Advertisements

Friday, August 12, 2011

Pinda amshangaa Mbowe kuhusu Madiwani


Waziri Mkuu Mizengo Peter Pinda
Fidelis Butahe
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda amewaruka viongozi wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe akisema hawakufikia hatua ya kuunda kamati ya pamoja ya kitaifa katika mazungumzo yao ya wiki iliyopita kuhusu kutafuta suluhu ya mgogoro wa Umeya wa Jiji la Arusha. Msimamo huo wa Waziri Mkuu unapingana na ule wa Mbowe aliyetangaza mara baada ya mazungumzo hayo kwamba wamekubaliana kuunda tume hiyo na taarifa yake ya awali ikiwa imepokewa na kujadiliwa na Kamati Kuu (CC) ya Chadema iliyoketi mjini Dodoma kuanzia Agosti tano hadi sita.

Mbowe katika mkutano wake na waandishi wa habari mnamo Agosti saba, mwaka huu mjini Dodoma, alisema: “Kamati hii itakuwa na wajumbe kutoka CCM na Chadema, itaundwa haraka iwezekanavyo ndani ya mwezi mmoja na Mwenyekiti anatarajiwa kuwa Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa.” 

 Hata hivyo, akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Dk Mary Mwanjelwa katika kipindi cha maswali ya kwa Waziri Mkuu, bungeni jana, Pinda alikiri kukutana na Mbowe na Katibu Mkuu wake, Dk Willibrod Slaa, kujadili hali ya kisiasa isiyoridhisha jijini Arusha kutokana na mgogoro huo wa umeya, lakini akasisitiza kuwa hakukuwa na makubaliano ya moja kwa moja ya kuunda kamati.
Pinda alisema alipokea ombi la Mbowe kutaka kufanya naye mkutano huku pia akiomba awepo na Dk Slaa, lakini akasema alistuka kuona taarifa katika vyombo vya habari kwamba amekubaliana na viongozi hao wa upinzani kuunda tume hiyo.

Alisema katika mazungumzo hayo,  aliwaeleza viongozi hao kwamba kwa kuwa suala hilo ni la kisiasa litakuwa nje ya uwezo wake lakini anaweza kumuomba Msajili wa Vyama vya Siasa aweze kusaidia uwepo wa mazungumzo hayo na kushangaa lakini alishangaa kuona Chadema kutangaza hadharani kuwapo kwa tume wakati ndiyo kwanza mchakato ulikuwa unaanza.
  “Nilikutana na Mbowe Agosti sita mwaka huu saa tatu asubuhi, baada ya kuniomba nikutane nao nyumbani kwangu. Katika mazungumzo yetu lilijitokeza suala la Arusha ambalo walionekana kulitilia shaka na kutaka upatikane ufumbuzi kwa maslahi ya wananchi.”

 Pinda alisema msimamo wake katika mazungumzo hayo ulikuwa kwamba kama ni ufumbuzi huo wa kisiasa asingeweza kutoa majibu ya moja kwa moja huku akisisitiza, kama ni sheria basi anayeona hakutendewa haki angekwenda mahakamani. Lakini, aliongeza, “Niliwaeleza kuwa suala hilo Msajili wa Vyama vya Siasa (John Tendwa), angeweza kutusaidia…, niliwaeleza kuwa nitamtafuta msajili na kumweleza aandike barua kwa CCM na Chadema ili kuvikutanisha vyama hivyo...”   “Juzi nilipomuona mheshimiwa (Mbowe) akizungumza kuwa tumekubalina hivyo (kuunda tume ya muafaka) nilishangaa…,hakuwa sahihi, namshukuru Mwanjelwa kwa kulileta suala hili kwa ajili ya kupatiwa ufafanuzi.”
Kutokana na majibu hayo Mwanjelwa alitaka kusikia ushauri wa Waziri Mkuu kwa madiwani wa Arusha waliofukuzwa.  Akijibu swali hilo Pinda alisema: “...Nilichomshauri Mbowe, nilimwabia maamuzi wanayokwenda kuyafanya Arusha ni ya Chadema, lakini busara inahitajika, busara yenyewe ni kuendelea na hali iliyopo mpaka hali itakapokuwa nzuri.”

“Sasa nashangaa maamuzi waliyochukua ya kuwafukuza madiwani, sijui hayo mazungumzo yatakuwaje. Ushauri wangu kwa madiwani waliofukuzwa kama wanaona si sahihi waende mahakamani.”  Mnyika akwama hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu

Baada ya kumalizika kipindi kipindi hicho cha Maswali kwaWaziri Mkuu, Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika aliomba mwongozo kwa Naibu Spika, Job Ndugai akidai kuwa Waziri Mkuu ametoa majibu ya kupotosha.    Aliomba mwongozo huo kwa kutumia kanuni ya 68(7) na kanuni ya 133.
Kanuni hiyo ya 133 inaeleza kuwa, Mbunge yeyote anaweza kutoa taarifa ya maandishi kwa Spika na kutaka kuleta hoja ya kutokuwa na  imani na Waziri Mkuu kwa mujibu wa ibara 53(a) ya Katiba.  Baada ya kusoma vifungu hivyo Mnyika alisema kumekuwa na kawaida katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu, kiongozi huyo kutoa majibu yenye upotoshwaji lakini kabla ya kuendelea Ndugai alimtaka aketi.

Akitoa maelezo juu ya mwongozo huo wa Mnyika, Naibu Spika alisema kanuni hiyo ya 133 inaeleza wazi kuwa, Mbunge anapaswa kutoa taarifa ya maandishi kwa Spika na taarifa hiyo inapaswa kuwekwa saini na kuungwa mkono na asilimia 20 ya wabunge.  Naibu Spika alisema, kwa kuwa wabunge wote wapo 357 ni lazima wabunge ambao wataunga mkono hoja hiyo wawe zaidi ya 72.

Alisema baada ya hoja hiyo kupokelewa itajadiliwa na kupigwa kura ya siri na wabunge na ndipo uamuzi utapatikana.  Kabla ya mwongozo huo wa Mnyika, Mbunge wa Mbozi Magharibi, David Silinde aliomba kutoa taarifa kwa kutumia kifungu cha 68 (8) lakini aliambiwa na Naibu Spika kwamba alifanya makosa kutumia kanuni hiyo na hivyo kuzuiwa kuomba taarifa kwa Waziri Mkuu.
Kanuni ya 68(8) inaeleza kuwa mbunge yoyote anaweza kusimama mahali pake na kusema taarifa na kwa ruhusa ya Spika atatoa taarifa au ufafanuzi kwa mbunge anayesema ambapo Spika atamtaka mbunge anayesema aketi kusikiliza taarifa hiyo. 

Wauza dawa za kulevya  Akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo aliyetaka kujua ni lini Serikali itawataja kwa majina wauzaji wa dawa za kulevya wakiwamo viongozi wa dini ambao hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete aliwanyooshea kidole, Pinda alisema kwa sasa kesi nyingi ziko mahakamani na vita ya dawa za kulevya si ya Tanzania pekee.

 “Rais aliposema kuna viongozi wa dini wanauza dawa za kulevya hakuwa na maana ya kuyashtaki madhehebu ya dini… alilenga kadhehebu fulani kuwa ndiko kanakofanya shughuli hizo, ni hivi vikanisa vidogovidogo,” alisema Pinda.

Mwananchi

No comments: