ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 26, 2011

Mapenzi ni furaha,itafute kwa nguvu zote!-2

NATABASAMU! Nafanya hivyo kwa sababu siku na wakati wa kukutana navyi rafiki zangu umewadia. Enheee! Niambieni, mambo vipi? Bila shaka popote mlipo mnaitikia poa. Maridadi kabisa, kwa upande wangu ni mzima wa afya njema.

Nawaomba sana mfungue vichwa vyenu na kupata darasa hili ambalo linawasaidia wengi sana katika kuboresha uhusiano. Ni imani yangu mkimaliza kusoma, kuna kitu utavuna. Hutatoka bure na hutabaki kama ulivyokuwa.


Nazungumzia juu ya furaha ya maisha, kama nilivyosema wiki iliyopita, mapenzi ndiyo furaha yenyewe marafiki zangu. Kama ndivyo, basi ni wajibu wetu
kuitafuta kwa nguvu zote. Kwa maneno mengine, kama utakuwa upo kwenye uhusiano ambao umejaa matatizo, hakuna amani, migogoro kila siku, utakuwa huna furaha.

Nilieleza kwa mapana sana kuhusu aina ya watu ambao wanaamua kuingia kwenye uhusiano kwa masilahi yao binafsi. Yaani anakubali kuwa mpenzi wa fulani kwa sababu tayari kuna masilahi ambayo anaamini atayapata akiwa na mtu huyo.

Hayo ni makosa rafiki zangu, inakupasa uchague mtu ambaye moyo wako unampenda. Ngoja nikuambie, unapokuwa na mtu unayempenda, hata ikitokea siku akakuudhi, ni rahisi kumsamehe.

Ni rahisi kuweka kila kitu pembeni na kubakiza penzi lake la dhati ambalo umelihifadhi moyoni mwako. Upo rafiki yangu? Kuwa kwenye uhusiano ambao moyo wako haujaridhia, unakuwa upo kwenye penzi la kitumwa.

Unakuwa mtumwa bila kujijua, unakuwa gerezani hali ukiamini unaishi huru. Hutakuwa na furaha naye, hutasisimka faragha, kila kitu atakachokufanyia, utaona kama anakuzingua. Hana jipya tena kwako.

Utajenga chuki isiyo na maana, kwa sababu huna mapenzi naye. Kwenye mapenzi ya dhati hakuna chuki, hakuna hasira, kuna tabasamu mwanana usoni. Kuna amani. Rafiki zangu hebu sasa, tuendelee na vipengele vingine. Bila shaka kuna kitu utajifunza.

Utakuwa unatenda haki?
Rafiki zangu, kuingia katika uhusiano na mpenzi ambaye hujampenda, ni hatari sana. Kwanza unakuwa hujautendea haki moyo wako. Ni jambo ambalo linaweza kukusababisha ukajuta kuzaliwa.

Kuwa makini, maamuzi yahusuyo mapenzi ni lazima yafanywe kwa umakini wa hali ya juu sana. Unapofanya maamuzi juu ya mapenzi, unakuwa unapanga mustakabali wa maisha yako yajayo.

Maisha yako wewe mwenyewe, lazima ujichagulie maisha mazuri, matamu, yenye furaha yasiyo na huzuni. Uamuzi upo mikononi mwako. Unataka maisha ya aina gani? Ni kazi yako kuchagua.

Upe moyo wako haki, unatakiwa kuwa na chaguo la kweli na siyo kuulazimisha kwa matakwa yako. Twende tukaone kipengele kingine.

Husababisha usaliti
Rafiki zangu, unapokuwa na mtu ambaye hayupo moyoni mwako ni wazi itafikia mahali utahitaji pumziko la kweli. Hapo lazima utalazimika kutafuta mwenzi mwingine kwa ajili ya kukupa faraja.
Usaliti unaingia

 Kwanza unaanza kumsaliti mpenzi wako, lakini ni dalili za mwanzo za kumfanya naye akusaliti. Kwa vyovyote vile, msaliti hasa ambaye anafanya hivyo kwa lengo la kukata kiu yake ya mapenzi, huwa haoneshi ushirikiano wa kutosha kwa mwenzake.

Jambo hilo husababisha mwenzi ambaye hajui kinachoendelea, naye kutumbukia kwenye usaliti kwa lengo la kujifariji. Mbaya kuliko zote, katika usaliti huu ninaouzunguzia hapa, ni rahisi kuleteana magonjwa.
Nini cha kufanya?

Kama bado hujaingia kwenye uhusiano, chukua somo hili kama mwongozo kwako. Kuna madhara mengi yanaweza kusababishwa kwa tatizo hili la kukosa amani ya moyo kwa kuingia kwenye uhusiano bila mapenzi ya dhati.

Kuwa makini katika kufanya uchaguzi, achana na fikra ya kuingia kwenye uhusiano ilimradi nawe uwe na mpenzi. Acha moyo wako uwe mwamuzi wa mwisho. Kama humpendi achana naye. Unaweza usione madhara mapenzi, lakini baadaye kuna madhara makubwa sana ambayo utakutana nayo.

Fanya uchaguzi sahihi ambao baadaye hutaujutia. Kama ni kweli unataka kuishi kwa furaha, lazima uwe na mwenzi ambaye moyo wako umeridhia.

Kama umeshaigia...
Inawezekana umesoma somo hili kwa makini na umelielewa, yawezekana kabisa unajua au umegundua kwamba mpenzi uliye naye sasa (bila ndoa) si chaguo lako sahihi. Kama ndivyo, najua utakuwa njia panda.

Si ushauri mzuri sana kumshauri mtu aachane na mpenzi wake, lakini kama tutaenda mbali zaidi, tunaweza kujiuliza; mapenzi ni nini hasa? Mpenzi maana yake ni nini? Kwa tafsiri ya haraka, mapenzi ni hisia za upendo wa dhati kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine.

Umeona eeeh? Yaani kama hisia hizo hazipo kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, hapo kunakuwa hakuna mapenzi. Tafsiri ya pili ya mpenzi, ni yule ambaye anapendwa na mwingine/ mwenzi/patna.

Tunakwenda sawa? Hizo ndiyo maana zake. Kwa tafsiri nyepesi, kama upo katika uhusiano na mtu ‘mpenzi’ ambaye umejiridhisha kwamba huna mapenzi ya dhati naye, ni wazi kwamba hajafikia hadhi ya kuitwa mpenzi. Wewe unaweza kuwa mpenzi wake, lakini yeye si mpenzi wako.

Je, ni sawa kuendelea naye? AMUA MWENYEWE.
Ramadhan Kareem!

www.globalpublishers.info

No comments: