ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 26, 2011

Wabunge wa Zanzibar wamjia juu Tundu Lissu



Wabunge kutoka Zanzibar wameishambulia hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Rasmi ya Upinzani wa Wizara ya Katiba na Sheria, wakisema Zanzibar si koloni la Tanganyika.
Walitoa kauli hiyo wakati wakichangia hotuba ya kambi hiyo kuhusu makadiro ya matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/2012.
Hotuba hiyo iliwasilishwa bungeni juzi na Msemaji Mkuu wa Kambi hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu.
Mbunge wa Magomeni (CCM), Muhammad Amour Chomboh, alisema maneno yaliyotolewa na Lissu ni ya ufedhuli.
Napenda kumfahamisha yeye (Lissu) pamoja na wengi walio humu ndani wenye mawazo mgando kama yeye na waliokuwapo nje ya jumba hili, Zanzibar sio koloni la Tanganyika na halitakuwa hata siku moja koloni la Tanganyika. Na mheshimiwa Lissu Agosti 8 mwaka huu, alizungumza huyu kuhusiana na mambo ya Muungano kuchangia katika hotuba ya Muungano akajaribu kuwataja viongozi, ambao ni victim (waathirika) wa Muungano, ambao ni muongo na mnafiki,” alisema.

Aliongeza: “Nataka kumwambia kuwa Wanzanzibari hawatakubaliana na mpuuzi yoyote na uozo wowote, ambao umezungumzwa hapa kwa minajili ya kutaka kutugombanisha,” alisema.
Alipotaka kuendelea, alikatishwa na Lissu aliyekuwa akiomba utaratibu.
Kwa mara nyingine, Lissu alisimama akitaka kutoa taarifa hata hivyo, lakini Spika wa Bunge, Anne Makinda, aliingilia kati na kuwataka wabunge wote kuwa wavumilivu na kisha kumruhusu Chomboh kuendelea kuchangia.
Mbunge wa Tumbe (CUF), Rashid Ali Abdallah, alisema kauli aliyoitoa Lissu wakati akisoma hotuba hiyo, inaonyesha kuwa haelewi maana ya taifa.
Haelewi historia ya Zanzibar. Na kwa maana hiyo, mwelekeo wa Kambi ya Upinzani umepotea njia. Nadhani haya ni maoni yake. Unaposema Rais wa Zanzibar atolewe katika mambo yanayohusiana na Muungano una maana gani? Ipo serikali ya Tanganyika kujadili mambo ya Tanganyika hapa?” alihoji.
Aliongeza: “…Nazungumza hili kwa uchungu kabisa. Huyu ni msomi, lakini sijui amehitimu vipi usomi wake…jambo la msingi ni kuimarisha taifa letu liwe na nguvu lenye utawala bora na misingi ya uwajibikaji. Mawazo haya ya mheshimiwa waziri kivuli wa katiba na sheria ni mawazo funyu, yamepitwa na wakati na hayatapewa nafasi.”
Naye Mbunge wa Donge (CCM), Sadifa Juma Khamis, alisema mazungumzo yaliyotolewa na Lissu juzi yamevunja hata Katiba iliyopo hivi sasa.
Aliwataka kuangalia kifungu namba nane na namba tisa vya Katiba, vinavyomtaka mwananchi kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni yanayohusu nchi yake ya Tanzania.
Alisema kungekuwa na Serikali ya Tanganyika wasingeingilia mambo yanayohusu serikali hiyo.
Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, alisema Lissu katika hotuba alitoa maneno ya uchochezi.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hili la muungano bado halijaa kaa sawa, wanasiasa wanapaswa kuwashirikisha wananchi ili waulewe muungano huu hasa ni wa kitu gani. CCM wamekuwa waoga kuujadili muungano. Ni nyema kila jambo likawekwa wazi si kwa misingi ya kuuvunja bali kuimarisha ili watanzania wanufaike na matunda ya muungano.