ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 14, 2011

Aliyevimba mguu afariki

Daniel Mjema,Moshi
MGONJWA Abbas Abdallah, mkazi wa Kiru Ndogo, wilayani Babati mkoani Manyara, aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi, kufuatia kuvimba mguu wake mmoja, amefariki dunia.Abbas alifariki dunia dunia saa 4:00 usiku wa juzi akiwa katika chumba cha  wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu, baada ya madaktari kumfanyia upasuaji wa mguu wake.

Habari zilisema Abbas, alifariki saa 13 baada ya jopo la madaktari wa KCMC kumfanyia upasuaji ulioambatana na  kukata nyama zilizokuwa zimevimba.Baba mzazi wa marehemu, Abdallah Juma na kaka mkubwa wa marehemu, Seleman Abdalah, walilithibitishia Mwananchi jana kuhusu kufariki kwa kijana huyo.

“Ni kweli kwamba amefariki dunia na sasa ndio tumepata gari tunajaribu kama Mungu akipenda tuweze kumsafirisha leo (jana),  kwenda Kiru Ndogo kwa mazishi kesho (leo),”alisema baba yake.



Mzazi huyo alisema mmiliki wa Kampuni ya mabasi ya Hood, Mohamed Hood, ambaye ni mmoja wa wafadhili wakuu wa marehemu, ametoa gari la kumsafirisha hadi kijijini kwao kwa mazishi.Kaka wa marehemu, Seleman ambaye alikuwa akimuuguza marehemu, alisema mdogo wake walichukuliwa saa 3:00 asubuhi juzi na kupelekwa chumba cha upasuaji.

“Baada ya upasuaji ambao nilielezwa na wauguzi kuwa madaktari walimkata mguu ili kupunguza nyama, alipelekwa ICU ambako hakuna mtu anaruhusiwa kuingia,”alisema.“Ilipofika saa 1:00 usiku jana (juzi) nilikwenda nikamuona kupitia  vioo akiwa na mashine na moja iliyokuwa akipiga sana alarm (sauti),ikuelewa nikabaki kumuomba Mungu”.

Seleman alifafanua kuwa baadaye alipitiwa na usingizi na alishtuliwa na muuguzi mmoja ambaye alimwamsha na kumuuliza kama alikuwa amekwenda kumuona tena mgonjwa.

Kwa mujibu wa Seleman, muuguzi huyo ambaye hamfahamu kwa jina, alimwambia kuwa alipaswa kwenda tena kumuangalia mdogo wake ili kujua hali yake.

 “Nilikwenda ICU nikagonga mlango muuguzi akaja nikamwambia mgonjwa wangu anaendeleaje akaniambia kuna tatizo kidogo madaktari wanahangaika nalo,”alisema.

Alisema akiwa amesimama nje ya ICU aliona kitoroli kinachotumika kutoa maiti wodini kikiingizwa katika wodi hiyo na hapo ndipo aliposhuku kuwa mdogo wake hayupo tena duniani.“Baada ya muda mfupi kidogo akaja muuguzi mwingine akaniambia naitwa ndani na ndio wakaniambia mdogo wangu amefariki na wakanifunulia nikauona mwili wake,”alisema.

Siku moja kabla ya kufanyiwa upasuaji huo, Abbas akisema anaamini baada ya upasuaji huo angerejea katika hali yake ya kawaida na kuwa kama binadamu wengine.

“Kama sio Mwananchi  ningefia kijijini lakini nawashukuru wameandika habari zangu na nimepata wasamaria wema akiwemo Hood ambaye ni msaada mkubwa kwangu,”alisema kaka yake akimkariri mdogo wake.

Kwa mujibu wa ndugu, huyo mdogo wake aliwahi kusema kuwa haelewi cha kumlipa Hood ambaye amegharamia chakula na gharama za matibabu ikiwamo sh7 milioni ambazo alisema ni gharama kwa ajili ya upasuaji huo.

Alisema tangu ugonjwa huo umtokee mwaka 2005 ulipoanza kama uvimbe mdogo wa kawaida, hajawahi kupata msaada kama alioupata baada ya Mwananchi kutoa habari zake.Lakini pamoja na matarajio ya Abbas kurejea katika hali ya kawaida ya binadamu, ndoto yake imeyeyuka kama mshumaa wakati madaktari wakijaribu kufanya ndoto yake kutimia.

Kufikishwa hospitalini kwa marehemu, kulitokana na jitihada kubwa zilizofanywa na kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), kuandika habari za Abbas.

Baadaye MCL kwa kushirikiana na Benki ya CRDB Limited, walimfunguliwa akaunti Abbas katika Tawi la Moshi ambayo ilitumiwa na wasamaria wema kupitishia fedha za msaada.

Katika kufungua akaunti hiyo,CRDB walilegeza  masharti ya kufungua akaunti yanayotaka mteja kufika mwenyewe benki na ikatoa msaada wa sh150,000 za kufungulia akaunti.

No comments: