ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 1, 2011

Mzindakaya awalipua mawaziri, wabunge

Kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chrisant Mzindakaya,akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.Picha na Fidelis Felix
James Magai
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Chrisant Mzindakaya, maarufu kama mzee wa mabomu amewataka mawaziri wanaoikosoa Serikali majukwaani kujiondoa kama hawaridhishwi na baadhi ya mambo.

Ingawa hakuwataja, lakini hivi karibuni kumekuwa na kupishana kwa misimamo miongoni mwa mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete huku Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe wakitajwa kuishambulia Serikali majukwaani.

Jana, akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam kutoa maoni yake, Mzindakaya ambaye aliwahi kuwa waziri alisema: “Mawaziri ni lazima wajenge umoja na wakubali uwajibikaji wa pamoja. Katika uwajibikaji wa pamoja, hakuna wa kuwaruka wenzake.”
Huku akimpongeza Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad kwa jinsi anavyozingatia uwajibikaji wa pamoja katika utekelezaji wa shughuli za Serikali, Mzindakaya alisema Baraza la Mawaziri haliwezi kuendeshwa na utandawazi.“Ukiona mambo si mazuri nenda kwa mkubwa wako kamwambie mimi ninataka kuondoka... lakini kutoka na kwenda kusema nje hiyo ni kutokukomaa kisiasa,” alisema Mzindakaya.

Alisema wakati akiwa serikalini tangu uwaziri na ukuu wa mkoa, kila alipoona kuna jambo ambalo si zuri alikuwa akimwandikia Rais na kwenye vikao vya Baraza la Mawaziri alikuwa akionyesha tofauti alizokuwa akiziona... "Kama jambo likimalizika linakuwa limelikwisha na si kwenda kulalamika nje hadharani.”
Alisema kama kuna wana-CCM wanaotamani urais mwaka 2015 na wako madarakani kwa sasa, hawana budi kuiweka kabatini ajenda hiyo na badala yake wamsaidie Rais Kikwete kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa kuwa ndiyo itakayowavusha.

Kauli ya hivi karibuni kuliibuka kutokuelewana miongoni mwa makada waandamizi wa CCM baada ya Waziri Sitta, Dk Mwakyembe wakiongozwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye kuhutubia mkutano mkubwa wa hadhara mkoani Mbeya na kusema kuwa kuna maeneo ambayo Serikali yao ilishindwa kuyafanyia kazi kikamilifu hasa lile kumaliza tatizo la umeme.

Msimamo wa Sitta
Baada ya kushambuliwa kutokana na kauli yake ya Mbeya, Sitta alisimamia kile alichokisema huku akisisitiza kwamba Serikali makini lazima ikiri upungufu kutokana na makosa yake: "Nilichokisema Mbeya ni kuwaambia Watanzania ukweli, nitaendelea kuwaambia ukweli."

Spika huyo wa Bunge la Tisa, alisema Serikali makini haiwezi kudanganya wananchi wake na kusisitiza: "Watanzania wa leo ni watu wenye akili huwezi kuwambia habari nzuri za umeme wakati umeme ni tatizo. Siwezi kuishi katika uongo. Naamini katika ukweli na nitaendelea kusema ukweli. Sasa hivi utamdanganya Mtanzania gani? Kuna vijana zaidi ya 100,000 wako vyuo vikuu leo uende kwa wananchi ukawadanganye!"

Mzindakaya na mwenendo wa bunge
Akizungumzia mwenendo wa sasa wa Bunge, Mzindakaya alisema mambo yanayoonekana kupitia kwenye runinga ni aibu kubwa na kwamba mwelekeo wa chombo hicho unatia wasiwasi.

Kada huyo wa CCM aliyekaa bungeni kwa takriban miaka 40 kabla ya kung'atuka mwaka jana, alisema Bunge ni chombo cha heshima katika kujenga mustakabali wa nchi na kwamba pamoja na shughuli nyingine, lina kazi kubwa ya kujenga utaifa bila kujali itikadi za vyama.

Mzindakaya alisema hadhi na uadilifu wa Bunge viko mikononi mwa wabunge na kuongeza kuwa, Bunge tukufu ni lazima lifanane na utakatifu huo huku akisisitiza: “Utakatifu wa Bunge si majengo, bali uadilfu huo unajengwa na wabunge.”
“Katika mihimili mitatu ya Dola, yaani Serikali, Mahakama na Bunge, Bunge ndilo linaonekana wazi kuwa ni mali ya wananchi, hivyo ni lazima lijenge image (taswira) ya mali yao," alisema.

Alisema uadilifu si usomi, bali ni tabia akisema hivi sasa bungeni kuna vijana wengi tu waliosoma kuliko enzi zao, lakini linazidi kupoteza hadhi yake. Alisema viongozi wanaochaguliwa wanapaswa waache baadhi ya mambo ili kulinda hadhi yao... “Huwezi kuwa mbunge au jaji halafu unakwenda baa unalewa hadi unaning’iniza miguu juu.
Mimi siku nilipoteuliwa kuwa RC (Mkuu wa Mkoa ) siku hiyo hiyo niliacha kwenda baa maana nilijiona ni mwakilishi wa Rais. Si kwamba niliacha kunywa, bali nilikuwa nakunywa nyumbani kwangu au kwa marafiki zangu walipokuwa wainialika."
Alisema ili kulinda hadhi ya Bunge, kuna kanuni ambazo zipo kwa ajili ya kuliongoza katika shughuli zake na kwamba kipimo cha utakatifu wake ni heshima ya wabunge.

“Hivyo hamtakiwi kubishana hovyo hovyo. Leo kila mbunge anasimama na Kanuni ya 68 tu ya mwongozo wa Spika lakini kuna kanuni nyingi tu ambazo ni sawa na Biblia," alisema.
Alisema Bunge linaendeshwa kwa kanuni ambazo wabunge hawana busi kuziheshimu na kusisitiza: "Bunge ni kanuni, hamuwezi kuendesha Bunge kama wapiga zeze. Hata mpira tu una kanuni, sembuse Bunge!”

Alisema mbunge mwadilifu hawezi kula rushwa kwani hawezi kupata ujasiri wa kuikemea. Alisema mbunge lazima awe mwadilifu kwa kuwa ni mtu mkubwa... “Wabunge ni watu wakubwa sana. Kwa mujibu wa Katiba kuna waheshimiwa wawili tu, mbunge na jaji. Hivyo ni lazima uwe mwadilifu kama huwezi acha, maana huwezi kuwa mheshimiwa halafu unakuwa wa hovyo.”

Kwa mtizamo wake, tatizo kubwa kwa sasa ni kwamba malengo ya kuingia bungeni miongoni mwa wanasiasa yamebadilika akisema wengi wao hawana wito.Alisema enzi ya utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, kiongozi alipoteuliwa alikuwa akipewa mafunzo maalumu ya uongozi. Alijitolea mfano akisema alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda, alikaa Chuo cha Kivukoni mwezi mzima akipata mafunzo.

“Ukifika kule ajenda ya kwanza ni uadilifu na uwajibikaji, ajenda ya pili ilikuwa majukumu yako.
Aliwataka wabunge wa CCM kuepuka kujiingiza katika malumbano na wabunge wa upinzani na badala yake wajikite katika kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama chao ili waweze kurejea 2015.

“Wabunge wa CCM ndiyo wenye chama tawala, hivyo wasifanye kosa kutumbukia katika malumbano. Kujibu hoja ni jambo jingine na kulumbana n jambo jingine. Kuna watu wanaweza kufanya vitu ili ku-disturb (kuvuruga) mfumo wa CCM, mkicheza mnaweza kujikuta miaka mitano yote mnakalia kulumbana tu bila kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya chama.
Wapinzani nao wanataka kuingia madarakani, wataingiaje bila kuwa-disturb?”,alisema.
Alisisitiza kuwa litakuwa ni kosa kwa wabunge na viongozi wa CCM kumwachia Rais Kikwete pekee kuzunguka mikoani kuangalia utekelezaji wa Ilani ya chama badala yake wote wajikite katika jukumu hilo.

“Tukifanya kosa, 2015 haturudi kwani kipimo si kubishana, bali utekelezaji wa ilani ya chama,” alisisitiza Mzindakaya na kuongeza kuwa yeye na hata Rais anatamani kuona baada ya kumaliza muda wake anaacha madaraka kwa chama chake.

Mzindakaya alisisitiza umoja na utaifa akiwataka wanasiasa kuweka kando tofauti za kiitikadi akisema kuwa kama kuna kosa kubwa ambalo wanasiasa wanaweza kulifanya ni kuacha utaifa ambao ndiyo umekuwa sifa kubwa ya Tanzania, Afrika na duniani kote.

Aliwapa changamoto wabunge na viongozi kuacha kulalamika na kubishana juu ya mahesabu yaani bajeti, bali walumbane katika kujenga uchumi huku akihoji ziliko klabu za kiuchumi kama ilivyo kwa mabunge mengine akitoa mfano wa Kenya.

Aliwataka pia wabunge na viongozi kwa jumla kuwa msitari wa mbele kuinua uchumi kwa vitendo badala ya kulalamika tu. “Lazima wanasiasa wa Tanzania tubadilike, kulaumiana na kunung’unika tu hakusaidii. Leo wananchi wanang’unika na viongozi wananung’unika, kinachotakiwa ni kutafuta majibu.”

Mwananchi

No comments: