ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 8, 2011

Chanzo cha usaliti, jinsi ya kuepuka kusalitiwa na kumgundua anayekusaliti!-2

ASSALAM alaikum wapenzi wasomaji wangu. Natumaini muwazima na mnaendelea vyema na majukumu yenu ya kila siku. Mimi namshukuru Mungu afya yangu ni njema na nipo hapa kumalizia mada niliyoianza wiki iliyopita.

Lengo hasa ni kuelezea chanzo cha wapenzi kusalitiana, kuepuka kusalitiwa na jinsi unavyoweza kumbaini mtu anayekusaliti. Wiki iliyopita nilizungumzia sababu za wengi kuwasaliti wapenzi wao, waliosoma watakuwa wamenufaika kwa namna moja ama nyingine.


Sasa nizungumzie jinsi unavyoweza kuepuka kusalitiwa. Hakuna anayefurahia kusalitiwa, kila mmoja anaumia pale mpenzi wake anapotoa penzi kwa mtu mwingine. Wapo waliokufa kwa presha baada ya kuwafuma wapenzi wao wakiwa na watu wengine au hata kusikia tu tetesi kuwa wanasalitiwa.

Ndiyo maana leo hii kila mtu yuko tayari kutumia gharama zozote kuhakikisha hasalitiwi. Zipo njia kadhaa za kumfanya mpenzi wako asikusaliti, zifuatazo ni baadhi tu.

Amini hawezi kukusaliti
Jambo la kwanza kabisa ni kujenga imani kwamba mpenzi wako anakupenda, anakuheshimu na kukuthamini hivyo hawezi kushawishika kwa namna yoyote ile kukusaliti.

Hii itakufanya kuwa na furaha na yeye, pia utamfanyia mambo ya kumfurahisha. Ukiwa huna imani na mpenzi wako, unaweza kujikuta unapunguza mapenzi kwake na matokeo yake ukachochea yeye kuanza kukusaliti.

Mtosheleze
Mpenzi wako mchukulie kama mtoto. Unapomlisha unahakikisha ameshiba ndiyo unamuacha. Akitaka pipi unamnunulia. Vivyo hivyo kwa mpenzi wako. Mtoshelezea katika kila nyanja.

Muoneshe upendo wa hali ya juu, mpe heshima anayostahili na pale mnapokuwa kwenye mambo yetu yalee, mpe hadi aseme nimeshiba mpenzi wangu. Ukifanya hivyo aende nje kutafuta nini? Akienda, huyo ana tamaa zake za kijinga na ukibaini muache haraka.

Zungumza naye
Ndiyo, vunja ukimya, zungumza naye! Si vibaya ukawa unazungumza na mpenzi wako juu ya mambo yahusuyo uhusiano wenu. Muulize ni mambo gani ukimfanyia anasikia furaha, akikuambia na mambo hayo yakawa ndani ya uwezo wako, jitahidi kumtimizia.

Muulize, anachukizwa na mambo gani, akikuambia basi jiepushe nayo. Hata asipokuambia, ukimchunguza utayabaini tu.
Hayo ni baadhi tu ya mambo ambayo ukiyazingatia yanaweza kukusaidia katika kumfunga ‘spidi gavana’ kimtindo mpenzi wako ili asikusaliti. Kama itatokea akakusaliti licha ya kumfanyia yote hayo, huyo siyo mtu wa kuendelea kuwa naye.

Lakini sasa, kuna watu ambao licha ya wapenzi wao kujitahidi kuwatimizia kila kitu  bado wanakuwa na tamaa na kufikia hatua ya kutoka nje ya ndoa. Utafiti usiyo rasmi unaonesha kuwa, wengi wanasaliti lakini baadhi wanafanya hivyo kwa siri kubwa.

Inawezekana hata wewe unayesoma makala haya unamuamini sana mpenzi wako lakini akawa anakusaliti bila wewe kujua. Swali la kujiuliza ni je, mtu anaweza kumbaini mpenzi ambaye anayemsaliti? Kimsingi kuna dalili za mtu ambaye si muaminifu kwa mpenzi wake. Kwa leo nitaeleza chache tu.

Usiri unaongezeka
Anachelewa sana kurudi nyumbani, ukimuuliza anaishia kukuambia ni mambo ya kazi. Simu yake ukiisogelea ni tatizo, hataki kabisa uiguse. Hii ni moja ya dalili ambayo inaashiria kuwa, mpenzi wako anakusaliti.

Yawezekana akawa anachelewa kutokana na sababu za msingi, yawezekana pia hataki uiguse simu yake kwa sababu za msingi lakini asipokuwa wazi kwako, elewa kuna jambo baya nyuma ya pazi.

Mahaba yanapungua
Siku zote mtu anayetoa penzi nje ya ndoa ni lazima atakuwa anapunguza asilimia flani ya penzi kwa mwenza wake. Anaweza kuwa si mtu wa kupenda sana kukutana na wewe faragha kama ilivyokuwa huko nyuma bila sababu za msingi. Mnaweza mkakutana lakini dozi anayokupa ikiwa siyo kama ile uliyoizoea.

Upendo unapungua
Mara nyingi mtu anayekusaliti hawezi kuonesha upendo ule ule kama ilivyokuwa zamani. Unaweza kushangaa anakuwa mkali bila sababu, haoneshi kukubembeleza wala kukuthamini kama ilivyokuwa huko nyuma. Huyo atakuwa na mtu anayemzuzua.

Jamani hayo ni kwa uchache tu, ninachotaka kusema katika kuhitimisha makala haya ni kwamba, kama kweli unampenda, usimsaliti, ukimsaliti unathibitisha kwamba huna mapenzi ya dhati kwake na kama huna mapenzi ya dhati kwake, hana sababu ya kuendelea kuwa na wewe hivyo akikuacha usiumie.

Tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.

www.globalpublishers.info

No comments: