ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 19, 2011

Mapenzi ni furaha, itafute kwa nguvu zote!

NAKUKARIBISHA kwa moyo mkunjufu katika safu hii nzuri ya kupeana darasa la mapenzi. Ni imani yangu umekuwa ukivuna mengi kupitia hapa. Haya, kaa tayari kusoma mada mpya ya leo, lakini kabla sijaenda kuanza mada yenyewe naomba niwashukuru wote ambao mnanimiminia pongezi kupitia simu na waraka pepe.

Pongezi zenu zinanipa nguvu ya kuendelea kufanya hiki nikifanyacho. Hebu tujiulize; kwa nini tunakuwa na wapenzi? Kwa nini mapenzi yakawepo? Kwa nini tunaoa na kuolewa? Kwa nini baadhi ya watu hujinyonga baada ya kuachwa na wapenzi wao? 


Unadhani ni kwa nini mapenzi yamekuwa sehemu ya maisha yetu? Kwa nini yameharibu baadhi ya maisha ya watu? Naamini kila mmoja anaweza kuwa na majibu yake kulingana na mtazamo wake mwenyewe.

Kwa vyovyote itakavyokuwa mapenzi ni sehemu ya maisha yetu na kwa hakika maisha yetu hayawezi kukamilika bila kuwepo mapenzi. Ninapozungumza juu ya mapenzi namaanisha yale yanayotoka moyoni mwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Mapenzi ya dhati yasiyo na unafiki ndani yake.

Mapenzi hayo hukamilika baada ya wawili hao kuwa na hisia sawa za mapenzi. Amini kama upo katika uhusiano na mpenzi ambaye hakupendi, yaani wewe peke yako ndiyo unayempenda, utakuwa unatumikia mapenzi bila kujijua. Kama ndivyo, kwa nini uwe mtumwa kwa ajili ya kitu ambacho kinahitaji amani na faraja ya kweli?

Unadhani hakuna mwingine ambaye anaweza kukupenda kwa mapenzi ya dhati na penzi hilo likawa kwa pande zote mbili tofauti na ilivyo sasa? Inawezekana, huna sababu ya kulazimisha penzi kwa mtu ambaye hakupendi.

Mapenzi ni nguzo ya maisha yetu, kama ukifanikiwa kumpata mpenzi ambaye atakupenda na wewe ukampenda ni wazi kuwa maisha yako yatakuwa yenye furaha na hakika utafurahia sana maisha yako na huyo mwandani wako. Mapenzi yapo hivyo na kama ukijaribu kuyabadilisha utaumia mwenyewe!

Wakati mwingine unaweza ukapendwa na mpenzi ambaye hujampenda, unadhani kuna ulazima wa wewe kulazimisha kumpenda?
Moyo wako umeshazungumza na wewe, umekuweka wazi kuwa hauna mapenzi ya dhati kwa mtu huyo, kwa nini ujilazimishe? Tatizo hili mara nyingi huwa kwa wanawake zaidi.

Anatokea mwanaume anampenda sana, anapomtongoza anajikuta kuwa hampendi, anachokifanya ni kumwambia kuwa atamjibu baadaye! Lengo la kumwambia hivyo ni kwa ajili ya kujipanga na kufikiria. Mapenzi hayafikiriwi ndugu zangu.

Kama mtu unampenda, unapomuona tu siku ya kwanza, moyo wako hutetemeka juu yake na hutamani uambiwe kitu fulani na huyo aliyeuteka moyo wako ghafla. Hii inamaana kuwa atakapokuambia kuwa anakupenda, huwezi kusubiri zaidi, hutakuwa na kitu cha kusubiri, ni nafasi uliyokuwa ukiisubiria kwa hamu sana. Lazima utamkaribisha.

Naomba kusisitiza kitu kimoja, mapenzi ni furaha rafiki zangu, tena unatakiwa kuwa makini sana wakati wa kuitafuta furaha yenyewe. Hutakiwi kuwa na mapepe kabisa. Tuliza moyo wako, usikilize unataka nini? Usijilazimishe kumpenda mtu ambaye moyo wako haujaridhia.

Kwa maneno mengine, kama utalazimisha kuingia kwenye uhusiano wa aina hiyo, utalia siku nyingi ukiwa katika uhusiano wa aina hiyo. Je, kuna sababu ya jambo hilo kutokea?

Wapo baadhi ya wasichana, ambao wakitongozwa na wanaume ambao wanaona wazi kuwa hawawapendi, anakubali kuwa naye kwa lengo la kumchuma. Hufanya hivyo akijidanganya kuwa atajizoesha kupenda akiwa ndani ya uhusiano na mwanaume huyo. Hizo ni fikra potofu kabisa.

Kuna madhara gani?
Yapo mengi, lakini kubwa ni lile la kutokutosheka na mpenzi uliyenaye. Anaweza akakupa kila kitu lakini ukakosa penzi la dhati, ambalo ndiyo msingi wa uhusiano wenu. Unajua kama kuna mtu anakupenda na wewe unampenda, unajihisi furaha na amani siku zote.

Madhara makubwa zaidi ni pale utakapojikuta ukiingia katia uhusiano na mwanaume mwingine kwa ajili ya kusaka penzi la dhati. Faraja ya kweli. Ni hatari kufanya hivyo maana huwezi kujua mwenzi huyo ana mapatina wangapi nje yako.

Hatari kubwa inayoweza kupatikana hapo ni kuleteana magonjwa ya zinaa. Kwani hupendi maisha yako? Hebu kuwa makini kwa kuzingatia kwamba unahitaji furaha katika maisha yako.

Kamwe usijaribu kuingia katika aina hii ya uhusiano, ni jambo gumu sana kuamini kwamba unaweza ukampenda mtu baadaye, wakati tangu siku ya kwanza kukutana naye, moyo wako unamkataa.

Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya uamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo.

Kwa maneno mengine kama ukiingia kwenye uhusiano ambao moyo haujaridhia, ni wazi kwamba unatakiwa ujiandae kulia siku zote za ndoa yako. Upo tayari kuteseka? Jibu lako ndiyo hitimisho la mada hii. Naweka nukta.

Ramadhan Karim!

www.globalpublshers.info

1 comment:

Anonymous said...

Furaha ya kutafuta kwa nguvu hainoni, mapenzi ridhaa ya moyo.