ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 18, 2011

Dk. Malecela aukwaa ujumbe Bodi IANPHI

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Dk. Mwele Malecela, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Chama cha Kimataifa cha Afya ya Jamii (IANPHI)
Dk. Malecela, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Programu ya Kitaifa ya Udhibiti wa Matende na Mabusha nchini alichaguliwa katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika mwishomi mwa Septemba, mwaka huu, huko Helsinki, nchini Finland.

Amefanya kazi ya utafiti kwa miaka 24 sasa; na anakuwa mwanamke wa kwanza kuwa mjumbe wa bodi hiyo.
IANPHI ni chama cha Kimataifa cha Afya ya jamii kinacholenga kuboresha na kuendeleza mifumo ya afya ya jamii ili kuzilinda jamii za nchi wanachama dhidi ya majanga yatokanayo na milipuko ya magonjwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya IANPHI, Dk. Malecela ni miongoni mwa wajumbe watano wa bodi hiyo watakaohusika na uboreshaji wa mifumo ya sera ya nchi wanachama; pamoja na kuimarisha mifumo ya afya ya jamii na miundombinu yake kwa nchi wanachama kupitia taasisi za taifa za afya ya jamii za nchi husika.
Wajumbe wengine wa bodi hiyo, ni Reinhard Burger, ambaye ni Rais wa Taasisi ya Ujerumani ya Robert Koch; Rajae El Aouad (Mkurugenzi wa Taasisi ya Taifa ya Usafi ya Morocco); David Butler-Jones (Mkurugenzi wa Shirika la Afya ya Jamii la Canada); na Justin McCracken (Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Hifadhi ya Afya la Uingereza).
Akizungumza katika mahojiano maalum na NIPASHE baada ya kurejea nchini, Dk. Malecela alisema taasisi yake inatarajia kuendeleza utafiti wa ushirikiano na IANPHI katika maeneo ya magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, saratani, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.
Alisema katika tafiti hizo, IANPHI itashirikiana na NIMR katika ufuatiliaji wa viashiria vya magonjwa yasiyo ya kuambukiza na kujenga uwezo wa wanasayansi wa Tanzania kupitia programu maalum ya kujenga uwezo wa watafiti wa afya ya jamii inayoendeshwa chini ya IANPHI.
CHANZO: NIPASHE

No comments: