ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 5, 2011

Kauli ya kigogo CUF yaichefua CCM Z`bar

Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema kimesikitishwa na kauli ya Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Machano Khamis Ali, kwa kuwafananisha viongozi wa CCM Zanzibar wanaotetea Muungano wenye muundo wa serikali mbili kuwa sawa na watumwa.
Machano, alikaririwa na baadhi ya vyombo vya habari alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara Mkokotoni Jimbo la Tumbatu kuwa viongozi wa CCM Zanzibar wanaotetea muundo wa serikali mbili ni sawa na watumwa wanaofanya kazi ya kutetea mambo ambayo wenyewe rohoni mwao hawayapendi.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Vuai Ali Vuai, alisema kauli hiyo ya kiongozi wa CUF haina tija na inaweza kuyumbisha na kuiparaganya Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Alisema kauli hiyo haikutakiwa kutolewa katika kipindi hili cha mpito ambapo dunia nzima inaiangalia Zanzibar kwa macho mawili, baada ya kufungua ukurasa mpya kwa kufikiwa mwafaka uliowezesha kuundwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Chama cha Mapinduzi kinamtaka Machano kufuta kauli yake ndani ya siku saba na kuiomba radhi CCM na Wazanzibari na asipofanya hivyo CCM itakishitaki chama cha CUF kwa wananchi pamoja na jumuiya ya kimataifa”, alisema Vuai katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Alieleza kwamba kauli hiyo inaonyesha uvumilivu na ustaarabu wa kisiasa umeanza kuwashinda CUF kwa vile ni kitendo kinachokwenda kinyume na malengo ya kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Vuai aliongeza kuwa huu si wakati wa kampeni ni vizuri Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikapewa nafasi ya kutekeleza malengo na majukumu yake baada ya kupita bajeti ya serikali ya mwaka wa fedha wa 2011/2012.
Alisema kwamba ni jambo la kushangaza vyama vya siasa ndivyo vinataka kuamulia watu ni katiba gani wanayotaka katika mfumo wa Muungano kwa kulazimisha matakwa ya sera za vyama vyao.
“Viongozi wa vyama vya siasa watafanya makosa makubwa iwapo wataendelea kuyatumia majukwaa ya kisiasa kuwashawishi Wazanzibari wote wakubaliane na matakwa ya sera za vyama vyao, huko ni kwenda kinyume na misingi ya kidemokrasia”, alisema.
Alisema CCM inawaonya wanaharakati na viongozi wa vyama ambao wamekuwa wakifanya kazi za kuwapotosha wananchi kuhusu Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwataka wajikite zaidi kuelezea faida na sio tu kasoro zake.
Tangu kuanza kwa mjadala wa Katiba mpya,kumeibuka baadhi ya viongozi wa CCM wanaotetea muundo wa Muungano wa serikali tatu na wanaopinga kwa madai mfumo huo unakwenda kinyume na Ilani na sera ya CCM.
Akifunga kikao cha Bajeti cha Baraza la Wawakilishi, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Idd, alisema muundo wa serikali mbili ndio utakaoendelea kufuatwa na serikali ya umoja wa kitaifa kwa vile ni matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
CHANZO: NIPASHE

No comments: