ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 26, 2011

Sukari bei juu, haishikiki


Bei ya sukari nchini imepanda huku Mkurugenzi wa Kiwanda cha Sukari cha Moshi (TPC), Robert Baissac, akisema kuwa sababu za kupanda ni kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji katika kiwanda hicho.
Baissac alitoa taarifa hizo jana mjini Moshi katika mkutano na waandishi wa habari.
Alisema kuwa mfuko wa kilo 50 unauzwa kwa Sh. 75,050 na kuwa wasambazaji watauza kwa bei ambayo watapata faida.
Alisema sababu kubwa ya kupanda kwa bei hiyo ni kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji wa kiwanda ambapo pia gharama za mafuta zinachangia kupanda kwa bidhaa hiyo.

“Ndugu zangu sukari imepanda kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji...sisi hapa kiwandani sukari kwa mfuko wa kilo 50 inauzwa kwa bei ya Shilingi.75,050 na kwa mfuko wa kilo 25 inauzwa kwa Sh.37,530… pia kwa mfuko wa kilo 20 tunauza kwa Shilingi 32,850, hizo ndizo bei zetu kwa hapa kiwandani,” alisema.
Alisema viwanda vingine vya sukari katika nchi nyingine duniani ikiwemo Brazil vimepandisha bei ya sukari kutokana na gharama za uzalishaji kupanda.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili mjini Moshi ulibaini kuwa kilo moja inauzwa kati ya Sh. 2,200 na Sh. 2,500.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili mjini Moshi, walilalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo. Noel Damian na Mama Stellah, walisema bei hiyo inawaumiza sana hasa watu wa kipato cha chini kutokana na hali ya maisha pia kupanda na kuongeza kuwa ni vyema serikali ikalitupia macho suala hilo.
Walishauri kuwa ni vyema wauzaji wa rejareja wakauza kwa Sh.1,900 kwa kilo kwani kwa bei wanayonunulia kiwandani hapo hata wakiuza kwa bei hiyo watapata faida ya kutosha.
Mwanzoni mwa mwaka huu, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alitembelea TPC na kutoa tamko la kushushwa kwa bei ya sukari na kuagiza iuzwe kwa Sh.1,700 kwa mlaji wa kawaida, lakini agizo hilo mpaka sasa linazidi kupigwa danadana.
DAR ES SALAAM
Bei ya sukari katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam imepanda kutoka Sh. 1,800 kwa kilo moja mwezi uliopita hadi kufikia kati ya Sh. Sh. 2,100 na 2,200 kwa kilo.
Upandaji huo wa bei ulianza wiki hii. Bei ya jumla kwa mfuko wa kilo 50 kwa sasa unauzwa Sh. 98,000 kutoka Sh. 86,000 kabla ya Jumatatu wiki hii.
Uchunguzi uliofanywa katika maduka maeneo ya Mwenge, Sinza, Goba, Tabata na Kiwalani unaonyesha kuwa bei imepanda na sasa kilo moja inauzwa kati ya Sh. 2,100 hadi Sh. 2,200.
Katika eneo la Kiwalani, kiroba kimoja cha kilo 25 kimepanda kutoka Sh. 35,000 hadi Sh. 46,000.
Baadhi ya wafanyabiashara walioulizwa kuhusiana na kupanda kwa bei hiyo, walisema wauzaji wa jumla Jumatatu wiki hii waliwapandishia bei kwa mfuko mmoja kutoka Sh. 86,000 hadi 98,000 hatua iliyowafanya na wao kupandisha.
JIJI LA MWANZA
Jijini Mwanza bei imepanda kutoka Sh. 1,900 hadi Sh. 2,300.
Mmoja wa wauzaji wa duka katika eneo la Nyegezi, Jacob Lyimo, alisema dukani kwake sukari anaiuza kwa Sh. 2,200.
Lyimo alisema sukari imepanda bei baada ya kuadimika katika baadhi ya maduka ya jumla hivyo kufanya ipatikane kwa shida na kwa bei ya juu na kuwafanya wachuuzi wa rejareja nao kupandisha ili kupata angalau faida kidogo.
Katika duka moja la jumla lililopo katika barabara ya Rwegasore, kiroba cha kilo 50 kimekuwa kikiuzwa kwa Sh. 99,000 badala ya Sh. 80,000.
Naye muuza duka la jumla lililopo katikati ya Jiji la Mwanza karibu na Soko Kuu, alisema bei ya kiroba cha kilo 50 cha sukari inakwenda hadi Sh. 100,000 badala ya 85,000 hadi 90,000.
Mwandishi wa NIPASHE jana alitembelea baadhi ya maduka yaliyopo katika eneo la Nyegezi, Igogo, Miti Mirefu, barabara ya Kenyatta, Nyerere, Kilimahewa, Big Bite, Bwiru, Kirumba na Pasiansi, ambako bei ya sukari jana ilikuwa kati ya Sh. 2,200 hadi 2,300.
ARUSHA
Jijini Arusha katika Supermarket ya Masobe kilo moja ya sukari inauzwa kwa Sh. 2,500, Shoprite ni Sh. 1,800 wakati katika maduka ya mitaani ni kati ya Sh. 2,100 hadi 2,300.
JIJINI TANGA
Jijini Tanga kilo moja ya sukari inauzwa kati ya Sh. 2,000 na 2,200.
Wenye maduka wanasema kuwa mfuko wa kilo 50 wanauziwa kwa Sh. 96,000, lakini wanalalamika kuwa wenye viwanda wanawapunja kwa kuwauzia kilo 48.
JIJINI MBEYA
Jijini Mbeya bei ya rejareja ya sukari ni kati ya Sh. 2,000 na 2,100 wakati katika maduka ya jumla ni Sh. 1,800. Sukari hiyo ni inayotoka Malawi.
Mapema mwaka huu, Rais Jakaya Kikwete, aliagiza bei ya sukari isiuzwe zaidi ya Sh. 1,700 kwa kilo ingawa amri hiyo imeshindwa kutekelezwa na wafanyabiashara.
Imeandikwa na Charles Lyimo, Moshi; Richard Makore Dar; Cosmas Mlekani, Mwanza, John Ngunge, Arusha; Emamuel Lengwa, Mbeya na Lulu George, Tanga.
CHANZO: NIPASHE

No comments: