ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 13, 2011

Luhanjo 'alikosea kumsafisha Jairo


Mr Luhanjo
Mwandishi wetu
KATIBU Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo ama hakujua au alifanya makusudi kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo katika kashfa ya kuzichangisha fedha taasisi za wizara hiyo, kwa sababu Serikali ilishatoa waraka kuzuia utaratibu huo.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Ramadhani Khijjah alitoa waraka maalumu kwa makatibu wakuu wa wizara zote unaowazuia kuchangisha au kupokea fedha kutoka taasisi zilizo chini yake kwa sababu yeyote ile.

Waraka huo namba 3 wa Machi 7, mwaka huu, wenye kumbukumbu namba TYC/A/400/620/18, unaonyesha kuwa hatua hiyo imefikiwa baada ya kuonekana kwamba baadhi ya mashirika na taasisi za umma zinatoa ruzuku au mikopo kwa wizara, bila kuzingatia taratibu na sheria.
Kwa mujibu wa waraka huo, makatibu wakuu wa wizara, wakuu wa mashirika na taasisi za umma watakaoshindwa kuzingatia agizo hilo, watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa kanuni na taratibu zilizowekwa.


“Kwa kuzingatia misingi hiyo, Wizara haipaswi kupewa fedha za ziada kupitia mashirika na taasisi zilizo chini yake,” unaeleza waraka huo ambao Mwananchi imeuona.
Waraka huo unazidi kueleza: “Endapo kutatokea mahitaji yatakayolazimu Wizara kuzichangisha fedha taasisi zilizo chini yake, mashirika au taasisi za umma, lazima ipate kibali cha Waziri wa Fedha baada ya kushauriwa na Mlipaji Mkuu wa Serikali (PMG) na Msajili wa Hazina kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya mwaka 2008.”
inaaminika kuwa Luhanjo na Jairo wanaujua waraka huo kwa sababu nakala zake zilitumwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi Ikulu, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Ramadhani Khijjah hakutaka kuzungumzia waraka huo kwa madai kwamba amekuwa nje ya ofisi kwa muda mrefu. Alishauri mwandishi awasiliane na Msemaji wa Wizara ya Fedha na Uchumi au Kamishna wa Bajeti.
“Sikiliza ndugu yangu, mimi kwa sasa ni mgonjwa, nimekuwa nje ya ofisi kwa muda mrefu, hebu mtafute PR (Ofisa Uhusiano) au Kamishna wa Bajeti ndiyo wanaohusika na mambo hayo ni muda mrefu sasa sina kumbukumbu nzuri,” alisema Khijjah.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovic Utouh alipotakiwa kueleza kama katika uchunguzi wake dhidi ya Jairo walifahamu uwepo wa waraka huo, alisema asingeweza kusema chochote sasa kwa kuwa suala hilo sasa lipo mikononi mwa Kamati Teule ya Bunge.

“Mimi nakushauri upige simu huko ilipotoka barua hiyo, huenda tulipata au hatukupata hiyo haisaidii kwa sasa kwani kumeshaundwa Kamati Teule ya Bunge kufuatilia jambo hilo,” alisema Utouh na kuongeza: “Sitaki kuonekana naingilia kazi ya Kamati.”

Luhanjo hakutaka kuzungumzia suala hilo akisema: "Sipo tayari kujibu swali lako katika mazingira haya, elewa kijana!"  Jairo hakupatikana kuzungumzia suala hilo kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokewa.

Taarifa za kuwapo kwa waraka huo zimepatikana wakati Bunge limeunda Kamati Teule kuchunguza utaratibu uliotumiwa na taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo kwa ajili ya kufanikisha mchakato wa kupitisha wa bajeti.
Julai 18 mwaka huu, Jairo alituhumiwa bungeni kwamba amezichangisha fedha taasisi zilizoko chini ya wizara yake kwa ajili ya kupitisha bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2011/2012.

Tuhuma hizo zilitolewa na Mbunge wa Kilindi (CCM), Beatrice Shellukindo alipokuwa akichangia Bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini iliyowasilishwa na Waziri William Ngeleja.

Tuhuma nyingine zilizokuwa zimetolewa na Shellukindo ni za kulipa masurufu ya safari za watumishi walio chini ya wizara hiyo na taasisi zake, ambao tayari walikwishalipwa na wizara na taasisi zenyewe.Tuhuma hizo zilimfanya Katibu Mkuu Kiongozi, Phillemon Luhanjo kumpa Jairo likizo ya malipo ili kupisha uchunguzi ambao ulifanywa na Ofisi ya CAG ambao katika taarifa yake, haukuthibitisha madai hayo hivyo Jairo kurejeshwa kazini Agosti 23, mwaka huu.

Kamati ya Bunge ya kuchunguza sakata ya Jairo, ni ya pili kuundwa wakati wa uongozi wa Rais Jakaya Kikwete, zote zikiwa kwa wizara hiyohiyo ya Nishati na Madini.

 Februari 7, 2008 aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na waliowahi kuwa mawaziri wa Nishati na Madini, Dk Ibrahim Msabaha na Nazir Karamagi walilazimika kujiuzulu baada ya kutajwa katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kuchunguza mkataba tata wa Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Richmond.  Kamati hiyo iliongozwa na aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini, Dk Harrison Mwakyembe. Dk Mwakyembe sasa ni Naibu waziri wa Ujenzi.

Agosti 25, mwaka huu  Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza majina ya wabunge watano, wanaounda Kamati Teule kumchunguza Jairo. Walioteuliwa ni Injinia Ramo Makani Matala, Gosbert Blandes, Mchungaji Yohane Israel Natse, Khalifa Suleiman Khalifa na Martha Umbulla.

Mwananchi

No comments: