ANGALIA LIVE NEWS
Tuesday, September 13, 2011
Chadema yaigeuzia kibao CCM
Daniel Mjema na Joseph Zablon, Igunga
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa tuhuma nzito dhidi ya CCM kuwa kiliandaa kambi za vijana mahsusi kwa ajili ya kufanya vitendo vya kijasusi, ikiwamo kuwamwgia tindikali na upupu wafuasi wa vyama vingine.
Chadema pia kimedai kuwa CCM kimekodisha kikundi cha vijana 20 kutoka Tarime, Mara ili kuwakatakata watu mapanga kama ilivyotokea katika uchaguzi mdogo katika majimbo ya Tarime, Busanda na Biharamulo.
Tuhuma hizo zilitolewa jana mjini hapa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Chadema, Mwita Waitara mbele ya maofisa waandamizi kutoka makao makuu ya jeshi la polisi nchini akiwamo Naibu Kamishina wa Polisi, Isaya Mngullu.
Maofisa wengine waliohudhuria mkutano huo uliokuwa chini ya Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga, Richard Kalele ni Mkuu wa Kikosi cha FFU Makao Makuu, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Telesfory Anaclet.
Kikao hicho kiliitishwa pamoja na mambo mengine, kupitia upya ratiba za kampeni za vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa jimbo hilo na kujadili tukio la mfuasi wa CCM, Mussa Tesha kumwagiwa tindikali Ijumaa iliyopita.
CCM yaituhumu polisi
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa CCM, Matson Chizii ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumzia suala la tindikali na kuilaumu waziwazi polisi kuwa walichelewa kuchukua hatua hata baada ya wafuasi wa CCM kuripoti tukio hilo kwao.
“CCM tunawalaumu (polisi) walichelewa kwa sababu watu wetu waliripoti mapema lakini baadhi ya watendaji wa polisi waliokuwa kituoni, waliwajibu watu wetu kuwa hayo ni mambo ya kisiasa… hili si jambo la siasa ni jinai,” alisema Chizii.
Mngullu alimtaka Chizii kuwataja watu waliofika polisi kuripoti tukio la tindikali... “Tusaidie hao waliofika polisi wakapewa majibu kuwa hayo ni mambo ya kisiasa ni nani, ilikuwa ni lini na saa ngapi ili tutafute nani walikuwa zamu siku hiyo tuweze kuchukua hatua… tunaomba sana utusaidie kwa hili.”
Chizii alisema pamoja na kusuasua huko kwa polisi baada ya tukio hilo kuripotiwa, bado chama hicho kinahitaji majibu kutoka mamlaka za vyombo vya dola katika kutafuta ukweli wake.
“Tumerekodi maneno ya kijana yule na ametuambia yote, amewataja wale waliomteka wakati akienda kubandika mabango na kumfanyia ukatili ule na hata jana tumeongea naye bado macho hayaoni… tunasubiri majibu ya polisi,” alisema.
Mkurugenzi huyo akaenda mbali na kudai kuwa anazo taarifa za chama kimoja cha siasa ambacho hata hivyo, hakukitaja alichodai kuwa kilifanya vikao vyake vya siri na kukubaliana kuongeza ulinzi na nguvu ya kupambana na polisi waliopo Igunga.
“Ninazo taarifa za chama fulani hapa lakini sitakitaja kwamba sasa wataongeza ulinzi, wataongeza nguvu kupambana na polisi na wataongeza nguvu kwa kushirikiana na kamati zao zenye silaha… ikitokea hivi, Igunga itakuwa salama kweli?,” alihoji.
Katibu wa CCM Wilaya ya Igunga, Neema Adamu alisema alitaarifiwa juu ya tukio hilo saa 2:00 usiku na hapohapo akamtaarifu Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Igunga (OCD), Issa Muguha.
“Nilipopigiwa tu simu saa 2:00 kwamba kijana wetu ametekwa nilimpigia OCD na ilipofika saa 4:00 usiku nikapigiwa tena kwamba amepatikana lakini, hali yake si nzuri… nilifika polisi vijana wakaniambia majibu ya polisi hayakuwa mazuri,” alisema.
Kalele aliingilia kati mvutano huo na kutaka suala hilo liachiwe vyombo vya dola na mwenye taarifa sahihi aziwasilishe huko ili zifanyiwe kazi.
Waitara aguswa
Lakini maelezo hayo ya viongozi wa CCM yalionekana kumgusa Waitara ambaye alilazimisha apewe fursa ya kutoa maoni yake na ndipo aliposema itakuwa ni jambo la hatari kama polisi wanapewa taarifa lakini hawachukui hatua.
Mkurugenzi huyo alitoa mifano ya matukio ambayo bendera za chama chake zilichomwa au kuchanwa na kudai kwamba aliwahi kutoa taarifa polisi kuwa ameona gari moja katika ofisi za chama kimoja huku watu wakigawana mapanga.
Alisema suala la kuandaa kambi za vijana liliwahi kuzungumzwa na ofisi za polisi na Takukuru kwamba CCM wamekusanya vijana na kuweka makambi kwa wiki moja katika maeneo ya Uyui, Kiomboi, Uloni na Nzega kuanzia Septemba 4, mwaka huu.
“Mimi ninazo taarifa wapo vijana 20 wamekodiwa Tarime na wamewasili Igunga jana (juzi) saa 3:00 usiku. Wana upupu na mapanga… yupo kijana mmoja amerudi Chadema akitokea CCM tumemrekodi kila kitu na ushahidi upo,” alidai.
Akizungumza kwa kujiamini, mkurugenzi huyo alidai kuwa miongoni mwa mambo waliyoelezwa na vijana waliokuwa katika makambi hayo ni kwamba wameandaliwa wakapambane na kuleta vurugu kwenye kampeni hizo.
“Tulifanya uchaguzi Tarime watu walikatwa mapanga na hakuna watu waliokamatwa, Busanda na Biharamulo hivyohivyo na hivi sasa wapo Igunga… watu wana pingu, wana bastola na wanajifanya ni watu wa usalama wa taifa,” alisema Waitara.
Akizungumzia malalamiko ya wanasiasa hao, Kamanda Anaclet alivilaumu vyama vya siasa kwa kile alichoeleza kuwa ni kutokutoa ushirikiano wa kutosha kwa polisi wanapohitaji kukusanya ushahidi na vielelezo kwa ajili ya kuchukua hatua.
“Mtu anakuja analalamika bendera imechomwa moto mahali unamwambia ilete basi hata hiyo bendera au katuonyeshe eneo la tukio hatoi tena ushirikiano… tunawaambia tuleteeni mashahidi hamleti tutapelekaje kesi mahakamani?” alihoji.
Kuhsu suala la tuindikali, Kamishna Mngullu alisema tayari polisi wanayo majina ya watu wanaotajwa kuhusika na wanayafanyia kazi ingawa hawafahamu kama ni wafuasi wa chama cha siasa au la.
Alisema matukio yote yaliyotolewa taarifa polisi, yatafanyiwa kazi na majibu kurejeshwa kwa viongozi hao wa kisiasa huku akisisitiza kuwa polisi wamejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika kwa amani.
Angalizo la msimamizi wa uchaguzi
Kalele aliwataka viongozi wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo kuendesha kampeni zao kwa amani akionya kwamba kinyume chake utamalizika huku baadhi ya wafuasi wao wakiwa gerezani au majeruhi.
“Kampeni za kubeba silaha si kampeni, mnatakiwa kuwaambia wananchi chagua chama hiki au chagua chama changu si uvunjifu wa amani. Wananchi wa Igunga hawataki fujo na polisi mchukue hatua haraka mnapopewa taarifa,” alisema.
Kadri kampeni za uchaguzi huo zinavyozidi kupamba moto, ndivyo vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo vinavyoshutumiana na mchuano mkali umekuwa zaidi kwa vyama vya CCM, Chadema na CUF.
CCM kinarejea kwenye kampeni zake leo baada ya kusitisha kwa muda wa siku mbili kwa ajili ya kuomboleza vifo vya abiria zaidi ya 200 waliofariki dunia baada ya meli waliyokuwa wakisafiria kupinduka na kuzama baharini huko Zanzibar.
Mwananchi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment