ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 8, 2011

Dawa za kulevya kilo 97 zakamatwa



Tatizo linalokabili Taifa la biashara ya dawa za kulevya linazidi kushika kasi na kuonyesha hali ilivyo mbaya, Kikosi cha Kudhibiti Dawa za Kulevya nchini kimewakamata watu watano wakiwa na shehena ya kilo 97 za dawa hizo aina heroin yenye thamani ya Sh. bilioni 4.36 jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa kitengo hicho, Godfrey Nzowa, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuwa watu hao walikamatwa jijini Dar es Salaam juzi saa 3:30 usiku eneo la Africana Mbuyuni, wilayani Kinondoni na askari wa kikosi hicho kwa kushirikiana na polisi Mkoa wa Kinondoni.


Nzowa aliwataja waliokamatwa na dawa hizo kuwa ni Ali Mirzaei Pirbaksh, ambaye ni raia wa Iran; Said Mrisho, mkazi wa Tandale; Aziz Juma Kizingiti, mkazi wa Magomeni Mapipa; Abdul Mtumwa Lukongo, mkazi wa Kariakoo na Hamidu Kitwana Karim.

Kamanda Nzowa alisema watu hao walikamatwa na kilo 97 za heroin zikiwa kwenyemagari mawili.

Kwa mujibu wa Kamanda Nzowa, haikuweza kujulikana mara moja dawa hizo zilikotoka wala zilikokuwa zikipelekwa.

“Watu hawa tunatarajia kuwafikisha mahakamani hivi karibuni kujibu tuhuma zinazowakabili na upelelezi wa kesi hiyo unaendelea kwa kuwahoji watuhumiwa,” alisema Nzowa.

Aliwashukuru wananchi kwa ushirikiano wao na kuwataka waendelee nao, pia aliwataka watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja.

Kukamatwa kwa shehena hii kunazidi kuonyesha kuwa Tanzania ama ni njia ya kusafirisha dawa hizo au utumiaji nao uko juu sana kwa sasa.

Kamishna Nzowa alisema kuanzia Januari, mwaka huu hadi jana, ni kilo 294 za dawa hizo zimekamatwa nchini.

Mwishoni mwa Februari, mwaka huu, kikosi hicho kilikamata kilo 179 za heroin, zenye thamani ya Sh. bilioni sita na mapema Machi, mwaka huu, kikosi hicho kilikamata shehena nyingine ya kilo 81 za heroin jijini Dar es Salaam. 

Juni mwaka huu, Kamishna Nzowa, alipokuwa akitaja kukamatwa kwa mwanamama Mwanaidi Mfundo anayejulikana pia kwa jina la Naima Mohammed Nyakiniwa au Mama Leila, ambaye ni kinara wa biashara ya dawa hizo, alisema mwaka 2010, kilo 190 na gramu 780 za heroin zilikamatwa wakati cocaine zilizokamatwa zilikuwa kilo 64 na gramu 966.
CHANZO: NIPASHE

No comments: