ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 5, 2011

Magufuli akingiwa kifua bomoabomoa




Waandishi wetu
UAMUZI wa Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli, kuendelea na bomoabomoa kwa watu wote waliojenga katika hifadhi ya barabara nchini umeungwa mkono na wanazuoni ambao walisema siasa ziwekwe kando katika utekelezaji wake.Wasomi hao ambao walizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti jana, walisema mkakati wa Magufuli kubomoa nyumba zote zilijengwa kwenye hifadhi ya barabara ni halali kwa sababu ni makosa kisheria watu kujenga katika maeneo hayo. Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Jumatano wiki hii, Waziri Magufuli aliwatahadharisha watu waliojenga kwenye hifadhi ya barabara kwamba nyumba zao zitabomolewa kwa operesheni bomoabomoa itakayoanza hivi karibuni.Magufuli alisisitiza kuwa, hakuna atakayemzuia kutekeleza azma yake hiyo kwa vile anafuata sheria ya nchi ambayo Rais Jakaya Kikwete ameibariki kutumika wa kutia saini.


Agizo hilo la Dk Magufuli linakuja takribani miezi mitano baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete kwa nyakati tofauti kumzuia kuendelea na bomoabomoa aliyokuwa anaitekeleza sehemu mbalimbali nchini.
Machi 6, mwaka huu, akiwa ziarani mkoani Kagera, Waziri Mkuu Pinda alisimamisha bomoabomoa katika hifadhi ya barabara nchi nzima hadi itakapoamuliwa vinginevyo na Baraza la MawaziriMachi 20 mwaka huu, Rais Kikwete alipotembelea Wizara ya Ujenzi akamshauri Magufuli kuzingatia utu na historia ya eneo wakati akitekeleza bomoabomoa.Alisema litakuwa jambo la ajabu kama kubomoa nyumba ya sanaa au kihistoria iliyopo katika hifadhi ya barabara.
Kutokana na maagizo hayo ya wakuu wake wa kazi, Dk Magufuli alisimamisha bomoabomoa zilizokuwa zinaendeshwa nchi  nzima.  Hata hivyo, wakati Rais Kikwete akizindua Barabara ya Singida-Manyoni, Dk Magufuli alisisitiza kuwa atafufua bomoabomoa kwa maeneo yote ya hifadhi za barabara kwa kutumia sheria zinazomruhusu kufanya.Wakiunga mkono tangazo jipya la bomoabomoa lililotolewa na waziri Dk Magufuli, wanazuoni waliozungumza na Mwananchi Jumapili walisema kwamba, hifadhi za barabara zimewekwa kisheria hivyo zinatakiwa kuheshimiwa na hatua ya kubomoa nyumba zilizojengwa katika maeneo hayo ni halali.

Profesa Ngowi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dk Honest Ngowi, alisema wakati umefika kwa viongozi wa Serikali kuacha siasa, akisisitiza kuwa maamuzi yanayotakiwa kutolewa na wataalamu yasiingiliwe.
“Unajua kila kiongozi akiwa anasema lake katika mambo ya kisheria kama hili la bomoabomoa ujue wazi kwamba, siasa zinaanza kuingizwa katika utendaji,” alisema Dk Ngowi.
Alifafanua kwamba, sheria ya Tanzania inaeleza wazi kuwa si ruhusa kujenga katika hifadhi ya barabara, hivyo wanapoibuka watu na kupingana na sheria hiyo ni kinyume na taratibu zilizowekwa ili zifuatwe.

Profesa Rwegasira
Profesa Delfin Rwegasira wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema uamuzi juu ya ubomoaji wa nyumba zilizopo katika hifadhi ya barabara, ni halali lakini lazima lifanywe na wataalamu tena kwa umakini wa hali ya juu.“Jambo hili la upanuzi wa miji na ujenzi wa barabara lina mambo mengi…, lazima wingi wa watu utazamwe, pamoja na taratibu za kuwafidia watakaobomolewa nyumba zao,” alisema Rwegasira.Alitahadharisha kuwa katika utekelezaji wa suala hilo siasa hazitakiwi kuingizwa, badala yake waachiwe wataalamu.

Profesa Safari
Naye Profesa Abdallah Safari, ambaye kitaaluma ni mwanasheria alisema kuwa, kila kitu kilichopo katika hifadhi ya barabara kinatakiwa kubomolewa kwa mujibu wa sheria.
“Nakumbuka wakati wakipanua barabara ya kwenda Mbagala, kuna msikiti ulibomolewa, watu walilalamika lakini baadaye mambo yakaisha.  Hiyo ndiyo maana ya sheria, lazima itekelezwe,” alisema Safari.
Alisema Rais anachoweza kufanya ni kutoa msamaha kwa wafungwa na si kwa waliojenga katika hifadhi ya barabara, kwani kwa kufanya hivyo atakuwa amekiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hata hivyo, pamoja na kuunga mkono hatua ya Dk Magufuli, baadhi ya wahadhiri walisema inaonekana kuna mgongano wa maamuzi katika Serikali ambayo yanatakiwa kusahihishwa haraka.

Profesa Wangwe
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mkurugenzi  wa Taasisi ya Utafiti Kuhusu Kuondoa Umaskini (Repoa),  Profesa Samweli Wangwe, amesema haoni kama huko ni kugongana kwa kauli ila ni ushauri.Hata hivyo, alisema kutoa ushauri kama huo katika majukwaa ya siasa inaleta picha mbaya kwa wananchi.“Mimi ninachoona ni kwamba alipewa ushauri siyo mgongano, sema huo ushauri siyo vizuri kuutolea kwenye majukwaa, ingepaswa aambiwe wakiwa wenyewe,” Profesa Wangwe alisema na kuongeza:
“Sheria inataka nyumba zibomolewe, zisipobomolewa itakuwa ni kuvunja sheria, kwa hiyo ingebidi aambiwe jinsi ya kuzivunja ili kusiwe na athari sana.” 

Kulipa fidia
Alipoulizwa kuhusu fidia kwa watakaokumbwa na bomoabomoa hiyo,  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, alisema waliojenga kwenye hifadhi ya barabara hawatalipwa fidia, isipokuwa wale barabara itawafuata watalipwa.Akizungumza kwa njia ya simu  na Mwananchi Jumapili jana, Prof Tibaijuka alisema kuwa, kazi ya wizara yake ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata haki , lakini akaonya kuwa watakaokuwa wamevunja sheria kwa kujenga ndani ya hifadhi ya barabara hawana haki.
Januari 13, mwaka huu Magufuli aliagiza kuwa wananchi waliojenga katika hifadhi ya barabara waaanze kubomoa nyumba hizo mapema na kwamba wasitegemee kulipwa fidia.
Pia alimtaka Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam pamoja na madiwani kujipanga na kuondoa nyumba zilizopo katika maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya njia ya mabasi yaendayo kasi ili kuwawezesha makandarasi kuanza kazi hiyo.Waziri Magufuli amekuwa akisisitiza kwamba waliojenga ndani ya barabara wamevunja sheria namba 13 ya mwaka 2007  na kwamba hawastahili kulipwa fidia.
Mwananchi

No comments: