ANGALIA LIVE NEWS

Friday, September 30, 2011

Tabia sumu zitakazokufanya ukimbiwe na wanaume!

KUKATA tamaa ni ugonjwa mbaya maishani, kwa kuwa hapa tunazungumzia mapenzi, niseme kwamba kukata tamaa ya kupata mwenzi sahihi ni sumu hatari katika maisha ya mwanadamu.
Inaweza kukutoa uhai. Achana na tabia ya kuishi kwa historia, hata kama umeumizwa kiasi gani huko nyuma, amini kwamba wapo ambao wana mapenzi, wanaojua thamani ya kupendwa. Muda wa kukutana naye haujafika, lakini yupo. Vuta subira.

Rafiki zangu, utangulizi huo niaamini unaweza kuwapa nguvu baadhi ya wenzetu ambao wapo kwenye matatizo ya kuacha, kuachwa au kuachana na wapenzi wao. Nimesema mara nyingi sana, kuwa suala hili linaumiza kwa pande zote.
Yaani muachaji na muachwaji au waachanaji wote wana maumivu sawa, kubwa ni kwamba wawe walikuwa kwenye mapenzi ya dhati. Baada ya jambo hilo kutokea, ndipo maumivu yanapoanzia, hasa linapokuja suala la kutafuta mwenzi mwingine.
Wengi hupatwa na ganzi ya moyo, wakidhani kwamba si rahisi kupata mpenzi mwingine ambaye atakuwa na penzi la dhati. Si kweli, usikate tamaa rafiki. Sasa twende kwenye mada yetu ya msingi.
Nazungumzia juu ya tabia ambazo wanaume wengi hawazipendi, kwamba wakikutana na wanawake wenye nazo, uamuzi wao ni kuwaachana mara moja. Kwa nini? Kwa sababu si nzuri. Inawezekana unazijua au huzijui, lakini leo utapata nafasi ya kuzitambua na kuzifanyia kazi.
Wanawake wana hulka karibu sawa kama nilivyotangulia kusema katika makala zangu zilizotangulia, kwa upande wa wanaume ni tofauti kidogo, wanaume wana hulka tofauti kulingana na matakwa na utashi wao, japokuwa kuna baadhi ya vitu huwa wanakaribiana sana hasa katika kutoa uamuzi.
Wanaume wengi hufikiria sana kabla ya kufikia hatua ya kutoa uamuzi, lakini kwa bahati mbaya  wanaume wengi baada ya kutoa maamuzi huwa hawarudi nyuma.
Yaani wao ni mbele kwa mbele, tofauti na wanawake ambao huwa na uamuzi wa haraka lakini baada ya kukaa kwa muda na kufikiri hujiona wakosaji na kutaka kurekebisha uamuzi wao. Wakati huo wanakuwa wamechelewa.
Nimetanguliza hayo kwa makusudi kabisa, unapaswa kufahamu kuwa mume wako au mchumba wako unapomfanyia mambo asiyoyapendelea, hukuvumilia kwa muda lakini kumbuka kuwa akitoa uamuzi siyo rahisi kurudi nyuma, hiyo inamaanisha kuwa uwezekano wa kumkosa huwa mkubwa zaidi.
Unapaswa kujua vitu vinavyowakwaza wanaume, lakini pia unatakiwa kujua ni mambo gani hasa ambayo mumeo au mchumba wako anavichukia ili kukwepa kumchukiza na kusababisha mfarakano usio na lazima katika uhusiano wenu.
Pengine unaweza ukawa na maswali mengi sana juu ya hilo, inawezekana unafanya makosa bila kufahamu, sasa hebu tuliza ubongo wako katika vipengele vifuatavyo, utabagua pumba na nafaka.

KUTAKA MAISHA GHALI
Hili limekuwa tatizo kubwa sana kwa baadhi ya wasichana, yaani hata kama maisha yake ni ya kawaida lakini kwa mpenzi wake atayafanya yaonekane ghali sana! Akitolewa ‘out’ huagiza vyakula na vinywaji vya bei kali.
Tafsiri inayokuja hapo ni kwamba unakuwa na mpenzi huyo kwa ajili ya kujinufaisha tu na si penzi la dhati. Wanaume wengi hawapendi kabisa tabia hiyo, ila huvumilia kwa muda lakini tambua kuwa siku akitoa maamuzi utayajutia.
Kimsingi mwanamke mwenye matarajio ya kudumu na mwanaume wake, ikiwa ni pamoja na kuishi naye katika ndoa, hawezi kumkomoa mpenzi wake kwa kuhitaji vitu vya gharama kubwa ambavyo ni kama hasara kwa mpenzi wake.
Mwingine anaweza akapewa ofa ya kwenda kufanya ununuzi wa nguo, lakini akifika huko hufanya vurugu tupu! Huchagua nguo za bei mbaya kiasi kwamba inakuwa kero kwa mpenzi wake. Hata hivyo, unapaswa kumjua mpenzi wako alivyo na kipato chake, usijifanye wa ghali ishi maisha ya kawaida, labda kama atakushawishi kuchukua au kutumia vitu vya gharama kubwa.
Elewa kuwa kwa kufanya hivyo unamwogopesha mwanaume huyo kuwa na fikra za kutaka kuishi nawe katika ndoa, badala yake utaendelea kuwa chombo cha starehe siku zote.

UTEGEMEZI
Hii sasa imekuwa kama ‘fashion’ kwa sababu baadhi ya wanawake wanapokuwa na wapenzi wao, huona kama wamepata mahali pa kutatua matatizo yao yote! Nani amekwambia kuwa na mpenzi ndiyo sehemu ya kumaliza matatizo yako yote?
Bahati mbaya siku hizi wameongezewa majina, zaidi ya buzi kama ilivyozoeleka mwanzoni, siku hizi hufananishwa na kadi ya kuchukulia fedha benki, ambapo ukihitaji fedha unachukua wakati wowote!
Wanaume wa sasa hawapo hivyo, wanahitaji wanawake wenye malengo, ambao watakuwa na msaada mkubwa katika maisha yao. Hakuna mwanaume ambaye anategemea kuishi na mwanamke asiye na kazi wala mpangilio unaoelweka wa maisha yake ya baadaye.
Utakuta mwingine anamtegemea mpenzi wake kwa kila kitu, kila wakati mara simu yangu haina dola, mara sina fedha ya kula yaani matatizo chungu nzima. Sawa haikatazwi kumwambia mpenzi wako shida zako lakini ikizidi sana inakuwa kero!
Hivi kwani kabla ya kuwa naye ulikuwa unaishi vipi? Mwanaume anapogundua kuwa wewe ni tegemezi kwake kwa kila kitu, unampa wasiwasi kwamba huna nia ya kuwa naye katika maisha yake yote, badala yake umepanga kumfanya benki ya kuchotea fedha.
Mapenzi ya siku hizi kusaidiana, siyo kila kitu mpaka mpenzi wako, vitu vingine fanya mwenyewe, au kama mna utaratibu wa kusaidiana katika matatizo mbalimbali, si kila siku wewe ndiye mwenye matatizo!
Kwa ujumla haya ni mambo ambayo yanachukiwa na wanaume wengi. Kama unazo, acha mara moja ili uweze kumpata mwenzi ambaye atakuwa wako wa milele. Bila shaka nimesomeka. Ahsante kwa kusoma, tukutane wiki ijayo.
Joseph Shaluwa ni mshauri wa mambo ya mapenzi anayeandikia magazeti ya Global Publishers, ameandika vitabu vya True Love na Let’s Talk About Love vilivyopo mitaani.

1 comment:

Anonymous said...

Hii inasaidia sana.Its lovely