ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 22, 2011

Mradi wa umeme megawati 600 wasainiwa



Ule mradi wa umeme wa makaa ya mawe ambao umeimbwa kwa miaka na miaka hatimaye umepata uhai baada ya Serikali jana kusaini mkataba wa ubia na kampuni ya Sichuan Hongda Group ya nchini China kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya chuma na makaa  ya mawe, mradi ambao unatarajia kugharimu Dola za Marekani bilioni tatu (Sh. trilioni 4.8).
Kupitia mpango huo, wawekezaji watazalisha megawati 600 za umeme kati hizo, 300 zitaingizwa kwenye Gridi ya Taifa na nyingine zitatumika maeneo ya uzalishaji.

Mradi huo ni mkubwa kuliko miradi yote iliyowahi kuanzishwa katika sekta ya madini nchini na fedha zake zinakaribia nusu ya bajeti ya serikali kwa mwaka huu wa fedha ambayo ni Sh. tilioni 13.


Katika mradi huo serikali itaambulia asilimia 20 ya mapato huku asilimia 80 ikichukuliwa na Schuan Hongda Group ambayo imekubali kuwekeza kwa asilimia 100 katika mradi huo.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana baada ya serikali kutiliana saini mkataba na kampuni hiyo, ambapo kazi hiyo inatarajia kukamilika na kuanza uzalishaji wa umeme na uchimbaji wa chuma ndani ya miaka mitatu ijayo.

Mwenyekiti wa Bodi ya  Shirika la Maendeleo (NDC), Dk. Chrisant Mzindakaya, alisaini mkataba huo kwa niaba ya serikali na kampuni ya Sichuan Hongda Group iliwakilishwa na Mwenyekiti wake wa Bodi, Liu Canglong.

DK. BILAL: MRADI HUO NI FAIDA KUBWA
Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal, ambaye alikuwa mgeni rasmi, alisema uanzishwa wa miradi hiyo ni faida kubwa kwa taifa na kwa wananchi wake.

Alitaja baadhi ya faida hizo kuwa ni pamoja na kuongeza ajira,  kukuza pato la taifa na kupata majibu sahihi kuhusiana na tatizo la nishati ya umeme.

WAZIRI CHAMI: UTASAIDIA AJIRA, MIUNDOMBINU
Akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kusainiwa kwa mkataba huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, alisema mchakato wa kutaka kuingia ubia katika mradi huo ulianza mwaka 2007 na kuhitimishwa jana.

Alisema mradi huo una manufaa makubwa kwa taifa kwa kuwa utasaidia upatikanaji wa ajira, ujenzi wa miundombinu ikiwemo reli, barabara na bandari pamoja na kuongeza mapato ya serikali.

Alisema mradi wa Mchuchuma unatoa makaa ya mawe na ule wa Liganga unazalisha chuma ghafi ambacho kitatumika katika viwanda vya ndani na sehemu nyingine itauzwa nje ya nchi.

MZINDAKAYA: PIGO KWA WALIOPINGA
Kwa upande wake, Dk. Mzindakaya, alisema awali watalaam waliofanya utafiti walitoa taarifa za uongo kuwa malighafi iliyopo katika miradi hiyo ilikuwa inaonekana kama uyoga na kwamba ilikuwa juu hivyo ingekwisha muda mfupi baada ya kuanza kuchimbwa.

Hata hivyo, alisema watalaamu waliofanya utafiti mara ya pili walitoa matokeo tofauti ambayo walisema madini hayo ni mengi na yanafikia mita 500 kutoka juu ya ardhi. 

Alisema miradi ya barabara, reli, bandari na usambazaji wa umeme itaanzishwa, ingawa haipo katika mkataba kwa kuwa bila kufanya hivyo viwanda vya kuchimba chuma ghafi na makaa ya mawe haviwezi kumudu kufanya kazi zake.

Alisema ifikapo mwaka 2018, NDC inatarajia kuzalisha megawati 1,800 za umeme kupitia miradi yake ya Kiwira, Mchuchuma na Ngaka na hivyo kusaidia kumaliza tatizo la nishati hiyo nchini.

Alisema mkataba huo unatoa nafasi kwa NDC kuendelea kununua hisa zake hadi kufikia asilimia 49 baada ya mbia mwenzake kurudisha gharama zake alizotumia katika kuanzisha mradi huo.

Dk. Mzindakaya ambaye ni mwanasiasa wa siku nyingi, aliwaponda wanasiasa wenzake waliokuwa mstari wa mbele kupinga uanzishwaji wa mradi huo na kuwaita kuwa “mafundi” wa kuzuia miradi mikubwa.

Hata hivyo, alijigamba kuwa baada ya mabishano ya muda mrefu hivi sasa Rais Jakaya Kikwete na Baraza la Mawaziri wameridhia na kwamba hakuna  tena mtu wa kuzuia miradi hiyo isianzishwe.

“Hakuna mtu wa kuzuia mradi huu mkubwa na wenye manufaa makubwa kwa taifa, maana kuna watu ni mafundi wa kuzuia miradi mikubwa kama hii,” alisema. 

Kwa upande wake, Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, ambaye miradi hiyo imeanzishwa kwenye jimbo lake, aliipongeza serikali kwa kuthubutu kukubali kuingia ubia na kuanzisha mradi huo.

“Huu ni mradi mkubwa katika sekta ya madini ambao utaipatia serikali mapato kwa asilimia 20 tofauti na miradi mingine katika sekta ya madini ambayo serikali imekuwa ikiambulia asilimia tatu tu,” alisema. 

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na wabunge, viongozi wastaafu wa NDC, Balozi wa China nchini pamoja na wawakilishi kutoka Jimbo la Ludewa ambako mradi huo utatekelezwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: