ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 24, 2011

Siri ya Yanga kuivimbia Voda hii hapa

Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura
Siri ya Yanga kugomea kuvaa jezi zenye kuitangaza kampuni ya huduma za simu ya Vodacom kwa mwaka mzima, imebainika kwamba ni manufaa madogo mno ambayo kuyakosa si tatizo kwa klabu hiyo kubwa ambayo inanufaika kwa mkataba mnono wa kampuni ya bia nchini (TBL).
Kiasi kikubwa kabisa ambacho Yanga inaweza kupata ni thamani ya chini ya Sh. milioni 80 kwa kuitangaza Vodacom mwaka mzima, wakati mkataba wao na TBL ni wa thamani ya Sh. milioni 500 kwa mwaka.

Wakati TBL ina mkataba wa Sh. bilioni 1 kwa mwaka kwa klabu mbili za Simba na Yanga, katika mkataba wa Vodacom na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kisi hicho cha Sh. bilioni 1 ni mkataba wa jumla wa mwaka mzima wa klabu zote 14 za Ligi Kuu pamoja na nauli na sare za waamuzi.
Afisa habari wa TFF, Boniface Wambura alikaririwa jana akisema kuwa Yanga kwa kugomea kuvaa jezi za Vodacom watakosa nauli, jezi na zawadi endapo wataibuka mabingwa wa ligi.
Katika mchanganuo wa mkataba huo wa Sh. bilioni 1 za Vodacom katika udhamini wa ligi kuu msimu huu, kiasi cha Sh. milioni 352 ni kwa ajili ya jezi za klabu zote 14 na waamuzi na pia klabu zitapata nauli ya Sh. milioni 4 kila baada ya miezi mitatu.
Kama itachukuliwa mfano kwamba waamuzi ni timu moja nyingine katika ligi kuu ya Bara, Sh. milioni 352 za jezi zitagawanywa kwa 15 hivyo mgawo wa kila timu katika jezi utakuwa ni Sh. milioni 23.5. Na kwa kuwa nauli inayotolewa katika mkataba huo wa Vodacom ni Sh. milioni 4 (kila baada ya miezi mitatu), kila klabu kwa mwaka itapata Sh. milioni 12. Na kama klabu itatwaa ubingwa itapata Sh. milioni 40.
Kwa maana hiyo katika mkataba huo, kiasi cha juu kabisa klabu ambacho inaweza kutwaa ni jumla ya Sh. milioni 23.5, Sh. milioni 12 na Sh. milioni 40 za ubingwa, ambazo ni Sh. milioni 75.5.
Kwa klabu kama ya Simba, kiasi cha Sh. milioni 75.5 kwa mwaka ni takriban sawa na mshahara wa mshambuliaji wao Mzambia Felix Sunzu pekee anayelipwa dola 3,500 (sawa na Sh. milioni 5.6) kwa mwezi, ambazo kwa mwaka ni sawa na Sh. milioni 67.2.
Mgomo wa Yanga kutovaa jezi hizo za Vodacom umefuatia nembo mpya ya kampuni hiyo yenye rangi nyekundu na nyeupe, ambazo ni rangi za utamaduni wa wapinzani wao wa jadi Simba.
Katika mkataba unaowanufaisha Simba na Yanga wa TBL, klabu hizo mbili kila moja zitapata mabasi makubwa ya kubeba abiria 52 yenye thamani ya kati ya Sh. milioni 200-300, mishahara ya wachezaji Sh. milioni 25 kila mwezi, jezi zenye thamani ya Sh. milioni 70, Sh. milioni 20 za kugharamia matamasha yao (kama vile Simba Day) na zawadi ya Sh. milioni milioni 30 kwa klabu itakayotwaa ubingwa.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia wakati tukienda mitamboni jana, Yanga imeanza mazungumzo na kampuni mbili za simu kwa ajili ya kuingia nayo mikataba ya udhamini.
Louis Sendeu, Afisa wa Habari wa Yanga, aliimbia NIPASHE kwamba wameruhusiwa na TFF kuendelea na mazungumzo na kampuni hizo kwa sababu Vodacom hawatashughulika tena na klabu hiyo ya Jangwani.
"Tumefika katika hatua nzuri ya mazungumzo, tutazitaja kampuni hizo wakati mambo yatakapokuwa sawa," alisema Sendeu.
Hata hivyo, viongozi wa TFF hawakupatikana kuthibitisha kama ni kweli klabu inaweza kudhaminiwa na kampuni nyingine ya simu ilhali mdhamini mkuu wa ligi hiyo ni kampuni tofauti ya huduma za simu.
CHANZO: NIPASHE


No comments: