ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 14, 2011

Kada CCM atamani upinzani ushinde 2015


Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa (kushoto) akimsaidia Kada wa CCM, Mustafa Sabodo kunyanyuka kwenye kiti nyumbani kwa kada huyo Upanga, jijini Dar es Salaam jana. Picha na Michael Jamson
AWAMWAGIA MAMILIONI YA MSAADA CHADEMA, ASIFU MSIMAMO WA DK SLAA
Geofrey Nyang’oro
KADA wa CCM, Mustafa Sabodo ameahidi kuchimba visima 200 katika majimbo yote ya wabunge wa Chadema nchini, huku akieleza kuwa angependa kuona upinzani unachukua nchi mwaka 2015.Sabodo ambaye ni kada wa CCM tangu enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyarere, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akipokea mpango wa uchimbaji visima hivyo kutoka kwa Katibu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa.Kauli hiyo ya Sabodo ambaye tayari katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana aliisaidia Chadema Sh100 milioni za kampeni, imekuja kipindi ambacho CCM, inakabiliwa na mpasuko kutokana na siasa za makundi.

Wakati CCM ikikabiliwa na kipindi hicho kigumu kisiasa, jana Sabodo ambaye aliahidi kuendelea kukisaidia Chadema, alisema “Ningependa kuona upinzani ukichukua nchi mwaka 2015”.

Jana Saa 4:00 asubuhi, Dk Slaa akiongozana na Mkurugenzi wa Mambo ya  Bunge wa Chadema, John Mrema walifika nyumbani kwa Sabodo kwa  lengo la kukabidhi mchakato wa utekelezaji wa mradi huo wa visima na pia kumshukuru kada huyo wa CCM  kwa misaada yake kwa chama hicho.

Katika mazungumzo hayo, Sabodo alimhakikishia Dk Slaa kwamba ataendelea kusaidia chama hicho katika miradi mbalimbali, inayohusu wananchi hususani suala la maji na elimu.

Sabodo alisema  elimu ni muhimu katika maisha ya binadamu, lakini maji pia ni uhai, kwakuwa bila maji hakuna mtu anayeweza kufanya chochote.

Mradi wa Sh2.5 bilioni
Sabodo alisema ametenga Sh2.5 bilioni kwa ajili ya kuchimba visima vya maji virefu na vifupi 700 katika maeneo yenye ukame,  huku visima 200 kati ya hivyo vikielekezwa katika majimbo 23 wanakotoka wabunge wa Chadema na Jimbo la Igunga. Chadema kina jumla ya wabunge 48 na 25 kati yao ni wa Viti Maalum.

Alifafanua kwamba anatoa msaada wa maji kwa sababu anatambua umuhimu wa huduma hiyo kwa jamii huku akisisitiza kwamba maji siyo anasa bali ni hitaji la  lazima.

Kuhusu sababu ya kujenga urafiki na Dk Slaa Sabodo alisema: “Mimi siyo kwamba navutiwa na wewe Dk Slaa hata nikaona umuhimu wa kutoa msaada kwa Chadema, ninavutiwa na Principle (Kanuni) zako na chama chako,”alisema Sabodo.

Michango hiyo ya Sabodo kwa Chadema iliwahi kuibua manung'uniko kwa baadhi ya makada wa CCM, lakini aliyekuwa Katibu Mkuu, Yusuph Makamba, aliwahi kuliambia gazeti hili kwamba, "Siyo vibaya Mkristo kumsaidia Mwislam, ndiyo ubinadamu," hivyo haoni tatizo kwa Sabodo kusaidia upinzani.

Dk Slaa anena
Kwa upande wake, Dk Slaa alisema chama hicho  kinatarajia kuchimba visima vya maji 11 katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora ikiwa ni wiki takriban mbili tangu kumalizika kwa uchaguzi mdogo wa jimbo hilo uliofanyika Oktoba 2.

Dk Slaa alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kukabidhi mchanganuo wa namna walivyogawa mradi wa utekelezaji wa visima 200, vilivyotolewa na Sabodo   kwa lengo la kuchimbwa katika majimbo tofuati wanakotoka wabunge wa Chadema.

Alisema lengo la kutekeleza mradi huo wa maji katika Jimbo la Igunga limetokana na  ziara aliyoifanya katika vijiji 98, vilivyopo katika jimbo hilo na kugundua wananchi wake wanakabiliwa na tatizo kubwa la maji.

“Katika mpango kazi wetu, tumepanga kuchimba visima 11 katika Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, hii  imetokana na ziara yangu katika vijiji 98 ambapo niligundua kuwa wakazi hao wanakabiliwa na  tatizo kubwa la maji,”alifafanua Dk Slaa.

Chadema kilishika nafasi ya pili katika uchaguzi mdogo wa jimbo hilo, kwa aliyekuwa mgombea wake, Joseph Kashindye kupata kura 23,260 sawa na asilimia 44.3, nyuma ya mgombea wa CCM, Dalaly Kafumu aliyeshinda kwa kura 26,484 kati ya 52,487 halali zilizopigwa, sawa na asilimia 50.4.

Dk Slaa alimshukuru Sabodo kwa msaada wake wa kukusudia kuchimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali nchini, yanayokabiliwa na uhaba akisema kitendo hicho ni cha utu kwa kuwa maji ni uhai.

“Nitoe shukrani kwa niaba ya wabunge ninaowawakilisha kufuatuia msaada wako wa kukusudia kuchimba  visima   200 vya maji katika majimbo yao, ni maelfu ya watu watanufaika na msaada huu,”alisema Dk Slaa na kuongeza:,

“Sisi tumekuja kukushukuru kwa niaba ya wabunge wetu na wananchi, lakini pia wabunge wangu watakuja mmoja mmoja kukushukru wewe ni baba yao. Ushindi walioupata ulitokana pia na msaada wako mkubwa wa kifedha wakati wa kampeni,”alisema Dk Slaa.

Kwa upande wake, mchumba wa Dk Slaa, Mushumbushi, alishukuru msaada huo wa maji kutoka kwa Sabodo akisema utawasaidia wanawake na watoto.

“Watu wanaopatwana athari nyingi kutokana na tatizo la maji ni wanawake na watoto, ni wanawake ndio hupatwa na matatizo ya kubakwa wanapokwenda umbali mrefu kuteka maji. Pia ukame wa maji umevunja hata baadhi ya ndoa,”alisema Mushumbushi.

Wamzungumzia Nyerere
Akizungumzia kumbukumbu ya kifo cha baba wa taifa Mwalimu Nyerere, Sabodo alisema kwa miaka 12 Taifa limeshuhudia maadui wa taifa wakiongezeka.“Baba wa taifa aliacha maadui wakuu watatu, ujinga, mardhi na umasikini. Lakini sasa badala ya kupungua, wameongezeka wawili na kufanya idadi hiyo kuwa watano,”alisema Sabodo.

Sabodo aliwataja maadui hao wapya kuwa ni wizi wa mali za umma wanaotokana na  mmomonyoko wa maadili pamoja na    ufisadi.

Katika mazungumzo yake, Sabodo hakusita kueleza kuwa hali ya sasa ya uadilifu kwa viongozi imeshuka kwa kiwango kikubwa na kusisitiza kwamba, vitendo hivyo ndivyo vinavyoliangamiza taifa.

Kwa upande wake, Dk Slaa alisema kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere inaadhimishwa kwa utani kutokana na viongozi wengi wakiwemo wenye mamlaka kushindwa kufuata maadili ya mwasisi huyo  wa taifa.

Alisema kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere haipaswi kusherehekewa kama siku ya shamrashamra  na badala yake, kwa kufuata maadili na msingi aliyosimamia.


Mwananchi

No comments: