ANGALIA LIVE NEWS

Friday, October 14, 2011

Mkulo, Zitto hapatoshi


Waziri Kivuli wa Fedha na Uchumi, Zitto Kabwe akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jana katika Ofisi ndogo za Bunge, jijini Dar es Salaam. Picha na Edwin Mjwahuzi
Waandishi Wetu
HATUA ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe kutaka vyombo vya dola kufanya uchunguzi wa kina kwa kitendo cha Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo kusitisha utendaji wa Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) kwa madai ya kulinda maslahi yake binafsi, imezua mvutano mkali baina yake na waziri huyo.

Oktoba 10, mwaka huu Mkulo alitoa maelekezo ya kusitishwa kwa Bodi ya Wakurugenzi ya CHC, wakati bodi hiyo ikisubiri kupokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG), Ludovick Utouh kufuatia ukaguzi uliofanywa kutokana na kuwapo kwa tuhuma za ufisadi ndani ya shirika hilo la umma.

Zitto katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, alimtaka Mkulo ajiuzulu ili kupisha uchunguzi huru dhidi ya tuhuma hizo.

Zitto alisema anapendekeza uchunguzi wa kina ufanyike kwa kutumia vyombo vya dola na hasa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuhusu tuhuma dhidi ya Mkulo na alazimishwe kisheria kujibu maswali ya wakaguzi kuhusu tuhuma dhidi yake.Hata hivyo, Mkulo katika mazungumzo yake na Mwananchi amekanusha tuhuma hizo akisema kuwa Zitto ana maslahi binafsi ndani ya CHC, hivyo kumtaka mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini (Chadema) kuueleza umma sababu za kushupalia suala hilo.

Mkulo alisema anashangazwa na hatua ya Zitto kufuatilia matokeo ya uchunguzi wa CAG kwani mbunge huyo aliwahi kusema bungeni kwamba hakukuwa na sababu ya CAG kufanya uchunguzi ndani ya CHC kwa madai kwamba hatua hiyo ilikuwa ni uonevu dhidi ya Kaimu Mkurugenzi alisimamishwa kazi, Methusela Mbajo.

Hoja ya Zitto
Zitto ambaye pia ni Waziri Kivuli wa Fedha, pia alitaka ripoti ya ukaguzi huo unaofanywa na Kampuni ya Ersnt&Young iliyopewa kazi na CAG, iwasilishwe kwa Spika wa Bunge ili ijadiliwe bungeni badala ya kukabidhiwa kwa waziri huyo ambaye ni mtuhumiwa.

 Zitto alisisitiza, “Katika uchunguzi wake CAG kupitia kampuni ya Ernest&Young walitaka kufanya mahojiano na Waziri wa Fedha juu ya tuhuma mbalimbali zinazomkabili ndani ya CHC, lakini hawakufanikiwa,”alisema Zitto.

Waziri kivuli huyo alisema  Mkulo alikataa kuhojiwa na wakaguzi na badala yake akaandika barua  yenye kumbukumbu TYC/B/70/2/03 ya Oktoba 8 mwaka huu, yenye kujibu tuhuma moja tena kwa juu juu, kuhusu yeye kuliamuru shirika kuuza kiwanja cha shirika bila kufuata taratibu za kisheria.  “Wakati uchunguzi unaendelea ndugu Mustafa Mkulo asimamishwe kazi ya uwaziri wa Fedha hadi hapo uchunguzi utakapokamilika,”alisisitiza  Zitto.

Zitto alisema wakati Mkulo akikanusha kuliagiza  CHC kuuza kiwanja kwa mtu anayemtaka,  yeye (Zitto) anao ushahidi tosha wa nyaraka kutoka Hazina, unaonyesha waziri huyo mwenye dhamana ya fedha na uchumi alitoa agizo hilo.  Waziri huyo kivuli alisema katika kuthibitisha hilo, anazo nyaraka ambayo ni  TYC/A/290/13/4 ya Machi 9 mwaka huu ambayo inawagiza CHC kutekeleza agizo la Waziri wa Fedha kuhusu kiwanja namba 10 kilichopo barabara ya Nyerere jijini Dar es Salaam.
  ”Vilevile, nina ushahidi wa mkutano uliofanyika huko Morogoro Hotel kati ya Waziri wa Fedha na mwenyekiti wa bodi ya CHC kuhusu jambo hilo,” alifafanua  Zitto.  Zitto alisema siku mbili baada ya kumjibu CAG, Mkulo aliamua kutengua uamuzi wake wa kuongeza muda wa bodi ya CHC mpaka mwezi Desemba mwaka huu na hivyo kuivunja.

Kuvunjwa kwa bodi Zitto alisema kitendo cha Waziri kuiamuru bodi kumsimamisha kazi aliyekuwa mkurugenzi mkuu wa CHC na baadaye kuivunja bodi hiyo wakati inasubiri taarifa ya CAG, ni kuingilia uchunguzi na pia matumizi mabaya ya ofisi ya umma ili kulinda maslahi binafsi.  “Ni dhahiri akiendelea kuwa Waziri wa Fedha ataharibu uchunguzi,”alisema Zitto.  Zitto alisema  ni muhimu Rais Jakaya Kikwete akaangalia kama kweli anaitendea haki nchi na uchumi wake, kwa kuendelea kuwa na Waziri wa Fedha ambaye  anasema uongo bungeni.

 “Ni waziri mwenye kutumia ofisi yake vibaya kwa kuchukua maamuzi yanayoingilia uchunguzi unaomhusu ili kujilinda,”alisema Zitto.  Alisema  kutokana na ukweli kwamba suala la CHC lilianzia bungeni na hata waziri mwenyewe kukiri kuwa taarifa ya uchunguzi inapaswa kuwekwa wazi, hivyo ni muhimu ikapelekwa kwa Spika wa Bunge kwa hatua zaidi.

Lakini wakati CAG akiwa katika hatua za mwisho kukamilisha ripoti yake ambayo kimsingi ilipaswa kukabidhiwa kwa bodi ya CHC, uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa Mkulo amevunja bodi hiyo iliyokuwa ikioongozwa na Profesa Hamis Kahigi ambaye pia ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokine cha Kilimo (SUA), kabla ya kumaliza muda wake wa nyongeza ambao ulipaswa kumalizika Desemba 31, mwaka huu.

Mkulo ajibu mapigo
Akizungumzua na Mwananchi kwa simu kutoka Kilosa mkoani Morogoro jana jioni Mkulo alimshambulia Zitto akisema mbunge  huyo “ana mambo yake binafsi”.

“Kwanza ni strange (ni ajabu) ripoti ya CAG haijatolewa, na kama mnakumbuka haya mambo yalianzia bungeni, kama mbunge anafikia mahali anazungumza mambo haya mbele ya press (vyombo vya habari) nadhani amekiuka taratibu,”alisema Mkulo na kuongeza:

“Kwa jinsi ya utaratibu ulivyo, Serikali inawajibika kutoa kauli bungeni kwa sababu huko ndiko suala hili lilikoanzia, hivyo ingekuwa busara kama mtu anayefahamu taratibu hizi angesubiri huko”.

“Kama nilivyosema jana (juzi) bodi ya CHC ilikwishamaliza muda wake na mimi kama waziri nilikuwa nimewapa muda wa nyongeza, lakini baada ya Bunge kuongeza muda wa miaka mitatu wa utendaji wa shirika hilo, nilimwandikia Rais kumuomba ateue Mwenyekiti, baada ya kufanya hivyo, bodi hii haiwezi kuendelea kuwapo,”alisema Mkulo.

Alisema ripoti ya CAG kwa vyovyote itawasilishwa bungeni kutokana na suala lenyewe lilivyo, na kwamba kauli ya Zitto kwamba kusitishwa kwa bodi ya CHC ni njama za kutaka kuteka ripoti hiyo si za kweli.

“Kwanza Zitto hafahamu chanzo cha ukaguzi wa CAG, Waziri Mkuu (Mizengo Pinda) alielekeza ufanyike ukaguzi kutokana na maono kadha wa kadha aliyoyabini, mimi nikaiagiza bodi itekeleze agizo hilo, sasa atasemaje kwamba mimi nataka ripoti ambayo kimsingi uchunguzi wake haukuanzia kwangu?,”alihoji Mkulo na kuongeza kwamba hilo linathibitisha kwamba Zitto hana uelewa kuhusu suala hilo.

Waziri huyo mwenye dhamana ya fedha na uchumi, pia alihoji sababu za Zitto kufuatilia kwa karibu kazi zinazofanywa na CAG na kusema kuwa “pengine muulizeni ana maslahi gani katika suala hili”.

“Haiwezekani mtu ambaye siyo mtumishi wa Serikali wala siyo waziri, jana, leo, kesho, keshokutwa upo tu unafuatilia CAG anafanya nini, ameandika ripoti gani, hata kabla ripoti yenyewe haijatoka, lazima mtu wa aina hiyo ana special interest (maslahi maalum), angeweka wazi maslahi yake katika hili badala ya kukimbilia kwenye press kuchafua wenzake,”alisema Mkulo.

Chimbuko la mzozo
Katika Mkutano wa Nne wa Bunge, Mkulo aliingia katika mvutano na Zitto baada ya waziri huyo kumtuhumu mbunge huyo na Kamati yake kwamba walihongwa ili kutetea nyongeza ya muda wa CHC, tofauti na mawazo ya Serikali ya kutaka kufutwa kwa shirika hilo.
Baada ya tuhuma hizo, Zitto aliapa bungeni kwamba kama uchunguzi utathibitisha yeye au wajumbe wa POAC wamehongwa, angejiuzulu uenyekiti na ubunge na kumtaka Waziri Mkulo nae atoe kiapo chake bungeni kama atajiuzulu akibainika amefanya ufisadi ndani ya CHC.  Mkulo akijibu swali hilo alishindwa kula kiapo na Spika wa Bunge, Anne Makinda akamkumbusha kuhusu kula kiapo kama atajiuzulu, lakini waziri huyo aligoma kufanya hivyo.

Mwananchi

No comments: