ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 7, 2011

Mnyika, Azzan, Mtemvu watema moto D’Salaam

Migogoro ya uuzaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA), tuhuma za ubadhirifu katika Shirika la Maendeleo ya Uchumi Dar es Salaam (DDC) na ugawaji wa vizimba vya biashara katika Jengo la Machinga Complex, jana ilisababisha kuvunjika kwa kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji la Dar es Salaam.
 Kikao hicho kilivunjika baada ya wajumbe wa baraza hilo kuhoji muhtasari wa vikao vilivyopita, ambavyo vilijadili masuala hayo, lakini hayakuwamo kwenye nyaraka zilizokuwa zimesambazwa kwa wajumbe.

Hoja hiyo iliibuliwa na Mbunge wa Kinondoni, Idd Azzan, katika kikao hicho, ambaye alihoji kuwa inakuweje muhtasari wa mwaka 2010 uthibitishwe Septemba mwaka huu wakati mambo ya hivi karibuni yaliyopitishwa na Halmashauri hiyo hayamo kwenye orodha.


Azzan alisema kwa mujibu wa kanuni za baraza hilo kila baada ya miezi mitatu wanatakiwa kukutana na kupatiwa muhtasari wa vikao vilivyopita, kabla ya kuendelea kujadili masula mapya.

Mbunge huyo alipendekeza kikao hicho kisifanyike ili viongozi waliohusika katika suala hilo wajifunze na kamati husika ikae na kuangalia jambo hilo kwani walifanya uzembe na hawawezi kuendelea kuvunja kanuni.

Alisema kama mikutano hiyo ilifanyika hivyo wangetakiwa kupatiwa muhtasari wa vikao vilivyofanyika kwani ilikuwa ni ya muhimu kuifahamu.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Diwani wa Hananasifu, Abas Tarimba, ambaye alieleza kuwa muhtasari huo ni muhimu ili wajue kilichofanyika katika vikao vilivyopita.

Alisema hawawezi kuendelea na kikao hicho mpaka hapo watakapopatiwa muhtasari kwa mujibu wa kanuni wa baraza hilo ili kuuthibitisha.

Naye, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, aliunga mkono hoja hiyo na kuhoji sababu za hoja yake ya kutaka taarifa kamili ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu (CAG), kuhusu ukaguzu wa Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo Mkoani na nchi za jirani cha Ubungo (UBT), haikuwekwa katika orodha ya mambo ambayo yangejadiliwa.

Akijibu hoja hizo, Mkuruhenzi wa Jiji, Bakari Kingobi, alikiri kufanya kosa kwa kutowasilisha muhtasari wa vikao vilivyopita na kuahidi kuwasilisha katika kikao kijacho cha madiwani, lakini alipingwa na wajumbe wakipendekeza kuwa kikao cha jana kivunje ili muhutasari huo uwasilishwe.

Kingobi pia alisema hoja ya Mnyika ingesikilizwa katika kikao kijacho.

Mara baada ya Kingobi kuzungumza Meya wa jiji, Dk. Didas Masaburi, aliwataka wajumbe kuendelea na kikao hicho kwani kukosekana kwa muhtasari huo sio sababu ya kuvunjika kwa kikao hicho.

Kauli hiyo iliibua minong’ono na hatimaye, Mnyika alisimama na kueleza kuwa kuendelea kwa kikao hicho ni sawa na kuvunja kanuni za baraza hizo.

Mnyika alisema pamoja na mambo mengine, kanuni zinamtaka Mkurugenzi wa jiji kuwasilisha taarifa za vikao zilizopita ili zithibitishwe kama zipo sahihi.

Naye Mbunge wa Temeke, Abas Mtemvu, aliungana na Mnyika na kueleza kuwa haina haja ya kurudishwa nyuma kwa kupatiwa muhtasari na kwamba walitakiwa kupatiwa taarifa za vikao vilivyofanyika hivi karibuni.

Mtemvu alisema ni lazima muhtasari uwasilishwe ili wajumbe wote wazipitie ndipo waanze kujadili mambo mapya.

Baada ya kutokea kwa mvutano huo, walimtaka Mkurugenzi huyo kupeleka taarifa ni kwa nini limetokea tatizo hilo ili watendaji wachukuliwe hatua.

Mnyika pia alisema kuwa Mkurugenzi huyo anahusika katika uzembe huo na ni mmoja wa watuhumiwa wa sakata hilo la kukwamisha muhtasari.

Kutokana na hali hiyo wajumbe hao walijadili hoja moja kutafuta mtaa ambao utaitwa jina la mji wa Hamburgischen nchini Ujerumani katika jiji la Dar es Salaam, walipendekeza mtaa wa Garden ubadilishwe ili kukidhi mahitaji hayo.

Alifunga kikao hicho, Meya Masaburi alisema kuwa madiwani hao wapo makini na kwamba amemuagiza Mkurugenzi wa jiji kuwasilisha taarifa hizo katika kipindi cha wiki tatu ili wapange kikao kijacho.

Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa kikao hicho Azzan aliwaambia waandishi wa habari kuwa kuna mchezo mchafu ambao wanataka kuufanya kwani haiwezekani wasipatiwe muhtasari wakati walitakiwa kuzipitia kwa mujibu wa kanuni.

Alisema kuna mambo muhimu ni ambayo kikao kilichopita kilijadili yakiwamo bajeti ya Jiji, sakata la UDA, DDC, UBT na Machinga Complex.

Azzan alisema wajumbe walitakiwa kupatiwa muhtasari huo ili wajue kama kuna mapungufu yalitokea au la.

Baraza hilo linaundwa na madiwani tisa kutoka Manispaa tatu za jiji la Dar es Salaam kila moja ikitoa madiwani watatu, wabunge wanane kutoka majimbo ya Jiji la Dar es Salaam, mameya watatu wa manispaa hizo na wabunge wawili wa viti maalumu.

Kumekuwa na mgogoro ulijijenga kati ya Meya wa Jiji na baadhi ya wabunge wa jiji, kuhusiana na Machinga Complex, Uda na DDC. Wabunge wa Dar es Salaam walimtuhumu Meya Masaburi kuhusika katika uuzaji wa Uda kinyemelea. 

Waziri Mkuu alimwagiza Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kukagua taasisi hizo. Kazi hiyo bado inafanyika.
CHANZO: NIPASHE

No comments: