ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 29, 2011

Mapenzi ni ugonjwa wa moyo, ni asali inayotuliza moyo

KWA uwezo wa Mungu kesho inaweza kuwa Sikukuu ya Eid El-Fitry. Kiarabu leo inaitwa Yaumul Shaqqa. Yaani siku ambayo mwezi unaweza kuandama na watu kuamkia sikuu, endapo hautaonekana basi itakuwa swaumu kama kawaida halafu keshokutwa kitaeleweka.

Ni uwanja wetu wa mapenzi. Leo naomba nianze kwa kuuliza, kwa nini mapenzi ni tata? Unaweza kujiuliza swali hilo. Ni kwa faida ya kila mmoja kwa sababu yanatuhusu wote. Ni asali itulizayo moyo lakini ndani yake hutokea kuwa ugonjwa wa moyo.


Jiulize tena, kwa nini mapenzi yanasumbua? Mapenzi ni maumivu ya kichwa na moyo. Watu wengi waliomo ndani yake wanaweza kukupa ushuhuda wa mateso wanayoyapata kwenye uhusiano wao. Je, baada ya kuteseka huwa wanajiapiza kutorudi tena?

La hasha! Wanajaribu mara nyingi, hawakomi. Unaweza kujiuliza ni kwa nini lakini ukweli ni kwamba pamoja na maumivu ambayo mtu anaweza kuyapata kwenye mapenzi, bado yanabeba hisia kubwa kabisa katika maisha ya kila binadamu.

Maisha bila mapenzi hayajakamilika. Kutokana na hilo, uwanja upo wazi kwako kujiuliza ni kwa nini kitu kitamu namna hiyo kikafanywa kuwa tata, jumlisha na maumivu ya hapa na pale. Uvumilivu ukizingatiwa, huyeyusha utata unaojitokeza hapa na pale.

Muhimu zaidi ni kwamba mapenzi hayatoshelezi kwa uwajibikaji wa nusu nusu. Yanahitaji nidhamu na utekelezaji wa moja kwa moja kutoka moyoni. Yanayomhusu mwenzi wako ni vema uyabebe kama yako, hivyo ndivyo uhusiano unavyotaka.

Mapenzi yanahitaji akili, utashi na fikra zako bila kusahau nguvu zote katika kuzalisha matunda ya kila siku kwenye uhusiano ulionao. Utata unaoonekana ni ule unaotokana na wenzi kutotimiza matarajio ya kila mmoja.

Imetokea kuamini kuwa maneno ni mhimili wa kudumu kwa uhusiano na ngono husuluhisha migogoro ya muda mfupi. Wapenzi wanaponuniana, endapo watakutana faragha, hasira zote huspotea. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, ni zaidi ya kutosheka kimwili na utamu wa maneno mazuri.

Kwa mfano, ndoa nyingi zinakumbwa na matatizo ya watu kushindwa kuwa wakweli. Mwanaume au mwanamke anaweza kusema ni kiasi gani mwenzi wake anamuumiza. Lakini mwisho wa mazungumzo hawezi kukiri kasoro zake ambazo pengine ndiyo chanzo cha kila kitu.

Utata zaidi katika mapenzi ni kuwa inapotokea watu wanajuana kwa undani mno, hasa baada ya kuishi muda mrefu, ni hapo ndipo maneno hayawezi kufaa kitu, wala mchezo wa faragha hautaleta maelewano kwa maana hakuna kitu kigeni.

Lingine la utata katika mapenzi ni kwamba huwezi kuficha tabia yako muda wote. Ukishazoeana na mwenzi wako hasa baada ya kuwa pamoja muda mrefu, utaanza kujiachia. Ni kipindi ambacho mmoja anaweza kuhisi amesalitiwa kwa sababu mwanzoni hakuona hivyo ‘vitabia vya kuudhi’, alifichwa.

MAPENZI NI KARATA TATU
Kuna msemo kuwa mapenzi hayashindwi ila watu ndiyo hushindwa na mapenzi. Tunarukia kwenye uhusiano bila kuwa na uhakika ni kiasi gani tunawapenda wenzetu na ni kwa kiwango kipi tumejiandaa kubeba majukumu.

Mwisho wa siku tunafeli. Tatizo ni kwamba tunaanzisha uhusiano mpya bila kutatua kasoro zilizosababisha tukashindwa kwenye uhusiano na mtu wa kwanza. Hapo nadhani unaweza kuona kwamba wakati mwingine mapenzi siyo tata ila wenyewe tunayafanya kuwa magumu.

Tuna mambo mengi, ya kifamilia, kikazi, imani, dini, kabila, tofauti za kimtazamo na matarajio ya kila mmoja. Hatuko sawa. Tunapoingia kwenye uhusiano, fikra zetu zinakuwa zimejaa lakini ajabu ni kwamba tunapoingia kwenye uhusiano hatuyapi kipaumbele katika kuyajadili na kukubaliana. Hisia za juu hutupeleka kama vipofu.

Uhusiano wa kimapenzi wa watu wengi huanza pale ambapo mtu anajihisi yupo mpweke na anahitaji kampani. Wakati mwingine inatokea kwa sababu mtu anakuwa anakabiliwa na ‘presha’ ya kuwa na mwenzake kwa kigezo kwamba umri umekwenda. Si kwamba amemuona mtu mwenye sifa anazohitaji.

Umri ni kigezo kimoja lakini inawezekana ikawa mtu anataka kuwa na mwenzake kwa sababu ya msukumo wa nafasi yake kwenye jamii au kimila. Pengine ni dada sasa wadogo zake wameolewa yeye bado yupo tu. Au ni kaka, kwa hiyo kama kiongozi wa familia anaona bora aoe mapema kabla ya wadogo zake.

Kama umeingia kwenye uhusiano kwa sababu ya presha ya aina hiyo, utawezaje kuwa na matunda sahihi? Kichecheo cha uhusiano wa kimapenzi kinapaswa kuwa mapenzi. Mnapendana, kwa hiyo nyoyo zenu zinavutana kuingia kwenye sayari spesho. 

Usiwe na papara, angalia mahitaji ya moyo wako, weka mbele matarajio yako. Fikra zako uziweke wazi. Unapotafuta mwenzi hakikisha husumbuliwi na presha yoyote. Jambo ambalo unapaswa kuamini ni kwamba aliye ndani ya mawazo yako utampata kama ukijipa nafasi.

Kuna mambo ya kufanyia kazi, tukutane wiki ijayo ili tuendelee kujifunza kuhusu
utata uliopo kwenye mapenzi.

www.globalpublishers.info

No comments: