ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 13, 2011

Waliochukua kinyemela vizimba 700 Machinga Complex walizwa

Zaidi ya vizimba 700 katika jengo la wafanyabiashara wadogo (Machinga Complex), vimevunjwa kutokana baadhi yao kushindwa kuvitumia ipasavyo.
Akizungumza wakati wa zoezi la uvunjaji wa vizimba hivyo, Meneja wa uendeshaji wa vizimba, Teddy Kundi, alisema wameamua kuvivunja baada ya kuona wafanyabiashara wengi waliopewa vizimba hivyo hawavitumii.

Alisema,  baadhi ya sababu kuu zilizosababishwa kuvunjwa kwa vizimba hivyo ni kushindwa kulipa kodi, kuhodhi vizimba pasipo kuvifanyia biashara  mtindo ambapo unafanywa na wafanyabiashara.


Kundi alisema ni mara ya tatu tangu waanze kutoa notisi kwa wafanyabiashara hao kuvitumia vizimba,  lakini wamekuwa wakikaidi na kusindwa kuvitumia.

“Mara nyingi tumekuwa tukiwaambia kwamba wasipovitumia vizimba tutanyang`anya, lakini mpaka sasa hawakutii na ndiyo maana tukaamua tuvivunje  ili kama hawavihitaji tuwapatie watu wengine,” alisema.

Aidha alisema wametoa mwezi mmoja kwa wafanyabiashara wote ambao wamevunjiwa vizimba vyao kwamba endapo hawatajitokeza kuvikomboa vizimba vyao, watavipiga mnada.

Baadhi ya wafanyabiasahara katika soko hilo, walisema  maisha yao yamekuwa magumu kutokana kukosekana kwa wateja katika soko hilo.

“Yaani  tunapata shida sana, kila siku tunashinda hapa asubuhi mpaka jioni  bila kupata wateja,  kwa hiyo inatulazimu unapotoka nyumbani lazima uwe na nauli na hela ya kula kwa sababu  bila hivyo unashinda njaa,” alisema lucy Jonh na kuongeza:

“Tunaiomba serikali ivunje soko la Karume, ambalo ndilo linajulikana sana na watu na wafanyabiashara wakihamia huku labada ndio inaweza kuwa afadhali kwetu, lakini bila hivyo kwa kweli tutashindwa.”

Jengo hilo la Machinga Complex lina vizimba 4,206, ambapo baadhi bado havijananza  kutumika kutokana na wafanyabiashara wengi kukimbia kufanya biashara katika eneo hilo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: