Friday, September 2, 2011

`Polisi ndiyo chanzo kikubwa cha ajali nyingi za barabarani`



BaadhI ya majeruhi wa basi la kampuni ya Champion T 763 AEQ lililopata ajali na kuua watu wanane na wengine 53 kujeruhiwa likiwa safarini kutoka Mwanza kwenda jijini Dar es Salaam, wamelitupia lawama Jeshi la Polisi kuwa ndiyo chanzo kikubwa cha ajali zinazotokea barabarani.
Majeruhi ambao wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma wakiendelea kupatiwa matibabu, wamedai kuwa polisi wamekuwa wakiruhusu mabasi mabovu kubeba abiria baada ya kupokea rushwa bila kujali usalama wa Watanzania.
Madai hayo yalitolewa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. James Msekela, alipowatembelea majeruhi hao hospitali hapo juzi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya Mkuu wa Mkoa, majeruhi hao, Mohamed Sioji (54), mkazi wa Kijiji cha Senene Mvuri Kata ya Luhandi Tarafa ya Ntiko Singida Vijijini aliyelazwa wodi namba 11.
Sioji alisema polisi wamekuwa na tabia ya kupokea rushwa hata kama magari hayo yana makosa ambayo yanayoweza kusababisha ajali barabarani.
Alisema pamoja na ukaguzi wanaofanya kwa magari barabarani, lakini hawako makini katika kazi zao bali wanachojali zaidi ni fedha wanazopewa na kuyaruhusu yaendelee na safari.
Kwa upande wake, Raja Singa (35), mkazi wa jijini Dar es Salaam aliyelazwa katika wodi namba moja, aliiomba serikali kuweka sheria kali kwa madereva watakaosababisha ajali kwa uzembe.
Singa alipendekeza madereva hao wanyang'anywe leseni zao huku wamiliki wa magari yatakayobainika kuwa ni mabovu walipe fidia kwa watu wanaopoteza maisha yao na majeruhi.
Aidha, aliiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa (Takukuru), itumike kwa lengo la kuwakamata askari wanaopokea rushwa pamoja na madereva wanaotoa.
Alisema Takukuru ikitumika itasaidia kuondoa tatizo hilo la kuwepo kwa ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa kuondoa maisha ya watu ambao ni nguvu kazi ya taifa.
CHANZO: NIPASHE

No comments: