ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, August 27, 2011

Mbowe, Wassira hapatoshi


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira akifurahia jambo na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe wakati wakitoka bungeni baada ya kumalizika kwa kikao cha asubuhi, jana mjini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi
Neville Meena, Dodoma
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu) Stephen Wasira na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana walitoleana matamshi makali kiasi cha kutishia kuvunjika kwa kipindi cha televisheni iliyokuwa ikiwahoji.

Viongozi hao walitoleana lugha kinzani walipokuwa wakihojiwa kwenye kipindi cha Jambo Tanzania, kinachorushwa na Televisheni ya Taifa (TBC 1).

Hali ilianza kubadilika baada ya Wassira kumshambulia Mbowe akisema kambi ya upinzani iko ovyoovyo na kwamba hata Baraza la Mawaziri kivuli alilounda Mbowe ni kama halipo na mawaziri hao kivuli hawaeleweki.

“Huwezi kusema Serikali yetu ni dhaifu wakati hata baraza hilo unaloliita kivuli ni ovyo tu ni kama halipo, hata hao mnaowaita mawaziri kivuli hawaeleweki kila mtu na lake,” alisema Wassira na kusababisha tafrani ndogo huku mtangazaji wa TBC1, Elisha Elia akijitahidi kuingilia kati.

Kauli za Wassira zinatokana na Mbowe kusema kwamba Serikali ilikuwa imeonyesha udhaifu mkubwa kwa kutokuwa na maandalizi mazuri ya bajeti zake hasa za wizara na kwamba ndiyo sababu ililazimika kuhamisha baadhi ya fedha baada ya kupata shinikizo la wabunge.

Alisema udhaifu huo unathibitisha udhaifu katika Baraza la Mawaziri la Rais Jakaya Kikwete ambalo alisema lilikuwa na fursa ya kujadili na kupitia bajeti hizo kabla ya kuwasilishwa bungeni.

“Ndiyo maana hapa ilibidi bajeti kama ya Nishati irudishwe na Serikali ije na mpango wa kukabiliana na mgawo wa umeme, si kwamba walikuwa hawajui, walikuwa wanafahamu kuhusu jambo hili, lakini sasa walisubiri mpaka warudishwe na Bunge, huu ni udhaifu, tena mkubwa sana wa Serikali yetu,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Kwa Serikali makini hatutegemei ingeleta bajeti za aina ile, hasa katika Wizara za Nishati na Madini; Maliasili na Utalii pamoja na ile ya Uchukuzi, huu ni udhaifu mkubwa.”

Kauli ya Mbowe ilimfanya Wassira ahamaki na kusema si kweli kuwa Serikali ni dhaifu, hivyo kuwarushia kombora Chadema kwamba hawana wanaoweza kushikilia nafasi za uwaziri endapo CCM kitaondoka madarakani.

"Mimi sioni Waziri pale, hata jana nilimwambia hivyo Zitto (Kabwe) tena nilimtajia majina lakini leo sitapenda kuyataja, hebu niambie nani ana uwezo wa kuongoza wizara kama tukiwaondoa hawa waliopo serikalini?” alihoji Wasira akionyesha kukerwa na maneno ya Mbowe.

Kauli hizo zilizua malumbano na kutokusikilizana huku Mbowe alisema kauli ya Wassira ni ya dharau kwa wabunge wa Chadema na wananchi waliowachagua katika majimbo yao.

“Unaona, hawa ndiyo aina ya mawaziri tulio nao katika Serikali yetu, tunategemea nini, huu ndiyo uwezo wao wa katika kuzungumzia masuala muhimu kwa taifa. Waziri amefanya dharau kubwa sana, sasa unategemea Serikali yenye watu wa aina hii itatekeleza majukumu yake vizuri?” alisema.

Mbowe alisema katika mfumo kandamizi wa demokrasia unaoendeshwa na CCM dhidi ya wapinzani, ni vigumu kwa wagombea wa upinzani kushinda nafasi za ubunge na kwamba mbunge yeyote wa upinzani anayeingia bungeni lazima awe na uwezo mkubwa na kukubalika zaidi na wananchi tofauti na wale wa chama tawala.

“Hebu tuwe wa kweli michango mingi ya wabunge wa upinzani ndiyo imeiamsha Serikali, sasa anaposema haoni mawaziri vivuli napata shaka na uwezo wake,” alisema Mbowe.

Mbowe alidai kuwa hakuna ubishi kuwa Serikali ni dhaifu kwani katika vikao vya Kamati za kudumu za Bunge, Kamati ya Miundombinu iliiagiza Serikali kuongeza Sh95bilioni kwa Wizara ya Uchukuzi lakini haikufanya hivyo mpaka pale ilipoumbuka bungeni.

Alisema pia Wizara ya Nishati na Madini nayo ilirudishwa na wabunge baada ya kuonekana kuandaa mipango mingi ya kumaliza tatizo la umeme pasi na kuweka fedha za kutosha

"Katika mazingira haya, umakini wa Serikali uko wapi, Serikali hii ina sera, mipango mingi mizuri lakini
tatizo kubwa ni utekelezaji sasa huo siyo udhaifu?”

Wassira alisema kuwa Serikali inapeleka bungeni bajeti zake ili ziweze kupata michango kutoka kwa wabunge kwa lengo la kuziboresha zaidi lakini kurudishwa kwake si kigezo cha udhaifu.

Alisema hakuna marekebisho makubwa yaliyofanyika katika Bajeti ya Serikali kwani fedha zilizopitishwa ni zilezile zilizopelekwa katika wizara zilizohitaji kuongezewa fedha.

"Hawa Chadema hawapendi amani, kila kukicha wanafanya maandamano, wanapinga kila jambo kuanzia Januari Mosi mpaka Desemba Mosi, huu ni upinzani gani?” alisema.

Malumbano hayo yalipamba moto zaidi baada ya Mbowe kusema anamheshimu Wassira hivyo asingependa kuingia katika malumbano ya kisiasa ambayo hayatokuwa na tija kwa taifa.

Hata hivyo, Wassira aliingilia kati na kusema hahitaji kuheshimiwa na Mbowe kwa kuwa anaisema Serikali kuwa ni dhaifu ambayo na yeye yumo.

“Yaani unasema unaniheshimu ili niseme hata pale unapoiita Serikali yangu ni dhaifu? Sihitaji hiyo
heshima," alisema Wassira

Mtangazaji wa kipindi hicho, Elia alilazimika kuingilia kati vijembe hivyo kwa lengo la kutuliza upepo ambao ulishaanza kuonyesha kubadilika kutokana na viongozi hao wawili kukinzana, hivyo kutokuwapo kwa masikilizano miongoni mwao.

Baada ya kuwatuliza, aliwapa nafasi ya kusema neno la mwisho na Mbowe akaitaka Serikali itimize wajibu wake kwa kutekeleza kwa vitendo huku Wassira akisema Bunge lilianza vibaya vikao vyake kwa kuwapo kwa mivutano mikubwa lakini wamemaliza vizuri kwani katika maslahi ya kitaifa wabunge walikuwa pamoja.

No comments: