Monday, September 5, 2011

Igunga: Kimbunga chaanza


Kimbunga cha uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Igunga, mkoani Tabora kinaaza leo ambapo wagombea wa vyama vitatu vya siasa vinavyopewa nafasi ya kulinyakua jimbo hilo wataanza kurejesha fomu kwa msimamizi wa uchaguzi huo leo na kesho.
Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo mdogo, Dk. Peter Kafumu, leo anatarajia kurejesha fomu yake katika ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Igunga, Protace Magayane.
Wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Chama Cha Wananchi (CUF), Joseph Mwandu Kashindye na Leopard Mahona, wanatarajia kurejesha fomu hizo kesho ambayo ni siku ya mwisho wa kurejeshwa kwa fomu hizo na kufuatiwa na kuanza kwa kampeni za uchaguzi huo keshokutwa.

Kwa mujibu wa Magayane, mwisho wa kurudisha fomu hizo ni kesho saa 10:00 jioni huku na taratibu za kuweka pingamizi zikiendelea.
Mpaka sasa ni vyama sita vinawania kiti hicho cha ubunge kilichoachwa wazi na Rostam Aziz (CCM) aliyejiuzulu nafasi hiyo sambamba na ujumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM kupitia Mkoa wa Tabora akidai kuchoshwa na siasa uchwara, fitina na kuandamwa ndani ya chama hicho Julai 13, mwaka huu.
Vyama vingine vinavyowania kiti hicho na majina ya wagombea wake katika mabano ni UND (Lazaro Ndegaya), DP (Said Makeni) na Sau (John Maguma). Awali, TLP kilisimamisha mgombea ambaye hata hivyo, alijitoa kwa madai ya kutelekezwa na chama hicho.
Tayari CUF kimeshaweka wazi kuwa kampeni zake zitazinduliwa na Mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba, na Katibu Mkuu wa chama hicho, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoundwa baada ya uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Chadema hakijataja tarehe rasmi ya kuzindua kampeni zake wala kiongozi wake atakayezizindua.
Kwa upande wake, CCM nacho hakijataja tarehe ya uzinduzi wa kampeni, lakini kikao cha Kamati Kuu kilichoketi hivi karibuni jijini Dar es Salaam na kumpitisha Dk. Kafumu, kilimteua Rais Mstaafu, Benjamin Mkapa, kuzindua kampeni zake huku Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, akisema kuwa tarehe ya uzinduzi itatajwa ukifika wakati mwafaka.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Oktoba 2, mwaka huu baada ya kampeni kusitishwa siku moja kabla.

VYAMA VYAUNGANA KATIKA MSIBA
Wakati huo huo, wanachama wa CCM, viongozi wa chama hicho na vyama vingine vya siasa, juzi walishirikiana kikamilifu katika kuzika mwili wa mtoto Peter Zakaria, aliyefariki dunia Ijumaa iliyopita kwa kugongwa na lori aina ya Fuso katika maandalizi ya kumpokea Dk. Kafumu aliyekuwa anaingia jimboni humo kutokea Dar es Salaam.
Mratibu wa kampeni wa CCM, Lameck Mwigulu Nchemba, ambaye pia ni mbunge wa Iramba Magharibi, alisema msiba huo umekishtusha chama chake na wananchi kwa ujumla.
‘’Kwa kweli hatuna hali kabisa kwa hili lililotufika, lakini tunasema ni mipango ya Mungu, maana sote ni wa kwake, Chama kimegharimia shuguli zote za mazishi na tupo bega kwa bega na wafiwa, hatuwezi kuwaacha kwani hili limetufika,’’ alisema Nchemba wakati wa mazishi.
Kwa upande wake, Chadema kilitoa rambirambi ya Sh. 120,000 huku CCM wakitoa Shilingi milioni moja.
NAPE NNAUYE AWASILI
Katika hatua nyingine, Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, jana aliwasili katika Jimbo la Igunga kwa ajili ya shughuli za kampeni.
Nape aliwasili mchana na kwenda kutoa pole kwa familia ya mtoto Peter Ezekiel na kutoa ubani wa kiasi cha fedha ambacho hakutaka kukitaja.
”Nisingependa kusema mengi hapa, lakini naomba niwaombe kuwa watulivu wakati huu mgumu kwa msiba wa mtoto wetu mpendwa. Hii ni mipango ya Mungu, nimeona nipite hapa kuwapa pole kwa kuwa nilipata habari za msiba huu,” alisema Nape.
Msemaji wa familia ya mtoto huyo, Joseph Mlewa, alisema kuwa familia hiyo imefarijika kwa namna CCM ilivyoshughulikia msiba mwanzo hadi mwisho.
Msiba huo ulifuta shamrashamra na maandamamo yaliyokuwa yameandaliwa na uongozi wa CCM Wilaya ya Igunga kwa ajili ya kumsindikiza Dk. Kafumu kuchukua fomu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: