ANGALIA LIVE NEWS
Monday, August 29, 2011
Maaskofu KKKT watema cheche mbele ya Mkapa
Daniel Mjema, Same
ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Meru, Paul Akyoo amewataka Watanzania kutoruhusu viongozi wabinafsi wanaotumia nafasi zao kujineemesha na kuacha nchi katika hali aliyoiita mifupa mitupu.
Wakati Askofu Akyoo akitoa maneno hayo, mwenzake wa Dayosisi ya Pare, Charles Mjema alitaja mambo manane ya kutafakari katika maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru ambayo alisema ni pamoja na kuona kama kuna mgawanyo sawa wa rasilimali za taifa.
Maaskofu hao walitoa kauli hizo mwishoni mwa wiki huko Chome wilayani hapa mbele ya Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 100 tangu Injili iingie katika eneo hilo.
Askofu Akyoo
Akihubiri katika Ibada ya maadhimisho hayo, Askofu Akyoo aliyekuwa mhubiri mkuu alisema ubinafsi wa viongozi hao wanaotumia nafasi zao kujineemesha badala ya kujali maisha ya Watanzania umesababisha maisha ya wananchi kuwa magumu.
Alisema vitendo hivyo vya viongozi hao kutoweka mbele maslahi ya umma katika kuwatumikia Watanzania kumeifanya nchi kubakia mifupa mitupu na kuonya kwamba yanayotokea Somalia yamesababishwa na ubinafsi wa viongozi.
Hata hivyo, Askofu huyo aliipongeza Serikali kwa kuweka mazingira huru ya kuabudu na kudumisha amani nchini akisema pia imeweka mazingira mazuri yaliyoiwezesha KKKT kushiriki katika kuihudumia jamii kielimu, kiafya na maji.
Askofu Mjema
Askofu Mjema alisema wakati Watanzania wanaadhimisha Jubilee hiyo ya miaka 50 ya Uhuru wanapaswa kujiuliza maisha yao yakoje na kama kuna uwiano sawa kwa Watanzania kumiliki uchumi, rasilimali na maliasili zilizopo.
Hata hivyo, Askofu huyo alimwambia Mkapa kuwa haulizi maswali hayo ili yeye ayajibu, bali aliyasema ili kila muumini wa KKKT na Watanzania wajue ukweli wa yale yanayolikabili taifa ikilinganishwa na miaka 50 tangu nchi ipate uhuru wake.
Askofu huyo alisema theluthi moja ya Watanzania ni vijana na watoto wenye chini ya umri wa miaka 18 akahoji mikakati ya Serikali katika kutunza kundi hilo na kuliandaa, ili miaka michache ijayo lishike usukani wa uongozi wa kanisa na taifa.
“Je, shule za msingi zilizopo na sekondari zinatoa elimu inayolingana na watu tunaowaandaa kwa ajili ya taifa hili?... maisha ya Watanzania leo yakoje tunapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru? Je, kuna fursa sawa katika mambo ya maendeleo, uchumi na siasa? Mgawanyo wa ardhi una uwiano gani hapa nchini kwetu?”
Mjema aliwataka Watanzania kutafakari ni nani wenye fursa ya kutumia misitu na rasilimali za madini na kama Watanzania wanapata fursa ya kushiriki na kumiliki uchumi ambao ndiyo nguzo kuu ya maendeleo.
Mkapa akwepa
Katika hotuba yake, Mkapa alikwepa kujibu maswali ya Askofu huyo na kueleza kuwa dunia sasa inapitia mabadiliko makubwa ya hali ya hewa ambayo yanaathiri mazingira na kusababisha uhaba wa mvua na kuleta baa la njaa.
Rais huyo mstaafu aliwataka wananchi wote wanaoishi kuzunguka Msitu wa Shengena kutambua kwamba Mwenyezi Mungu ndiye aliyewaletea rasilimali hiyo na kuwataka waitunze na kukabiliana na yeyote anayeihujumu.
“Wapo watu wanaotafuta rasilimali kama mbao na madini ndani ya msitu huu kwa namna ambayo itaathiri ustawi endelevu wa misitu… wasiruhusiwe… mjue kuwa msitu huu una vyanzo vingi vya mito na chemchem,” alisema.
Mkapa alisema pamoja na kufungwa kwa msitu huo, bado watu wanaingia kuvuna miti kwa ajili ya mbao na kudokeza kuwa hao lazima wawe ni wenyeji wanaofahamu ni wakati gani walinzi wapo na ni wakati gani hawapo.
Hata hivyo, Mkapa alisema changamoto kubwa na halisi inayowakabili hivi sasa ni kutoitumia ardhi kubwa iliyopo nchini akisisitiza kuwa Tanzania bado inalo eneo kubwa la ardhi ambalo halitumiki kwa shughuli za kuinua uchumi wa nchi.
“Nyinyi mliobanana huku milimani mnaweza kufikiri ardhi inakwisha. Ukweli ni kwamba bado Tanzania ina maeneo ya ardhi kubwa sana ambayo haikaliwi, hailimwi na hatumiki kukuza uchumi wa nchi,” alisema.
Maadhimisho hayo yaliyohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Kaimu Mkuu wa Mkoa wa kilimanjaro, Said Jalembo yaliambatana na harambee ya ujenzi wa kanisa jipya la Chome na Mkapa alichangia Sh5 milioni.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment