ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 1, 2011

Mnyika amng`ang`ania Ngeleja, Jairo



Waziri kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, amemshauri Rais Jakaya Kikwete, kutumia mamlaka yake kuwatimua kazi viongozi wa wizara hiyo akiwemo, aliyekuwa Katibu Mkuu, David Jairo, Waziri wake, William Ngeleja, Naibu Waziri, Adam Malima pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, badala ya kusubiri shinikizo la kuwawajibisha kutoka Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza sakata la Jairo.
Bunge limeunda Kamati Teule kuchunguza mantiki ya Luhanjo kutolea maamuzi sakata la Jairo, aliyedaiwa kuchangisha fedha kwa taasisi zilizochini ya wizara hiyo, kwa ajili ya kusaidia kupitisha bajeti kwa kuwa liliingilia Kinga na Madaraka ya Bunge.
Iwapo Rais Kikwete atasubiri uwajibikaji utakaotokana na matokeo ya ripoti ya Kamati Teule ya Bunge na maazimio yatayopitishwa na Bunge imani kwa umma juu ya serikali yake itaendelea kuporomoka,” alisema Mnyika katika taarifa yake aliyoitoa kwenye vyombo vya habari jana.

Alisema kiwango cha shamra shamra za mapokezi ya Jairo aliporejea kazini, yaliyoashiria kufanyiwa maandalizi na kauli za Waziri Ngeleja katika mapokezi hayo, yanathibitisha kwamba kashfa inayomwandama Jairo ya kuchangisha fedha za kusaidia kupitisha bajeti ya Wizara, yalikuwa na ridhaa ya viongozi wake na watendaji wenzake katika Wizara ya Nishati na Madini.
Kiwango cha maandalizi kilichofanyika kinadhihirisha wazi kwamba Waziri Ngeleja alikuwa akifahamu kabla, kuhusu tukio husika ndio maana mpaka sasa hakuna hatua zozote ambazo Wizara imechukua katika sakata hili,” alisema.
Mnyika alifafanua kwamba: “Kauli ambazo Waziri Ngeleja alizitoa mbele ya vyombo vya habari Agosti 24, 2011 baada ya kumpokea Jairo kwa kumkumbatia zilionyesha furaha yake kwa uchunguzi uliofanyika dhidi yake kutokubaini upungufu na kutaka kuuaminisha umma kwamba hakukuwa na kasoro zozote katika Wizara anayoiongoza kutokana na ukusanyaji na matumizi ya fedha katika mchakato wa bajeti.”
Alisema kauli ya Ngeleja kwamba ripoti ya CAG imemtendea haki Jairo baada ya kubaini kwamba kitendo cha Jairo kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti, ni ‘utaratibu wa kawaida’ serikalini.
Natoa mwito kwa Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuhusu suala hilo, kuchunguza pia ushiriki wa Waziri na Naibu Waziri katika kashfa hiyo ili waweze kuwajibika,” alisema Mnyika.
Hata hivyo, Mnyika alisema anakusudia kuandika barua kwa CAG ili ripoti ya kamili ya ukaguzi wake kuhusu Jairo iwekwe hadharani, ili wananchi waweze kuijadili na kutoa maoni yao.
CHANZO: NIPASHE

No comments: