Saturday, September 3, 2011

Liyumba matatani tena, akutwa na simu gerezani


Amatus Liyumba
James Magai
ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Utawala na Utumishi (DPA) wa Benki Kuu Tanzania (BoT), Amatus Liyumba ambaye anatumikia kifungo cha miaka miwili jela, ameingia matatani tena akidaiwa kukutwa na simu gerezani aliyoitumia kuwasiliana na Rais Jakaya Kikwete.

Liyumba kwa sasa anatumikia adhabu ya kifungo cha miaka miwili katika Gereza la Ukonga, baada ya kupatikana na hatia ya matumizi mabaya ya madaraka katika ofisi ya umma wakati wa akifanya kazi BoT.

Wakati bado akiwa anaendelea na adhabu hiyo, taarifa zilizopatikana jijini Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile zilisema Liyumba alifikishwa katika Kituo cha Polisi cha Stakishari kilichopo Ukonga na kuhojiwa kwa kosa la kukutwa na simu gerezani.

Habari hizo zilifafanua kwamba Liyumba alifikishwa kituoni hapo saa 3:00 asubuhi kwa gari la Magereza lenye vioo vyeusi na kuhojiwa kwa muda wa takribani dakika 30 kuhusu tuhuma hizo.

Vyanzo hivyo vya habari vilifafanua kwamba, Liyumba anadaiwa kukutwa na simu ambayo ilibaki kituoni hapo kwa ushahidi.

Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Julai mwaka huu Liyumba alimpigia simu Rais Kikwete kwa kutumia simu hiyo. Hata hivyo, bado haijafahamika ni nini hasa alichomweleza Rais lakini habari zaidi zinadai kuwa kitendo hicho kilimfanya mkuu huyo wa nchi kuhoji iweje Liyumba amiliki simu wakati ni mfungwa?
Kutokana na tukio hilo, inadaiwa kuwa maofisa usalama walimwekea mtego na juzi usiku walimdaka akiwa na simu hiyo na asubuhi yake walimpeleka kituoni hapo kwa mahojiano.

“Sasa hivi kinachofanyika ni uchunguzi katika Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ili kujua alichokuwa akikifanya kwenye hiyo simu na uchunguzi huo ukikamilika basi anaweza kupandishwa kizimbani wakati wowote,” kilidokeza chanzo chetu.

Kifungo cha sasa
Liyumba alihukumiwa kwenda jela miaka miwili na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Mei 24, 2010 na hadi sasa ameshakaa gerezani kwa muda wa miezi 15 na siku 10 (mwaka mmoja, miezi mitatu).

Kabla ya hukumu hiyo, alikuwa amekaa mahabusu kwa muda wa miezi 15 na siku 26 tangu siku aliyopandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza, kisha kupelekwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

Alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Januari 27, 2009 akiwa na mshirika wake, Deogratias Kweka wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kuisababishia Serikali hasara ya Sh.221bilioni na matumizi mabaya ya ofisi za umma.

Walikuwa wakidaiwa kutenda makosa hayo kwa kuidhinisha upanuzi wa mradi wa majengo pacha ya BoT, bila idhini ya Bodi ya Wakurugenzi na hivyo kuongeza gharama za mradi tofauti na zilizoidhinishwa na bodi.

Hata hivyo, baadaye Kweka alifutiwa mashtaka na kubakia Liyumba peke yake ambaye naye alishinda kosa kubwa la kuisababishia Serikali hasara ya Sh.221bilioni na kubaki na kosa la matumizi mabaya ya madaraka ambalo lilimtia hatiani.

Mei 28 mwaka huohuo, kwa kutumia jopo la mawakili walioongozwa na Majura Magafu, Liyumba alikata rufaa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam akitoa sababu 12 za kupinga hukumu hiyo pamoja na adhabu.
 Katika sababu zake za kupinga hukumu hiyo jopo la mawakili wa Liyumba pamoja na mambo mengine, lilisema Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria na kiukweli katika kutathmini ushahidi na utetezi.

Hata hivyo, Desemba 21, 2010, Mahakama Kuu ilitupilia mbali rufaa  yake na kukubaliana na hukumu iliyotolewa Mahakama ya Kisutu.


Mwananchi

No comments: