Monday, September 5, 2011

Mapenzi ni ugonjwa wa moyo, ni asali inayotuliza moyo – 2

MUNGU aliye mpaji wa viumbe wote ndiye ametufanya tukutane tena leo kwenye safu hii. Tumshukuru kwa ukarimu anaotutendea, kwani asingetaka mimi na wewe maelezo yangekuwa tofauti hivi sasa.

Mada yetu ni ile ile. Kila mtu anahitaji mapenzi lakini wanashindwa kuyaelewa. Hawayatendei haki inavyostahili kwa kukosa uvumilivu.Jambo dogo linaweza kugharimu uhusiano na watu wakaachana huku wakijiapiza.

Wiki iliyopita nilichambua maeneo mengi lakini leo nagusa zaidi matatizo yanayozunguka mapenzi ambayo ni chanzo cha kuyafanya yaonekane ni tata.Yapo kwa kila uhusiano, kama moja halikugusi basi lingine litakuwa linakupa mateso.


KUKOSA FURAHA
Katika uhusiano, ni hatari sana pale mmoja anapoweza kufurahi, mwingine akawa hana amani. Ikitokea wahusika wakaona sawa kuwepo kwa utofauti huo ni sawa na kuliweka njia panda penzi lao.

KUTOAMINIANA KIHISIA
Inatokea mara nyingi kwamba mmoja anaamini yeye ndiye anayependa kuliko mwenzake. Huyo anaamua kushusha tuhuma kwamba hapendwi inavyotakiwa. Mfano ni kauli hii: “Najua hunipendi kama mimi ninavyokupenda.”

Mtazamo huo ni sababu ya kuwepo kwa penzi linazungukwa na shaka ndani yake. Uhusiano thabiti ni ule ambao wawili walioamua kupendana wanakuwa wanaishi na imani timilifu. Asitokee mmoja akawa anapenda kwa moyo mmoja mwingine ‘anamuinjoi’ mwenzake. Yaani anamcheza shere.

Wakati mwingine siyo kwamba mmoja ndiye anapenda zaidi, isipokuwa ni hisia zinazozunguka mapenzi. Wanasema, “wasiwasi wa mapenzi unaweza kuua kwa sababu ya kuwaza mambo ambayo mara nyingi yanakuwa si ya kweli.”

Kimsingi, hisia za kuona wewe ndiye unahusika zaidi kwenye mapenzi kuliko mwingine hazitakiwi. Jambo ambalo unaweza kufanya ili kuupa afya uhusiano wako ni kuzungumza na mwenzako pale unapotilia shaka mwenendo wake.

KOSA KUBWA
Watu wengi wamekuwa hodari kuhesabu mambo ambayo wanayafanya kwa wapenzi wao na kulinganisha na yale wanayotendewa. Mfano ni kiwango cha zawadi, kupigiana simu na SMS, wakati mwingine huingia mpaka kwenye familia kwa mmoja kudai mwenzake hajali ndugu wa upande wa pili.

“Yaani mimi nawajali ndugu zako lakini wewe huwajali wangu. Nimemnunulia simu mama mkwe wangu, wewe hata kipande cha kanga hujawahi kumnunulia wakati uwezo unao.” Hizo ni tuhuma ambazo mara nyingi huyafanya mapenzi yasiwe rahisi.

Ni kosa kubwa kuhesabu wema wako kwa mwenzi wako. Ni vema ukatambua kuwa usipomfanyia hivyo wewe, unataka nani mwingine afanye? Mwisho utapata jibu lililonyooka kuwa unayotekeleza ni wajibu wako, kwa hiyo fanya kwa moyo mweupe.

Kama umemnunulia simu mama mkwe wako, hilo ni jambo jema kwako, kwani umepalilia shamba lako. Yeye kama haoneshi kumjali mama mkwe wake, mkumbushe kila unapoona inafaa (siyo kila wakati, ataona kero). Akishindwa kabisa fukia mashimo.

Ni kwa namna gani utafukia mashimo? Jibu ni hili.Shadya ameolewa huu ni mwaka wa 15. Mume wake anaitwa Fadhil. Anasema kuwa baada ya kugundua kuwa mume wake ni mzito katika masuala ya kifamilia, aliamua kuwa anatimiza mambo yake mwenyewe huku sifa nyingi zikienda kwa Fadhil.

Anasema: “Mume wangu hana tatizo la kifedha.Uwezo wake ni mkubwa. Kinachomsumbua ni muda wa kushiriki mambo ya familia, hasa upande wangu. Nilizungumza naye sana lakini hakubadilika. Niliumia lakini siku nilipomuelewa, kila kitu kilikaa vema.

“Niligundua mume wangu ni mzito, kwa hiyo nilichofanya ni kumwakilisha. Naweza kununua nguo nikampa mama yangu lakini kule namwambia mama kwamba amenunuliwa na mkwe wake. Siku nikimnunulia kitu mama mkwe (mama yake), najisema ni mimi.

“Likitokea tatizo upande wa familia yangu, namhimiza mume wangu twende, siku akishindwa naweka maneno matamu ya kumtetea. Kama kunahitajika mchango, natoa halafu nasema aliyetoa ni yeye. Hiyo imefanya familia yangu imuone mume wangu ni mtu wa karibu kwao.

“Mume wangu alikuwa anapokea asante nyingi kwa vitu ambavyo mimi nimefanya kwa niaba yake. Zile asante zilimshtua. Taratibu akaanza kuhusika japo siyo sana. Sijawahi kugombana na mume wangu kwa sababu nilimuelewa, siyo mbaguzi lakini ni mzito.”

NI ELIMU PIA KWAKO
Alichokifanya Shadya ni kufukia mashimo. Jambo ambalo aliona mume wake angeweza kulitekeleza lakini akashindwa kwa sababu za kibinadamu, aliamua kulisimamia mwenyewe. Hakulaumu wala kukaa na donge moyoni.

Uamuzi huo umesababisha ndoa istawi. Maisha yanaendelea na hakuna kulaumiana. Hebu na wewe fanya unaloweza, unachoona mwenzi wako anashindwa, angalia kama ni makusudi au upungufu alionao kibinadamu. Kama ndivyo, basi fukia mashimo.

Kufukia mashimo hakuna maana ya kufanya kitu mbadala kama Shadya, unaweza kufukia kwa kupuuza vitu vidogo. Yaani usiweke moyoni mambo badala yake puuza halafu umtanie kwamba kuna vitu anashindwa.

Unapenda kumkumbatia mwenzi wako kila sehemu lakini yeye ni mwingi wa aibu, usikimbilie kufikiria kuwa hapendi kuonekana wewe ni mpenzi wake, tupia akili yako upande wa pili kuwa hana ujasiri wa kupigana mabusu na kukumbatiana mbele za watu.
Itaendelea wiki ijayo.

www.globalpublishers.info

No comments: