ANGALIA LIVE NEWS

Friday, August 5, 2011

Kamishna Mkuu wa TRA atakiwa kuhojiwa Zanzibar

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imeshauriwa kumwita Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya, ahojiwe na Kamati ya viongozi wakuu wa Baraza la Wawakilishi kuhusiana na kuendelea kutozwa kodi mara mbili wafanyabiashara kutoka Zanzibar.
 Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamza Hassan Juma, alipokuwa akizungumza na NIPASHE kufuatia mfanyabiashara mmoja kuzuiwa kupitisha betri mbili za gari jijini Dar es Saalam hadi zitakapolipiwa kodi, wakati tayari zimeshalipiwa kodi Zanzibar .

 Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa tatizo hilo ambalo linaathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya biashara Zanzibar na kusababisha wafanyabiashara kutoka Zanzibar kushindwa kulitumia soko la Tanzania Bara.
 Hamza alisema Kamishna wa TRA amefikia hatua ya kumdanganya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Dk. Amani Abeid Karume, kuwa tatizo hilo limeondolewa wakati bado. 
Alisema mwaka jana, Baraza la Biashara Zanzibar lilimwalika Kamishna huyo katika kikao kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wa Baraza hilo, Dk. Karume na kueleza kwamba vitendo hivyo vimeshadhibitiwa.
 “Kama Kamishna amefikia hatua ya kumdanganya Rais, basi kuna haja serikali imwite akutane na kamati ya Baraza la viongozi wakuu ili kulizungumzia tatizo hilo na lipate uamuzi wa kudumu,” alisema.
 Akizungumzia mkasa wa mfanyabiashara huyo Chum Faki Chum, alisema kiwango cha kodi alichotakiwa kulipa kilimshinda na kulazimika kwenda kukopa kwa jamaa zake, lakini hakufanikiwa.
 Alieleza kwamba kijana huyo aliporudi bandarini na kuwataka maafisa hao wampe majina waandikiane kwa maandishi ili aziache betri hizo na kwenda kulipia siku nyingine, maafisa hao walikataa na baadaye walimruhusu atoe betri hizo bila kulipa baada ya Mwakilishi huyo kuingilia kati.
 Hamza alisema kwa mujibu wa maelezo ya mfanyabiashara huyo, iwapo litaitishwa gwaride, maafisa waliokuwa zamu anaweza kuwafahamu kwa sura kwa vile vitendo wanavyofanya vinakwenda kinyume na maazimio yaliyofikiwa katika kutatua kero za Muungano.
CHANZO: NIPASHE

No comments: