Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, alisema kuwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo iliyokutana Oktoba 10 iliamua kufanya marekebisho kwenye kamati zake na kuongeza wajumbe kwenye kamati tano walizounda.
"Marekebisho haya tumeyafanya kwa ajili ya kuleta maendeleo klabuni kwetu, tunaamini kwamba kwa kushirikiana na wajumbe walioteuliwa kwenye kamati hii tutafikia malengo yetu kwa kuwa Simba inategemea mawazo ya watu wengi," alisema Rage.
Aliongeza kuwa kamati ya utendaji ya klabu hiyo imemteua Zitto kuwa mjumbe wa kamati ya fedha inayoongozwa na Geofrey Nyange 'Kaburu' (mwenyekiti)na makamu wake ni Adam Mgoi.
Wajumbe wengine kwenye kamati hiyo ni pamoja na Said Pamba, Kifiri, Juma Pinto, Abdul Mteketa na Mbunge wa Kilwa Kaskazini, Murtaza Mangungu.
Mfadhili wa zamani wa klabu hiyo, Azim Dewji, ameteuliwa kuwa makamu mwenyekiti wa kamati ya mashindano inayoongozwa na Joseph Itang'are ‘Kinesi’ na wajumbe ni Jerry Ambe, Swedi Mkwabi, Hassan Hasanoo, Mohamed Nassoro, Amos Makala, Richard Ndasa (Mbunge wa Sumve) na Suleiman Zacharia.
Katika kamati ya ufundi, mtangazaji wa redio, Ibrahim Masoud 'Maestro' ndiye aliyeteuliwa kuongoza kamati hiyo, akiwa na makamu wake Evans Aveva na wajumbe ni Dan Manembe, Khalid Abeid, Musley, Mulam Ng’hambi, Said Tuli, Rodney Chidua na Patrick Rweyemamu.
Kamati ya utendaji ya Simba imemuacha Zacharia Hans Poppe katika nafasi yake ya kuongoza kamati ya usajili, akisaidiwa na makamu wake Kassim Dewji na wajumbe ni Francis Waya, Crecentius Magori, Salim Abdallah, Collins Frisch na Gerald Lukumay.
Kamishna Msaidizi wa Polisi, Jamal Lwambow na Peter Swai wameteuliwa kuongoza kamati ya nidhamu ya klabu hiyo na wajumbe ni kamanda wa mkoa wa Polisi wa Kinondoni, Charles Kenyela, Evody Mmanda na Chaurembo.
Rage aliongeza kuwa uongozi wa klabu hiyo haubagui watu katika kuiletea maendeleo klabu yao na wanaamini kuwa kamati walizounda zitawasaidia katika kufikia malengo yao.
YONDANI MATATANI
Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu hiyo umempa nafasi ya mwisho beki wao wa kati, Kelvin Yondani na kumtaka aandike barua ya kutoa maelezo na pia msimamo wake kwa klabu hiyo baada ya kutoonekana katika mazoezi ya timu hiyo kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, mwenyekiti wa klabu hiyo, Ismail Aden Rage, alisema kuwa uongozi wake hauna ugomvi na mchezaji huyo na wanashangaa kutomuna mchezaji huyo mazoezini kwa kipindi chote hicho na tena bila kutoa taarifa.
Awali, mara baada ya mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) ‘wekundu’ hao na watani zao wa jadi, Yanga kulikuwa na taarifa kuwa mchezaji huyo anatuhumiwa kuihujumu timu yake.
Hata hivyo, Rage alishakanusha mara kadhaa uvumi kwamba wanamtuhumu Yondani na kusisitiza kuwa si yeye tu, bali hakuna mchezaji wao yeyote wanayemtuhumu kwa kucheza chini ya kiwango au kuwahujumu.
"Hatuna ugomvi na Yondani wala mchezaji yeyote, sisi pia tunashangaa ni kwa nini hajahudhuria mazoezi kwa kipindi cha wiki nne sasa… yeye (Yondan) bado ni mchezaji wetu kwa sababu ana mkataba na sisi," alisema Rage.
"Tunampa nafasi nyingine kutueleza kinachomsibu kwa sababu hatuwezi kumuadhibu kisheria bila kujua ana tatizo gani. Tunamtaka awasilishe maelezo yake kabla ya sisi kumchukulia hatua zaidi za kisheria," aliongezea Rage.
Aidha, Rage alisema kuwa kwa hatua ya sasa, wanaweza kumuadhibu Yondani na hata kumfukuza kwenye timu hiyo na kutoa taarifa kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na pia Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), ambao nao wanaweza wakamuongezea adhabu kwa mujibu wa kanuni.
Hata hivyo, Rage alisema kuwa wanasita kumchukulia hatua hiyo kali kwavile hawataki kumharibia (Yondani) maisha yake ya soka na ndiyo maana wamempa nafasi ya kutoa msimamo wake.
"Endapo sisi tutamfukuza, kanuni za FIFA zinaweka wazi kuwa na wao wanaweza wakamuadhibu kwa kumfungia ndani ya kipindi cha miaka miwili na hapo hatasajiliwe na klabu nyingine bila ridhaa ya timu iliyomuadhibu," alisema Rage.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment