Wakati Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) likisema jana kuwa utata wa usajili wa mshambuliaji mpya wa Simba, Gervais Kago, kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati umesababishwa na viongozi wa klabu hiyo kushindwa kufuata utaratibu mpya wa usajili wa njia ya mtandao (TMS) kama inavyoagizwa na FIFA, klabu hiyo ya Msimbazi imesema mgomo wao wa kucheza mechi ya kesho dhidi ya Yanga uko pale pale.
Akizungumza jana, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, alisema kuwa waliieleza Simba kwamba wanatakiwa kufanya usajili wa mchezaji huyo kwa TMS kwa sababu ni mchezaji wa kulipwa.
Osiah alisema kwamba kibali cha uhamisho (ITC) cha Kago ambacho shirikisho hilo imekipokea kinaonyesha kuwa mchezaji huyo ni wa ridhaa jambo ambalo ni tofauti na mkataba ambao Simba imeingia na mshambuliaji huyo aliyeng'ara na timu yake ya taifa.
Alisema kwamba TFF haitakwenda kinyume na kanuni zake za ligi ambazo zinaelekeza kwamba wachezaji wa kigeni wanatakiwa kuhamishwa kwa TMS na viongozi wa Simba waache kutoa lawama juu na mtendaji wa shirikisho hilo, Saad Kawemba, kama ana nia ya kuihujumu.
"Kanuni ndio zinamzuia Kago na si mtendaji wa TFF, viongozi wa Simba wanakwepa ukweli, tunawaeleza kuwa usajili huo haukwepeki," alisisitiza Osiah.
Aliongeza kwamba kwa mara kadhaa Simba ilikuwa ikielezwa kuhusu usajili wa nyota huyo na ikakumbushwa kwamba FIFA ndio hufungua na kufunga dirisha la usajili hivyo haitawezekana kumsajili nyota huyo baada ya Julai 31, jambo ambalo viongozi wa klabu hiyo hawakulitekeleza.
Alisema kwamba Simba hawatakiwi kuficha udhaifu wao kwa kulitupia lawama shirikisho na badala yake wanatakiwa wapeleke hoja zao kwa maandishi ili zifanyiwe kazi.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema jana mchana kwamba uamuzi wa timu yake kutocheza kesho katika mechi ya Ngao ya Jamii uko pale pale kwa sababu wanaona kuwa wanataka kuhujumiwa na TFF.
Rage alisema kwamba wanaona timu yao inataka kuhujumiwa kwa sababu jina la mchezaji huyo halikujadiliwa wala kuzungumzwa kwenye kikao cha Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji kilichofanyika hivi karibuni ambacho yeye ni mjumbe hali iliyomaanisha kwamba usajili wa Kago haukuwa na tatizo.
Alisema kwamba pia wanashangaa kuona mchezaji wao huyo anazuiwa kucheza kupitia taarifa za vyombo vya habari na si mawasiliano rasmi ya barua.
"Tunashangazwa na kauli hii, tulishawajulisha TFF kwamba Jamhuri ya Afrika ya Kati hawajibu chochote kuhusiana na maombi yetu, lakini hatukusikilizwa," alilalamika Rage.
Alisema kwamba inakuaje TFF itoe taarifa za kuzuiwa kuchezwa kwa Kago siku chache kabla ya kuivaa Yanga wakati ITC ya mshambuliaji huyo ilitumwa kwa njia ya fax iliwasili TFF tangu Julai 16.
Alisema mbali na kugomea mechi hiyo, Simba imetishia pia kutoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara inayoanza Jumamosi endapo zoezi la kupatiwa leseni za wachezaji wake halitakamilika hadi kufikia kesho.
Wakati huo huo, jana mchana Simba iliwasilisha barua na vielelezo mbalimbali kwa TFF ikionyesha jinsi walivyojaribu kumsajili kwa njia ya TMS mchezaji huyo.
Habari za ndani kutoka TFF zinaeleza kwamba mchezaji huyo huenda akapewa kibali cha muda cha kucheza na Simba itatakiwa ikamilishe usajili wake kwa njia ya TMS wakati wa dirisha dogo baadaye mwezi Novemba-Desemba mwaka huu.
Tayari tiketi za mechi hiyo zimeshaanza kuuzwa tangu jana mchana kwenye vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment