Kufuatia mwenendo mbovu wa timu yake katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara inayoendelea nchini, uongozi wa mabingwa watetezi wa ligi hiyo, Yanga, jana jioni uliwaweka 'kitimoto' makocha wake wawili, Mganda Sam Timbe na msaidizi wake Felix Minziro.Habari ambazo gazeti hili ilizipata jana mchana, kikao hicho cha dharura kilifanyika kwenye hoteli moja ya maeneo ya kati ya jiji (jina tunalo) na kiliitishwa na Kamati ya Utendaji ya Yanga inayoongozwa na Mwenyekiti wa klabu hiyo, Lloyd Nchunga.
Chanzo hicho cha habari kiliendelea kusema kwamba baada ya kumalizika kwa mechi yao ya juzi ya ligi dhidi ya Azam ambapo Yanga ililala kwa bao 1-0 huku wachezaji wake wakishindwa kuzitumia nafasi mbalimbali walizopata, ndipo viongozi wakataharuki na kutaka kujua undani zaidi kutoka kwa benchi hilo la ufundi.
"Kamati ya Utendaji imeitisha kikao cha dharura na itakutana na makocha wetu wawili ili kuwasikiliza na baadaye kufahamu chanzo cha matokeo hayo mabaya yanayoendelea," alisema mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga.
Jana mchana kulikuwa na habari kwamba Minziro anataka kubwaga manyanga na maamuzi hayo yanatokana na kile kilichodaiwa kuwa ni kukosa ushirikiano kutoka kwa Timbe.
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Ufundi ya Yanga (jina tunalo) aliliambia gazeti hili kuwa Minziro anakerwa na mambo mbalimbali yanayoendelea klabuni na pia
anashangazwa kwa kuona ushauri wake ukipuuzwa na Timbe.
Jana asubuhi, Timbe hakuonekana mazoezini na taarifa zinadai kwamba alishaueleza uongozi kuwa hajisikii vizuri na kutaka msaidizi wake, Minziro aendelee kukinoa kikosi hicho.
Taarifa nyingine zilidai kuwa Minziro amesikitshwa na uamuzi wa Timbe wa kung’ang’ania kumchezesha Hamis Kiiza dhidi ya Azam licha ya ukweli kwamba kiungo huyo wa kimataifa kutoka Uganda hakuwa amefanya mazoezi ya kutosha na wenzake.
Baada ya kumalizika kwa mechi dhidi ya Azam kwenye Uwanja wa Taifa, Minziro alidaiwa kuwaambia baadhi ya mashabiki kuwa ubishi wa Timbe ndio unaowaponza.
Alidaiwa kutoa mfano kuwa Kiiza hakuwa amefanya mazoezi ya kutosha na wenzake na aliwasili kikosini siku mbili kabla ya mechi yao dhidi ya Azam akitokea Msumbiji alikokuwa na timu yake ya taifa ya Uganda kushiriki michezo ya Afrika (All Africa Games).
Hata hivyo, Kiiza alipangwa kikosini na matokeo yake akacheza kwa kiwango cha chini, kinyume na vile alivyozoeleka.
Minziro alipotafutwa katika simu yake ya mkononi kuzungumzia taarifa hizo zikiwemo za kutaka kujiuzulu, hakuwa tayari kwa maelezo kwamba alikuwa kwenye kikao.
Miezi miwili iliyopita, Yanga ilionyesha kiwango cha juu na kutwaa taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) baada ya kushinda 1-0 katika fainali waliyocheza dhidi ya watani zao wa jadi, Simba.
Hata hivyo, Yanga iliyofanya usajili wa bei mbaya, ikiwa ni pamoja na kumtwaa nyota wa kimataifa kutoka Rwanda, Haruna Niyonzima ‘Fabregas’, imeendelea kupata matokeo mabaya katika mechi zake za hivi karibuni na hadi kufikia juzi, iliambulia pointi sita tu baada ya kucheza mechi sita, huku watani zao Simba wakiongoza katika msimamo wa ligi baada ya kufikisha pointi 14, wakiwa na mechi za idadi sawa na Yanga.
Kabla ya kufungwa na Azam juzi, Yanga walishinda mechi moja tu dhidi ya African Lyon na kufungwa katika mechi ya ufunguzi dhidi ya JKT Ruvu. Walionyesha kiwango cha wastani na kupata sare tatu dhidi ya Moro United, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment