Thursday, September 1, 2011

Jeshi la watu 70 Algeria laja leo




Timu ya taifa ya Algeria inawasili leo usiku na msafara wa watu 70 kwa ajili ya mechi yao ya Kundi D ya kuwania tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Taifa Stars kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumamosi.
Msafara huo wa watu 70 utajumuisha wachezaji, viongozi na waandishi wa habari na utawasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 3:00 usiku.
Akizungumza na NIPASHE jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema kuwa msafara huo utafikia kwenye hoteli ya Golden Tulip iliyopo Masaki.
"Wametutumia taarifa kuwa watakuja kwa ndege ya kukodi ya Air Algeria ambapo watatua usiku wa saa tatu tayari kwa ajili ya mchezo wao dhidi ya Taifa Stars," alisema na kuongeza kuwa TFF kwa upande wao wameshakamilisha maandalizi ya mchezo huo.
Stars inayoshika nafasi ya tatu kati ya timu nne za Kundi D ikiwa na pointi nne na Algeria inayoshika mkia ikiwa na pointi hizo pia tatu nyuma ya vinara Morocco, kila moja inahitaji kushinda Jumamosi ili kudumisha matumaini ya kusonga mbele huku mechi mbili zikiwa zimesalia ili kumalizika kwa hatua ya makundi.

Wakati timu hizo zilipokutana katika mechi yao ya kwanza Septemba 3 mwaka jana nchini Algeria, Stars ililazimisha sare 1-1 ugenini kwenye mechi ambayo wageni walipambana kufa na kiume huku kipa Shabani Kado akiibuka shujaa kwa kuokoa hatari nyingi za wazi.
Katika kutambua ushindani mkubwa uliopo, kocha Jan Poulsen wamewaita nyota wote wa Stars wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi wakiwemo Henry Joseph anyecheza soka la kulipwa nchini Norway, Mbwana Samata (DRC), Abdi Kassim (Vietnam) na Athuman Machupa (Sweden), ambao tayari wamejiunga na wenzao kwenye mazoezi yanayoendelea kwenye Uwanja wa Karume jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE


No comments: