawi na mashina ya jimbo.
Hata hivyo, alisema CCM taifa itakwenda kuongezea nguvu kwenye kampeni hizo na kwamba shughuli za msingi zitafanywa na wapenzi na washabiki walioko mkoani humo.
Hali kadhalika, alisema CC imejadili na kupitisha miundo mipya ya Idara ya Itikadi na Uenezi pamoja na Idara ya Mambo ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa kama sehemu ya maboresho yanayofanywa ndani ya chama.
Alisema wamefanya mabadiliko ya muundo ndani ya chama kwa kuiondoa idara ya propaganda na kuanzisha Idara ya Mawasiliano ya Umma. Nnauye alisema CC pia imejadili tatizo la uuzaji wa mahindi nje ya nchi, bei ya pamba, migogoro ya ardhi migodini na kero za Muungano.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
Na hatma ya Rais ni lini? Maana yeye kabebwa na hao mafisadi na ndio waliomuweka hapo alipo, tumechoshwa fufanywa wajinga! TUMECHOSHWAAAA!!!!!!
Post a Comment