ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 5, 2011

Viongozi Kahama wagawana kiwanja cha sekondari

Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dr Anna Tibaijuka
Shija Felician, Kahama
MATUMAINI ya wananchi wilayani Kahama ya kujenga Sekondari ya Kata ya Nyihogo, yameanza kupotea baada ya viongozi mbalimbali wa serikali kudaiwa kugawana eneo lililotengwa kwa ajili ya mradi huo.
Juhudi za Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Meja msatafu Bahati Matala, kutatua atizo hilo zimegonga mwamba baada ya viongozi waandamizi wa serikali wa sekta mbalimbali wilayani hapa kugawana viwanja eneo hilo.

Awali, Diwani wa Kata ya Nyihogo, Amos Sipemba, alisema viongozi hao wakiwamo wafanyabiashara walichukua eneo hilo kupitia watu wachache waliojifanya wazee, kabla lilikuwa likitumiwa na magereza ya wilaya kulima bustani za mbogamboga.
Sipemba alisema baada ya magereza kurudisha eneo hilo kwenye Serikali ya Kijiji cha Nyihogo mwaka juzi, walijitokeza wazee wakijifanya ni mali yao kisha kuliuza kwa mfanyabiashara mmoja wilayani hapa, ambaye alianza kuwauzia viongozi wa serikali kama kinga ya kumfanya asipokonywe.
Meja Matala alisema eneo hilo baada ya kukumbwa na mgogoro huo, tayari Kamati ya Maendeleo ya Kata ya Nyihogo, imepitisha maazimio kwenye vikao kujenga sekondari ya kata, kutokana na magereza kulikabidhi baada ya kulitumia kwa miaka 50.
Hata hivyo, Meja Matala alisema licha ya wananchi kuwa na mpango wa ujenzi wa sekondari, amewaagiza kusitisha kwanza ujenzi huo hadi mgogoro utakapomalizika, hali inayoonyesha kukataa tamaa ya kurejesha eneo hilo.
Uchunguzi unaonyesha idadi kubwa ya viongozi waandamizi wa serikali na baadhi ya wafanyabiashara wamejimilikisha eneo hilo kupitia ofisi ya Ardhi ya Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, ambayo ilipima kinyemela eneo hilo kabla halijasimamishwa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama, Eliza Bwana, licha ya kuagizwa na mkuu wa wilaya kusimamisha ujenzi wa eneo hilo kupitia mahakama, ameunda kamati ya kuchunguza suala hilo.
Baadhi ya wananchi wa eneo la Nyihogo, wamemwomba Mbunge wa Kahama, James Lembeli, kufikisha suala hilo kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ili afike kujionea ubadhirifu unaovuka mipaka unaofanywa na watumishi kwa kushirikiana na wafanyabiashara.
Kwa upande wake, Lembeli alimwagiza Sipemba kukusanya vielelezo vyote vya eneo hilo, ikiwamo vya magereza kulikabudhi kwa serikali ya kijiji ili apate sehemu ya kuanzia kushughulikia suala hilo.

Mwananchi

No comments: