ANGALIA LIVE NEWS

Monday, August 15, 2011

Simba kugomea mechi na Yanga

Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage
Timu ya Simba itagomea kucheza mechi ya kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, kama shirikisho la soka nchini (TFF) halitawapatia vibali vya wachezaji wao wote kufikia leo na pia watagomea kucheza Ligi Kuu ya Tanzania Bara kama hawatapatiwa vibali vyao hivyo kufikia Jumatano.
Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage, aliiambia NIPASHE jana kuwa maamuzi ya kugomea mechi hiyo yamefikiwa na Kamati ya Utendaji ya Simba iliyokutana jana kufuatia taarifa kwamba TFF imemzuia mshambuliaji mpya wa klabu hiyo Gervais Kago

kucheza dhidi ya Yanga kutokana na kutokamilisha taratibu za usajili.
TFF kupitia kwa mkurugenzi wake wa mashindano, Saad Kawemba, ilisema kwamba Kago hawezi kutumiwa na Simba kutokana na kutokamilishwa kwa taratibu za usajili wake baada ya klabu yake ya Stade Central Africaine ya Jamhuri ya Afrika ya Kati kutuma kibali chake cha uhamisho wa kimataifa (ITC) kwa njia ya fax badala ya katika mtandao wa 'Transfer Matching System' (TMS) kama ilivyoamrishwa na FIFA.
"Kamati ya Utendaji imeamua kwamba Simba haitacheza mechi dhidi ya Yanga Jumatano kama hatutapatiwa vibali vya wachezaji wetu wote, sio kibali cha Kago tu, tunataka vibali vya wachezaji wetu wote Jumatatu. Kama Jumatatu (leo) itapita hatutacheza mechi dhidi ya Yanga. Na kama Jumatano itapita hatujapata vibali hivyo hatutashiriki Ligi Kuu," alisema Rage.
Alisema hawako tayari kupoteza muda wa maandalizi katika kufuatilia hatma ya Kago na wachezaji wengine.
"Kago ni mchezaji wetu halali na tumefuata taratibu zote kumsajili. Tuliingia naye mkataba Julai 13, 2011 na klabu yake ya Stade Central Africaine ilituma ITC yake yenye kumbukumbu Na. 295 Julai 16, 2011, hivyo ni mchezaji wetu. Lakini kwa kuwa Afrika ya Kati hawajaanza kutumia TMS, tuliwatumia FIFA nakala ya ITC hiyo ili kupata ufafanuzi wa suala hilo na wakatueleza kwamba tunaweza kumsajili kwakuwa si nchi zote za Afrika ambazo zimeanza kutumia utaratibu huo wa mtandao.
"Halafu mbona jambo hili linatuzuia sisi tu kusajili wakati tumewauza Mbwana Samata, Patrick Ochan na Mussa Mgosi katika klabu za TP Mazembe na DC Motema Pembe kwa kutumia utaratibu wa zamani na wanachezea klabu zao mpya?," alihoji.
Rage pia ameelezea kushangazwa na kuibuka kwa suala la kuzuiwa Kago hivi sasa wakati jina lake halikuwemo miongoni mwa wachezaji waliopaswa kujadiliwa katika kikao
Kamati ya Rufaa, ambayo yeye ni mjumbe, ambapo ni majina ya wachezaji wawili tu wa Simba, Mganda Derick Walulya na Mkenya Wills Ochieng ndiyo yaliyoondolewa.
Alipoulizwa Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura alisema hawawezi kuzungumzia madai yoyote ya Simba kugomea mechi hiyo mpaka klabu hiyo ya Msimbazi itakapowasilisha barua rasmi.
VIINGILIO
Licha ya tishio la Simba kutocheza mechi dhidi ya Yanga, kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana jana, kiingilio cha chini katika mechi hiyo ya Ngao ya Jamii iliyopangwa kufanyika keshokutwa saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kitakuwa ni Sh. 5,000 kwa eneo la viti vya rangi ya kijani.
Taarifa hizo zilisema kuwa kiingilio cha juu katika mechi hiyo ya ufunguzi wa msimu, kitakuwa ni Sh. 40,000 kwa eneo la VIP A.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa zoezi la kuanza kuuza tiketi linatarajiwa kuanza leo mchana na mashabiki wanaombwa kununua mapema ili kupunguza usumbufu siku ya mechi.
Mechi hiyo imenunuliwa na mfanyabiashara maarufu nchini ambaye ni mmiliki wa vituo vya nishati ya mafuta - Big Bon, chanzo hicho kiliongeza.
Awali mechi hiyo ilipangwa kuchezwa Agosti 13 lakini Shirikisho la Soka Nchini (TFF) iliisogeza mbele hadi keshokutwa kwa sababu timu ya taifa, Taifa Stars, ilitarajiwa kuwa nje ya nchi kwa ajili ya mechi ya kimataifa iliyotarajiwa kufanyika Agosti 10 ambapo baadaye iliyeyuka kwa madai kwamba wakala wa mechi hiyo dhidi ya Sudan alishindwa kuipatia tiketi mapema.
Mechi hiyo ya watani pia ilitarajiwa kuanza saa 9:00 kutokana na sasa baadhi ya mashabiki kuwa kwenye mfungo wa Ramadhani lakini viongozi wa klabu hizo mbili wakaomba mchezo uanze usiku ili kutoa nafasi ya kupata mashabiki wengi kwa sababu Jumatano ni siku ya kazi hivyo mchana watawakosa watu wengi.
Mara ya mwisho timu hizo zilikuatana Julai 10 katika fainali za Kombe la Kagame na Yanga kuibuka na ushindi wa goli 1-0.
Mabingwa hao wa Bara, Yanga pia waliifunga Simba mwaka jana katika mchezo mwingine wa Ngao ya Hisani katika hatua ya matuta.
NURDIN APONA
Kiungo wa Yanga, Nurdin Bakari yuko fiti kuivaa timu ya Simba katika mechi yao ya keshokutwa, afisa habari wa klabu hiyo ya Jangwani, Loius Sendeu, aliiambia NIPASHE jana.
Bakari ambaye alikuwa majeruhi kwa sasa yuko fiti na amejiunga na wachezaji wenzake kwa ajili ya kujiandaa na mchezo huo.
Sendeu alisema Bakari amejumuika pamoja na Mzambia Davis Mwape kurejea mazoezini baada ya wote kuwa majeruhi.
MGOMO WA JEZI
Kufuatia Yanga kugomea jezi mpya walizopewa zenye nyembo nyekundu ya wadhamini wakuu wa ligi kuu, Vodocom, uongozi wa TFF umesema kwamba unasubiri leo katika zoezi ya ugawaji rasmi wa jezi hizo kuona kama Yanga watagomea kwenda kuzichukua.
"Hatujaletewa taarifa rasmi kama Yanga wamegomea jezi hivyo siwezi kutoa 'comment' katika hilo. Tusubiri kesho (leo) tuone kama watagomea," alisema Afisa Habari wa TFF, Boniface Wambura jana.
Yanga wameripotiwa kugomea jezi zenye nembo mpya ya Vodacom yenye rangi nyekundu kwa maelezo kwamba rangi hiyo inapingana na utamaduni wa klabu yao, kama Simba walivyowahi kukataa jezi zenye nembo za zamani ya kampuni hiyo iliyokuwa na rangi ya kijani na wakarekebishiwa.
SOURCE: NIPASHE

No comments: