ANGALIA LIVE NEWS
Friday, August 12, 2011
Slaa : Tutaandamana hadi kieleweke Ikulu
NI ENDAPO RAIS KIKWETE HATATATUA MATATIZO YA WANANCHI
Peter Saramba, Arusha
KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, amesema yeye na chama chake wapo tayari kufanya maandamano ya nchi nzima kuanzia Mwanza hadi Ikulu kumuomba Rais Kikwete kuachia madaraka iwapo ameshindwa kuhimili nguvu ya umma inayotaka mabadiliko na utatuzi wa matatizo kadhaa yanayoikabili taifa.
Akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya NMC eneo la Unga Ltd mjini hapa jana, Dk Slaa alisema chama hicho kitashindwa kuhimili nguvu ya umma inayotaka mabadiliko na utatuzi wa matatizo kadhaa yanayolikabili taifa na kuiomba Serikali kutafutia ufumbuzi malalamiko na hoja zinazotolewa na wananchi.
Kauli kama hiyo pia ilitolewa na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche ambaye alisema Serikali inapaswa kushughulikia na kumaliza matatizo ya ugumu wa maisha yakiwamo mgawo wa umeme na sasa mgomo wa wafanyabiashara wa mafuta uliosababisha uhaba wa nishati hiyo nchini.
Alisema Chadema imevumilia mengi tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu na imekuwa ikiwahimiza wananchi kuendelea kudumisha amani na utulivu uliopo lakini itafika kipindi kitashindwa kuhimili vishindo vya nguvu hiyo ya umma.
“Kikwete na Serikali yake wanatusukuma kufanya mambo tusiyopenda kufanya. Yanayotokea katika nchi za wenzetu sasa ni matokeo ya umma kutoridhishwa na matendo ya watawala. Wanalalamikia maandamano yetu, lakini nataka kuwaeleza kuwa haya wanayoyaona ni mawingu, mvua bado
inakuja siku watakapotuona tunaandamana nchi nzima kutoka Mwanza hadi Ikulu,” alisema Dk Slaa.
Kwa upande wake, Heche alisema: “Kwa niaba ya vijana wote wa Chadema napenda nimtahadharishe Rai Kikwete kuwa achukue hatua sasa kukabili matatizo yanayolikabili taifa la sivyo mimi binafsi nitawaongoza vijana kuandamana hadi Ikulu kumtaka aachie madaraka.”
Mbowe
Kwa upande wake, Mbowe alisema kuwepo madarakani hadi 2015 kwa Serikali ya Kikwete ni haki kikatiba, lakini akaonya kuwa umma unaweza kuamua vinginevyo iwapo Serikali itashindwa kuongoza kwa kujibu mahitaji na maslahi ya jamii.
Alisema chama chake kinataka amani na ufumbuzi wa kudumu kuhusu tatizo la umeya Arusha ili kuruhusu shughuli za maendeleo na kiuchumi ziendelee kwa kufanyika mazungumzo ya haki na yenye nia njema kwa maslahi ya umma badala ya vyama kama ambavyo CCM kimekuwa ikifanya kuhusu mgogoro huo.
“Amani itapatikana kwa kutenda haki. Amani haiwezi kupatikana kwa kauli za viongozi au vitisho. Tumekubaliana na Waziri Mkuu siku 30 kumaliza mgogoro wa Umeya Arusha, baada hapo tutakwenda sote Ofisi za Manispaa na tutalala pale hadi kieleweke,” alisema Mbowe.
Alisema uamuzi wa kuwatimua madiwani ulikuwa mgumu na ulifikiwa usiku wa manane katika kikao kilichoanza Saa 3:00 asubuhi baada ya wahusika kukataa kusikiliza ushauri wa watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa dini waliowataka kutekeleza maagizo ya Kamati Kuu.
Wenje
Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje na mwenzake wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa walisema wananchi wa majimbo yao wanaunga mkono uamuzi wa kuwatimua madiwani wasaliti huku Msigwa akienda mbali zaidi kwa kusema kila mapinduzi hutengeneza mashujaa na wasaliti wake.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Karatu, Lazaro Maasai alimuonya Mkurugenzi wa Manispaa ya Arusha kuwa ataongoza wananchi wa Arusha kumfungia nje iwapo ataendelea kuwatambua na kuwaruhusu madiwani waliofukuzwa uanachama.
Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalumu kupitia Mkoa wa Arusha, Joyce Mukhya alisema wananchi wa Arusha tayari wamepokea na kukubali uamuzi wa Kamati Kuu ya Chadema na hivi sasa wanasubiri uchaguzi mdogo ili kurejesha viti vya udiwani katika kata ambazo madiwani wake wamefukuzwa.
Tundu Lisu
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kukumbuka historia ya uamuzi uliowahi kutolewa na TANU mwaka 1968 kilipoamua kuwatimua uanachama wabunge saba wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo Kasela Bantu na Eli Anangisye waliokiuka maelekezo na maadili ya chama chao.
“Sisi Chadema siyo wa kwanza kufukuza waliokiuka maadili na maelekezo. Walianza TANU na hata CCM wanafanya hivyo hata sasa wanapovuana magamba. Kinachowasumbua sasa ni sisi Chadema kutekeleza kwa vitendo kufanya maamuzi huku wao wakishindwa kuwatimua mafisadi kama
walivyokubaliana kwenye halmashauri kuu yao,” alisema Lissu.
Godbless Lema
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alimshangaa Pinda kwa kujifanya mshauri wa madiwani waliofukuzwa akiwashauri kwenda mahakamani huku akishauri iwapo CCM inawapenda iwachukue na kuwasimamisha kwenye uchaguzi mdogo na kuahidi Chadema kitaibuka na ushindi wa kimbunga.
Lema aliahidi kuendeleza mapambano ya kudai haki ndani na nje ya Bunge hadi haki ya wananchi waliouawa na kujeruhiwa kwa kupigwa risasi na polisi katika maandamano ya Januari 5, mwaka huu ipatikane.
Wakili maarufu nchini na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Mabere Marando alisema wafanya jitihada kuwabembeleza madiwani waliofukuzwa kutekeleza waombe radhi na kujiuzulu nyadhifa zao ndani ya halmashauri bila mafanikio.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment