

Ramadhan Semtawa
SIKU 10 alizotangaza Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kumpa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kuchunguza tuhuma za rushwa zilizomkabili Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo zimemalizika, lakini kazi hiyo haijakamilika hadi jana ambayo ilikuwa siku ya mwisho.
Hatua hiyo ya Ikulu ilikuja baada ya Mbunge wa Kilindi kutoa madai bungeni kwamba, Jairo ameziandikia barua zaidi ya taasisi 20 zilizo chini ya wizara yake akizitaka zichange Sh50 milioni kila moja kwa ajili ya kuwezesha kupitishwa kwa Bajeti ya wizara hiyo ya Nishati na Madini, Luhanjo alikutana na waandishi wa habari na kutangaza kumpa likizo kupisha uchunguzi dhidi yake na kumtaka CAG akague mahesabu ya wizara hiyo ndani ya siku 10 kuanzia Julai 22, mwaka huu.
Kazi hiyo ya uchunguzi ilitarajiwa kuwa imemalizika jana Julai 31, mwaka huu, lakini alipozungumza na gazeti hili, CAG Ludovick Utouh alisema, "Leo nina siku ya tano."
Utouh alisema hadi jana, ofisi yake ilikuwa na siku ya tano tu katika uchunguzi huo aliouanza tangu alipopata barua na maelekezo rasmi ya kazi hiyo kutoka serikalini.Alipoulizwa kama ofisi yake inaweza kufanyia kazi tuhuma hizo kwa siku 10, alisema: "Ninachoweza kusema ni kwamba we are trying (tunajaribu) kufanya kazi kwa muda mwafaka uliopangwa kuona tija inapatikana."
Hata hivyo, Utouh alisema wakati mwingine ni vigumu kutoa muda maalumu wa uchunguzi wa jambo fulani kwani inategemea unyeti na ukubwa wake, lakini akasisitiza: "Tutafanya kazi kwa kuzingatia muda na kama kutakuwa na haja ya kuongeza muda umma utajulishwa."
Alisema wakati mwingine anayetoa siku maalumu za uchunguzi inawezekana alitegemea kwamba muda huo ungeweza kukamilisha kazi lakini, wakati mwingine inakuwa tofauti kwani kazi inaweza kwenda nje ya matarajio hayo.
Kauli ya Ikulu kupitia Luhanjo
Julai 21, Luhanjo alitangaza siku hizo 10 za uchunguzi dhidi ya Jairo huku wanasheria, viongozi wa dini na wasomi, wakitaka mtendaji huyo ajiuzulu au awajibishwe na Rais ambaye ndiye mwenye mamlaka ya juu ya uteuzi. Walisema hayo baada ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutua mzigo akisema kwamba suala hilo lipo mikononi mwa Rais.
Luhanjo ambaye ni Mkuu wa Utumishi wa Umma, aliwaambia waandishi wa habari kwamba Jairo analazimika kwenda likizo kuanzia Julai 22, mwaka huu ili kupisha uchunguzi wa awali ambao unalenga kubaini iwapo ametenda kosa la kinidhamu kwa mujibu wa sheria zinazoongoza utumishi wa umma.
"Nimeanzisha uchunguzi wa awali (preliminary investigation) kwa lengo la kupata ukweli kuhusu tuhuma hizo. Wakati uchunguzi huo ukiendelea, Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini amepewa likizo ya malipo kupisha uchunguzi wa awali (relieve of duties administratively pending preriminary investigation)..., hatua zitakazochukuliwa hapo baadaye zitategemea matokeo ya uchunguzi huo wa awali," alisema Luhanjo.
Hatua dhidi ya Jairo
Luhanjo alisema ikiwa uchunguzi wa CAG utabaini kuwa Jairo ana makosa ya kinidhamu, atapewa taarifa za tuhuma husika ambayo itaambatana na hati ya mashtaka ambayo itaeleza kwa kifupi makosa hayo na jinsi yalivyotendeka."Taarifa ya tuhuma itatoa maelezo kuhusu lini mtuhumiwa anapaswa awe amejibu tuhuma hizo na katika kipindi hiki mtuhumiwa atasimamishwa kazi na kulipwa nusu mshahara," alisema Luhanjo.
Katibu Mkuu Kiongozi alisema ikiwa atapelekewa tuhuma hizo, Jairo atalazimika kujibu kwa kukubali au kuzikataa na kwamba ikiwa atakubali mamlaka ya nidhamu ambayo kwa mujibu wa sheria ni Katibu Mkuu Kiongozi, inaweza kutoa adhabu."Kama mtuhumiwa amekanusha au amekana, mamlaka ya nidhamu itaunda kamati ya uchunguzi ambayo itapewa hadidu za rejea ambazo pamoja na mambo mengine, itaeleza lini uchunguzi huo unapaswa kukamilika."
Mwananchi
No comments:
Post a Comment