ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 14, 2011

Lipumba azindua kampeni za CUF kwa mkokoteni wa punda

Geofrey Nyang’oro Igunga
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba jana alizindua kampeni za chama hicho katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Igunga kwa staili ya aina yake baada ya kupanda mkokoteni uliokuwa ukikokotwa na punda.

Aina hiyo ya usafiri aliotumia Profesa Lipumba ni tofauti na ule ambao umetumiwa na baadhi ya vyama hasa CCM na Chadema ambavyo viongozi wao wa kitaifa walikuwa na misafara ya magari ya kifahari maarufu kama mashangingi.

Shamrashamra za uzinduzi huo zilianza mnamo saa 6:00 mchana kwa wanachama wa CUF kukusanyika katika maeneo ya pembezoni mwa barabara kwa ajili ya kumpokea Profesa Lipumba.

Baadaye mnamo saa 8:45 mchana, Profesa Lipumba aliwasili na kupanda kwenye mkokoteni uliokuwa ukivutwa na punda akiwa na mgombea wa ubunge kupitia chama hicho Leopad Mahona pamoja na maofisa wengine waandamizi akiwamo Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho Bara, Julius Mtatiro ambao walielekea Uwanja wa Sokoine mjini hapa.



Atema cheche
Akizungumza kwenye mkutano huo, Profesa Lipumba alisema CCM imepoteza dira na mwelekeo wa kuongoza nchi hali inayofanya taifa kubaki katika dimbwi la umasikini.

“Wakati wa kujiuzulu aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hili, Rostam Aziz alitaja sababu za kujiuzulu kuwa ni kutokana na CCM kuwa na siasa uchwara za kupakana matope,” alisema Lipumba.

Alisema kutokana na msingi huo, ni dhahiri chama hicho kimepoteza dira ya kuongoza na hakipaswi kuendelea kupewa dhamana ya kuongoza nchi.

Kuhusu Rais mstaafu Benjamin Mkapa aliyezindua kampeni za CCM jimboni humo, Profesa Lipumba aliponda tambo zake kwamba Serikali ya chama hicho imeliletea taifa maendeleo katika miaka 50 ya uhuru wakati hali ni mbaya.

Profesa Lipumba alisema ameshangazwa na kauli hiyo kwa sababu Tanzania bado ni masikini licha ya kuwa na rasilimali nyingi zikiwamo za madini, ardhi nzuri kwa kilimo pamoja na mifugo.

“Mkapa amekuja hapa na kusema barabara hii imeletwa na CCM... hii ndiyo barabara ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania? Barabara hii ingeweza kuwa kubwa ya kupitisha bidhaa za kutoka nje kirahisi na kuwezesha taifa kukua kiuchumi,” alisema Profesa Lipumba.

Aliwataka wakazi wa jimbo hilo ambao ndiyo waliokuwa wa kwanza kufanya uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1994, kuonyesha dira hiyo ya mabadiliko itakayoelekeza Tanzania yenye neema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2015, kwa kumchagua Mahona wa CUF.

Alisema katika Serikali ya Mkapa ndiyo iliyouza rasilimali za nchi kwa wawekezaji na kuliingiza taifa katika mikataba mibovu ya madini ambayo ilikuwa ikisimamiwa na mgombea ubunge kupitia CCM, Dk Dalaly Peter Kafumu. Alisema katika sekta ya madini, Tanzania inapoteza fedha nyingi kutokana na kupata Sh tatu pekee kati ya Sh100 inayotozwa kama mrabaha.

Alisema hivi sasa Tanzania inashika nafasi ya tatu kwa uuzaji wa madini ya dhahabu nje lakini hakuna inachofaidi kutokana na rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Profesa Lipumba alidai kwamba Serikali ya CCM imeendeleza ufisadi hadi sasa ambako tuhuma mbalimbali kama Richmond zimeibuka.Alisema kutokana na hali hiyo, umefika wakati wa kufanya mabadiliko kwa kuondoa chama hicho madarakani ili kupata Serikali makini itakayosimamia wananchi kujiletea maendeleo.

Profesa Lipumba ambaye leo ataendelea na kampeni katika Tarafa ya Igurubi, aliwataka wakazi wa Igunga kumchagua Mahona ili kuleta mabadiliko katika jimbo hilo.

Kwa upande wake, Mahona alisema endapo ataingia bungeni, atahakikisha kuwa anashughulikia kero za wananchi wake ikiwamo tatizo la maji, madini, huduma za afya na elimu ili kuwakomboa kimaisha.Uchaguzi huo mdogo katika jimbo la Igunga umepangwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu.


MWANANCHI

No comments: