Monday, September 5, 2011

Maisha ya Wazanzibari mashakani India


Vijana saba kutoka Zanzibar wamekwama mjini New Delhi, India, baada ya kukataliwa kujiunga na chuo kikuu kwa kukosa sifa za kusomea kozi walizothibitishwa na serikali.
Vijana hao ambao wote ni wasichana walithibitishwa kupata sifa za kuchukua mafunzo mbalimbali katika Chuo Kikuu cha NIILM kilichopo nchini humo.
Habari zinasema baada ya kufika chuoni mwezi uliopita, wote wamekataliwa kujiunga.
Wanafunzi hao ni Hafsa M. Abeid, Latifa J. Hamis, Hawa Abdala, Sharifa Rashid, Tatu Haji, Aziza Abdala na Joha Lali Ramadhani.
Wanafunzi sita wameomba kwa wazazi wao msaada wa kurudi nchini baada ya kutakiwa kuondoka chuoni haraka.

Hata hivyo, Joha amefanikiwa kupata fedha kutoka kwa wazazi wake nchini na anajiandaa kujiunga na chuo kingine nchini humo.
Kwa mujibu wa taarifa, wanafunzi hao hawakufikia sifa zinazotakiwa na chuo hivyo kikalazimika kuwaamuru kuondoka.
Moja ya masharti ya chuo hicho wakati wa kujiunga ni ilani yao kwamba wanaweza kufuta nafasi ya mwanafunzi yeyote atakayethibitika kuwa alidanganya katika taarifa alizotoa wakati wa maombi.
Haifahamiki taarifa za vijana hao zimekutwa na upungufu gani lakini habari za ndani zilizofikia gazeti hili zimesema moja ya masharti ni mwanafunzi kuwa yatima – mtu ambaye wazazi wake au baba yake ameshafariki dunia.
Nyaraka mbalimbali zilizopatikana zinaonyesha kuwa wazazi wa wanafunzi hao sita wameiandikia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kuomba msaada wa kuwarudisha nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, wasichana hao kwa sasa wanaishi katika mazingira magumu kwa kuwa wanatakiwa kuondoka chuoni mara moja.
Habari zilizopatikana mjini hapa zinaonyesha kuwa vijana hao walikwenda India chini ya ufadhili wa Rai Foundation Colleges.
Vijana hao walithibitishwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ajili ya kozi mbalimbali na uhakiki wa maombi yao ulisimamiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar.
Vijana kadhaa waliwasilisha maombi ya nafasi ya masomo ya juu katika chuo hicho zilizotangazwa Machi 10, mwaka jana baada ya kupokea nafasi hizo kutoka kwa Rai Foundation Colleges inayoendesha chuo kikuu katika miji tisa nchini India.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, sifa zilizotajwa kwa waombaji kuwa nazo, ni kuwa mwanamke, hajaolewa, masikini, awe amemaliza elimu ya kidato cha nne au sita na cheti cha ngazi ya stashahada. Kwa masomo ya Art, muombaji awe na alama 4.5 au masomo ya sayansi alama 2.5 au shahada ya pili (GFA) 3.5. Mwisho wa maombi ilikuwa Machi 31, 2010.
Baada ya wanafunzi saba kuthibitishwa kuwa na sifa, taarifa zinasema, serikali kwa kuwa haikuwa na fedha za kuwagharamia, iliwataka wazazi wao wabebe mzigo huo.
Gharama zilizotakiwa kulipwa na wazazi wa wanafunzi hao ni dola 733 kwa ajili ya nauli na dola 400 kwa ajili ya gharama za chakula na malazi watakapokuwa chuoni. Jumla ni dola 1,133.
Kwa mujibu wa barua ya pamoja ya wazazi wa vijana hao sita, wanaiomba serikali isaidie kulipa gharama za nauli Sh milioni milioni 10 ili watoto wao warejee nchini haraka kabla ya kukumbwa na utata katika maisha yao ughaibuni.
Baadhi ya wazazi hao wanalalamika kwamba ilikuaje serikali ikaidhinisha safari ya watoto hao na sasa waambiwe kuwa hawana sifa na wamefukuzwa chuo.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Abdalla Mzee Abdalla amekiri kupokea barua ya wazazi wa watoto hao sita ya kuomba msaada wa serikali kuwarudisha watoto hao nyumbani.
Mzee alisema wizara imeshaagiza Ubalozi wa Tanzania nchini India kufuatilia suala hilo na kutuma taarifa haraka ili hatua zinazofaa zichukuliwe.
Kuhusu kwanini wanafunzi waliidhinishwa wakati hawakuwa na sifa zilizotajwa na chuo, alisema matatizo yaliyotokea Wizara yake haihusiki lakini inaendelea na juhudi za kufuatilia tatizo hilo.
Kwa mujibu wa tovuti ya taasisi ya Rai, ilianzishwa mwaka 2002 na tajiri aitwaye Dk. Vinay Rai. Taasisi hiyo ina zaidi ya wanafunzi 11,000 katika vyuo vipatavyo 40 katika miji 20 nchini India. Wanufaikaji wakuu wa fursa hiyo ni wasichana fukara wanaolipiwa malazi na chakula.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: