ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 17, 2011

Masaburi agiza kuvunjwa vizimba Machinga Complex


Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi
Minael Msuya na Hussein Issa
BAADA ya kuifumua Bodi ya Shirika la Maendeleo ya Uchumi Dar es Salaam (DDC), Meya wa Jiji la  Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi amegeukia Machinga Complex ambako ameagiza bodi ya usimamizi wa mradi huo kuvunja vizimba zaidi ya 2,000 vilivyokodishwa huku vikiwa havifanyiwi biashara.

Hatua hiyo ya Dk Masaburi ambaye ametangaza mgogoro na wabunge wawili wa Dar es Salaam, Abbas Mtevu na Mussa Azzan Zungu, ni mwendelezo wa kile alichokiita mkakati wake wa kusafisha ufisadi uliotamalaki katika miradi mbalimbali ya jiji hilo.

Wiki moja iliyopita Dk masaburi alivunja bodi ya DDC inayoongozwa na Mtevu na jana alifanya ziara katika majengo ya Machinga Complex yaliyopo Ilala ambayo yako chini ya Zungu kama mwenyekiti wa bodi.

Dk Masaburi alitoa kauli hiyo baada ya kile alichokiita mikataba mibovu iliyotumika katika kugawa vizimba vya kufanyia biashara kinyume na taratibu.Dk Masaburi alisema baadhi ya watu waliopewa vizimba na bodi hiyo sio wahusika wakuu na kwamba wanapaswa kutangaza tenda kwa wafanyabiashara wakubwa ili wafanye biashara katika maeneo hayo na kuliongezea jiji kipato.

“Nilichokigundua hapa ni utawala na mikataba mibovu iliyotumika kinyume na taratibu zilizowekwa, baada ya kuwa na uamuzi wa kujenga jengo la Machinga Complex,” alifafanua  Masaburi na kuongeza;

“Hivi vizimba vya bodi inaonyesha mmepeana wenyewe kwa wenyewe, hakuna utaratibu uliotumika, kama wanaostahili kupewa vizimba hivi wametosheleza basi tangazeni tenda kuwa kuna maeneo ya kufanyia biashara katika jengo la Machinga Complex. “

Dk Masaburi aliitaka bodi hiyo kutoa idadi ya watu ambao wamepatiwa vizimba hivyo pamoja na mawasiliano yao, ili kuwashughulikia na kupata ufafanuzi juu ya kupata vizimba hivyo.

Alifafanua kwamba , kumekuwa na matatizo ya kiutawala na miundombinu mibovu katika jengo hilo kutokana na kuwapo kwa nyavu ambazo hazikustahili kuwekwa katika biashara ya machinga.

“Hizi nyavu zilizowekwa huku sijui nani aliyefanya utaratibu huu, Machinga anajiwekea mwenyewe utaratibu wa kupanga biashara yake unapomwekea nyavu hizi zinamzuia na kumnyima nafasi,” alisema.

Meya huyo  aliongeza,  “Bodi haina njia nyingine ya kuweza kuimarisha mikataba hiyo, hivyo naigiza ikae na viongozi wa vikundi vya wafanyabiashara wa machinga ili kuona namna ya kuimarisha mikataba na kuondoa hizo nyavu kwani hazina faida ingawa nasikia zimegharimu  Sh1.2 bilioni.”
Naye Meneja wa Machinga Complex, Teddy Kundi alisema vizimba vyote ambavyo havitumiki kwa biashara watavivunja na kuwa watapatiwa wamachinga ambao hawana vizimba.

“Leo saa 6:00  mchana tutaanza kuvivunja vizimba hivyo ni zaidi ya 2,000 na vile ambavyo bodi imevigawanya yenyewe kwa watu na wamewapatia tena watu wengine tutalifanyia kazi haraka ili kutekeleza agizo la meya,” alisema.
Hivi karibuni Dk Masaburi amejikuta katika mgogoro na wabunge wa Dar es Salaam baada ya kuwaambia wanafikiri kwa makalio badala ya ubongo, baada ya kumshambulia bungeni kwamba alihusika kuuza Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA).

No comments: