ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 8, 2011

Simba yapaa, Yanga yang'ang'ania mkiani

Beki wa kushoto wa Yanga akiwatoka wachezaji wa Mtibwa
Mabingwa wa soka wa Tanzania Bara, Yanga, jana waling'ang'ania katika "nafasi yao mpya" msimu huu ya mkiani kutokana na kuambulia pointi mbili katika mechi zao tatu za kwanza kufuatia sare ya 0-0 na Mtibwa mjini Morogoro, huku mahasimu wao Simba, wakishinda mechi yao ya tatu kati ya tatu walizocheza kwa kuwafunga Villa Squad goli 1-0 mjini Tanga.

Yanga iliyokosa makali tangu kuanza kwa ligi haikufurukuta kwenye Uwanja wa Jamhuri jana na kufikia ushindi pekee walioupata msimu huu ni kukubaliwa na wadhamini wa ligi kuu ya bara, Vodacom, kutumia jezi zenye nembo ya njano walizoanza kuzivaa jana baada ya mvutano mkubwa uliotishia kushushwa daraja kama wangeendelea kugomea jezi zenye nembo nyekundu, rangi ya mahasimu wao.
Watani zao, Simba waliendeleza mwanzo mzuri wa msimu mpya baada ya kumaliza mikono mitupu msimu uliopita, kwa ushindi mwembamba wa goli 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Gervais Kago wa timu ya taifa ya Jamhuri ya Afrika Kati, ambaye utata katika uhamisho wake ulikaribia kuifanya Simba itishie kugomea kusishiriki ligi hiyo mwaka huu. 

Kago aliifungia Simba bao pekee katika dakika ya saba ya mchezo kwenye uwanja wa nyumbani wa "kuazima" wa Simba, Mkwakwani, kufuatia kazi nzuri iliyofanywa na kiungo Haruna Moshi 'Boban' aliyerejea Msimbazi msimu huu baada ya kukataa kucheza soka "chini ya mkataba usioridhisha" nchini Sweden.

Kwa ushindi huo, Simba imekwea hadi nafasi ya pili katika msimamo ikiwa na pointi 9, sawa na vinara JKT Ruvu wenye idadi nzuri ya magoli, lakini timu hiyo ya jeshi ikiwa imecheza mechi mbili zaidi ya Wekundu wa Msimbazi.

Yanga ambayo haijashinda mechi yoyote kati ya saba ilizocheza tangu ilipotwaa ubingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame), ililalamika kuwakosa nyota wake kadhaa katika mechi zao za awali, lakini jana hata baadhi ya nyota wao waliporejea hawakuweza kuonyesha makali yao.

Kipa Bora wa Ligi Kuu ya Bara msimu uliopita Mghana Yaw Berko alirejea kikosini jana baada ya kukosa mechi za kwanza kutokana na kuwa majeruhi, kama ilivyokuwa kwa mshambuliaji Mzambia Davis Mwape na Mghana Kenneth Asamoah ambaye hata hivyo aliingia katika dakika ya 64 akichukua nafasi ya Jerryson Tegete.

Baada ya kipindi cha kwanza kumalizika huku Mtibwa wakionekana kushambulia zaidi na Yanga wakinusurika mara kadhaa, kocha Mganda Sam Timbe, aliyeipa Yanga ubingwa wa Kagame na Ligi Kuu ya Bara katika kipindi kifupi alichokaa na klabu hiyo ya Jangwani, alitumia muda wa mapumziko kuwapa somo wachezaji wake katikati ya uwanja kama inavyotokea kwenye mechi za mchangani maarufu kama "ndondo".

Hata hivyo walijinusuru na adhabu kwa sababu waliingia kwanza kwenye vyumba vya kuvalia kama kanuni za soka za dunia zinavyosema na kutoka muda huo huo.

Katika mechi ijayo, Yanga itakuwa mgeni wa Ruvu Shooting Septemba 10, wakati Simba itawakaribisha Polisi Dodoma Septemba 14.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: